HAKUWA NA KARATASI
Adeladius Makwega-MBAGALA
Salumu Abdallah Lilingani ni miongoni mwa watu wa mwanzo mwanzo kuishi katika Kijiji cha Mbagala miaka mingi kabla ya uhuru wa Tanganyika. Baba wa Salumu aliyefahamika kama Abdalla Lilingani kwa asili ni jamii na watu wanaotokea huko Nyasa, Malawi ya sasa.
Alitoka huko Nyasa na kufika Rufiji kutafuta maisha, hilo ni jambo la kawaida sana sana kama ilivyo kwa vijana wengi wa leo hii. Alipofika Rufiji alikaa hapo akaoa mwanamke wa Kirufiji, Inavyoonekana Abdalla Lilingani alimzaa Salumu Lilingani kwa mwanamke wa Kinyasa ambaye familia hii haina kumbukumbu zake.
Akiwa Rufiji Abdallah Lilingani alioa mwanamke mwingine wa Kirufiji, maisha ya ndoa yalianza huko mke wa Abdalla akimlea Salumu Abdallah huko huko Rufiji. Abdallah Lilingani alikaa Rufiji kwa kipindi kifupi sana akaambiwa kuwa anaweza kwenda Tanga kutafuta maisha, maana alijulishwa kuwa huko kuna kazi nyingi zinaweza kumuingizia fedha. Aliwaaga wakweze na mkewe na kumuacha mtoto wake Salumu na hii familia ya Warufiji.
Abdallah aliishi Tanga kwa muda, huku akiganga njaa, alimkumbuka mkewe Mrufiji aliyemuacha na mtoto wake Salumu huko kwa shemeji zake Wandengereko. Kumbuka msomaji wangu Salumu analelewa ujomba wa kambo, Jambo hili linaweza kuwa geni sana kwa jamii ya leo lakini Salumu alipata ngekewa hiyo. Kwa msomaji wangu naomba tilia maanani kitendo hicho cha kiungwana ambacho leo ni nadra sana kutokea lakini jamii zetu zina wajibu wa kujifunza hilo.
Wajerumani walipofika ukanda huo walisimuliwa kisa cha Salumu aliyeachwa na baba yake aliyeelekea huko Tanga, walivutiwa sana na kisa hicho na walimchukua kijana huyu kama yatima na kumlea wao wenyewe, baada ya mama yake wa kambo kupata mume mwingine. Familia ya ujomba wa kambo ya Salumu wangeweza hata kumuua lakini walimkabidhi kwa wamisionari.
Abadallah Lilingani alikaa Tanga kwa muda akaamua kurudi Rufiji kuitazama familia yake, alipofika huko alikuta mkewe ameolewa na mume mwingine na mtoto wake yupo na Wajerumani huku wakaimfundisha mambo mbalimbali ya kazi za mikono ikiwamo upishi na baadaye Salumu akafuzu na kuwa mhudumu wa makazi ya Wajerumani. Abdallah alifariki dunia huko huko Rufiji na kuzikwa, pengine mapenzi yalimuumiza sana kwa mkewe kupata mume mwingine.
Maisha ya Salumu na Wajerumani yaliendelea, walimpenda sana wakaamua kwenda naye Ujerumani akifanya kazi huko ughaibuni na pengine Salumu Abdallah Lilingani ni miongoni mwa Watanganyika wa kwanza kwanza kufanya kazi Ujerumani. Mtu kwao akiwa likizo alikuwa akirudi nyumbani kwao Tanganyika na kwa kuwa Rufiji ni mbali na Dar es Salaam alikuwa kila akifika Tanganyika alinunua nyumba, viwanja kadhaa na mashamba mengi likiwamo shamba lililopo katikati ya Mbagala Kizuiani/Mangaya/Kizinga jirani na shule ya Msingi Mbagala. Kumbuka huko Rufiji Salumu hakuwa na ndugu wa damu bali ndugu zaidi ya ujomba wake wa kambo tu.
Wakati huo Tanganyika ukoloni umepamba moto, Salumu akawa mkubwa, amekaa na wamisionari kwa muda mrefu na ameishi nao hadi Ujerumani. Tanganyika ikapata mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kati na mradi huo ulikamilika vizuri. Salumu sasa ni kijana mkubwa anayejitambua vizuri, huku akiwa na elimu mbalimbali kutoka kwa wamisionari hao waliomchukua kutoka Rufiji. Akawaomba wamisionari hao arudi nyumbani kwao Tanganyika, akakubaliwa na kufungusha vilago. Kutokana na elimu yake Salumu akapata kazi ya Mkuu wa Kituo cha Garimoshi kituo cha Tabora.
Akiwa Tabora alikuwa kijana mwenye nguvu zake, mtanashati, mwenye heshima kwa wakubwa na wadogo, Wanyamwezi walimpenda sana na wazee wa Kinyamwezi wakamuita chemba wakamwambia jambo ndugu Salumu ,
“Ndugu yetu wewe ni kijana, uliyekamilika hauwezi kuishi hapa bila mke, kama unaishi bila mke huko ni kuishi kihuni, katika kabila letu kitendo hicho ni kosa kubwa, lazima uoe mke sasa hivi.”
Kweli wazee hao waliompatia ujumbe huo walimpa binti yao na kumuoa wakati huo huo binti huyu wa Kinyamwezi aliyeitwa Binti Goha, mtoto wa Mzee Goha. Stesheni Masta ni mtu mkubwa sana , yeye ni lodi wazee wa Kinyamwezi walichangamkia fursa. Kwa hiyo maisha yaliendelea na kuzaa naye binti huyo wa Kinyamwezi watoto kadhaa nao hao Wanyamwezi ndiyo wakawa ndugu zake wa karibu kuliko Wandengereko wa Rufiji waliomlea.
Salumu alifanya kazi na Reli kwa miaka kadhaa na baadaye kustaafu na kurudi Dar es Salaam kwa kuwa alipokaa Ujerumani alipewa zawadi ya vifaa kadhaa vya kilimo bora aliamua kuishi Mbagala eneo lenye bonde kulima kilimo cha bustani huku nyumbani zake kadhaa za katikati ya jiji hili akizipangisha.
Maisha ya Mbagala yaliendelea vizuri na Serikali ya Mwalimu Nyerere ikipambana na kuleta maendeleo ya watu wake. Mwaka 1978 eneo la Tandika/Temeke–Azimio kulikuwa na ujenzi wa barabara za mitaa na nyumba kadhaa zilivunjwa, kulipwa na kutafutiwa maeneo mengine.
Watu kadhaa waliokuwa na mashamba eneo la Mbagala waliombwa karatasi za umiliki wa mashamba hayo kama ni za kisheria. Mongoni mwao ni Jaji Kimicha na Mzee Salumu Abadallah Lilingani. Jaji Kimicha kwa kuwa alikuwa ni mtu wa mahakama anatambua sheria eneo hilo lilikuwa na ushahidi wa umiliki wake katika karatasi lakini Salumu Abadallah Lilingani alikuwa hana umiliki wa karatasi bali umiliki wa kawaida tu.
Eneo hilo likachukuliwa na serikali na kugawiwa viwanja kwa wakazi hao wa Azimio huku likitengwa eneo la huduma kijamii kama vile nyumba za ibada na zahanati/kliniki.
Salumu Abdallah Lilingani alifariki dunia mwaka 1983 na eneo lake alilonunua kwa fedha ya jasho lake alilofanyia kazi nchni Ujerumani sasa linatusaidia watu wengi wa Mbagala na hata maeneo jirani- mama zetu, dada zetu na wake zetu wanajifungulia watoto wetu katika kiliniki hiyo, shule za msingi zimejengwa na hata barabara zimepita katika ardhi hiyo nao ukoo wa Lilingani ukiwa na ardhi ndogo kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga na makazi tu.
Wapo wanaomiliki ardhi hii ya Mbagala kwa karatasi na mwaka 1978 walipona na kubaki nazo na kumiliki hadi leo hii, la kusikitisha nina hakika ndugu hawa wanabeba ndugu zao wanakwenda kujifungua katika kiliniki ile iliyopo katika ardhi ya Salumu Bin Lilingani na hata watoto na wajukuu wao wakisoma katika shule zilizopo katika eneo hilohilo.Je maeneo yao walioachiwa kwa karatasi zinazoheshimika sana je wanayatumia kwa nini na Kwa manufaa ya nani?
Naendelea kulipiga chapuo la kuhakikishwa kata ya Mbagala inajengewa shule ya Sekondari yake mapema sana na leo hii matini haya namkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndugu yangu Amos Makala.
“Kaka Amosi Makala, leo hii mwanakwetu nimemsimulia ndugu Salumu Abadallah bin Lilingani-Mnyasa/Mndengereko /Mnyamwezi kwa kitendo chake cha utu. Ndugu huyu angeweza kupinga kupokonywa ardhi hiyo lakini alikuwa muungwana na uungwana wake unanufaisha wengi hata wale waliobaki na maeneno yao, ati kisa wana karatasi tu, ndugu yetu na kaka yangu Makala Kata ya Mbagala inahitaji shule ya Sekondari tusaidie kaka..”
Kwa maantiki ya kisa cha Salumu bin Lilingani hata kama hakuwa na karatasi ya ardhi hiyo, kitendo ch ardhi yake kunufaisha wengi ni jambo jema lazima tumkumbuke na kumpa haki yake ndugu huyu dhidi ya mtu yoyote yule hata kama ana karatasi ya kisheria kumiliki ardhi hiyo na ndiyo maana mwanakwetu nimeamua kusafiri safari ndefu ya simulizi ya ndugu huyu tangu alipotoka Nyasa, akaenda Rufiji, akaenda Ujerumani , akenda Tabora akarudi Dar es Salaam na hadi anafariki dunia mwaka 1983
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment