Adeladius Makwega-MBAGALA
Katikati ya mwaka 1980-1981 wazazi wangu walikuwa walimu wa Shule ya Msingi Berege, Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma. Msomaji wangu umbali kati ya Kijiji cha Berege na Gulwe ilipo stesheni maarufu sana na gari moshi ni kilometa 16 na umbali kati ya Gulwe na Mpwapwa Mjini ni Kilometa 12, ndiyo kusema kutoka Berege hadi Mpwawa ni Kilometa 28.
Stesheni ya gari moshi ya Gulwe wakati huo ilikuwa maarufu mno kwani hata sisi na wazazi wetu tulikuwa tunafika hapo tukingoja kupanda gari moshi kuelekea Dar es Salaam. Baba yangu anayefahamika kama Francis Fidelis Makwega wakati huo alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Berege na mama yangu mwalimu Doroth Hezron Mlemeta akiwa mwalimu.
Kama ilivyo leo hii, Mpwapwa ya wakati huo pia ilikuwa na wafugaji wengi wa mbuzi, kondoo na ng’ombe. Hata watumishi wa serikali waliiga tabia ya ufugaji kutoka wa Wagogo na Wakaguru, baba yangu na yeye alikuwa miongoni mwao.
Ng’ombe zetu zilikuwa zinahifadhiwa kwa mzee mmoja mwenye jina la Mgulo, huyu Mgulo alikuwa na baba yake aliyefahamika kama Mtangoo. Huku baadhi ya mifugo ikiwamo ndama na vimeme ilibaki katika nyumba tuliyokuwa tunaishi hapo hapo Shule ya Msingi Berege.Wanakijiji wa Berege wengi walikuwa wakulima na wafugaji kama nilivyokujulisha huku kikiwa kjiji chenye shida kubwa ya maji, japokuwa walikuwa na mashine ya kupampu maji kutoka kisima maalumu mara moja moja.
Nakumbuka kila mwishoni mwa mwaka walimu walikuwa wakizunguka vijijini kuandikisha watoto wa darasa la kwanza, wakiwakuta wanacheza wanawasalimu na kuwauliza, Wewe unasoma? Unajibu hapana, walimu hao walikuwa katika makundi ya wawili wawili wanakwambia haya mwanangu chukua mkono wako upitishe kichwani, alafu shika sikio. Ukishika sikio vizuri bila tabu unaandikishwa kujiunga na darasa la kwanza. Kwa watoto tuliokuwa tunakaa jirani na shule tulikuwa tunatamani kuanza shule kwa hiyo unajilazimisha kushika sikio lakini walimu walikataa wakisema wewe bado, wanaondoka zao.
Kwa kuwa mimi wakati huo nilikuwa sijaanza darasa la kwanza nikikosa sifa ya kulishika sikio langu nilipewa majukumu mawili na wazazi wangu; kwanza nakaa na wadogo zangu, mtoto akilia nambembeleza, akilia sana nampeleka kwa mama shuleni, jukumu la pili lilikuwa kwa siku ambazo anakuwepo yaya naambiwa niwachunge vimeme na ndama jirani na nyumba hii ya shule.
Nakumbuka siku moja nilikuwa na jukumu hilo, nikawa nachunga wanyama hao jirani na shule hii, upande uliyokuwa na korongo kuelekea Kijijini Berege Siku hiyo katika kundi la hawa mifugo wadogo alikuwapo beberu mmoja mkubwa sana, sikufahamu kwanini alikuwapo hapo, jukumu langu kama mtoto lilikuwa ni kutimiza kazi niliyoagizwa na wazazi wangu.
Pahala nilipokuwa nachunga ilikuwa nauona vizuri mlango wa nyumbani hii ya mwalimu mkuu, kwa hiyo nilikuwa nachunga huku nikifanya kazi ya ukolokoloni wa nyumba hii. Nikiwa nachunga siku moja mara nikamuona mgeni anabisha hodi nyumbani hapo, mwanakwetu nikaacha mifugo na kumkimbilia mgeni, nikiwa tumbo wazi na fimbo mkononi ya kuchungia.
Nikamfungulia mgeni mlango, nikaenda kuwaita wazazi wangu na wao wakaitikia wito huu.Baba na mama wakatoka hadi nyumbani, nikawaacha wanaongea na mgeni huyu ambaye ilionekana anatoka mbali sana. Mimi nikarudi machungani kwenye mifugo yangu.
Nikaendelea kuwachunga mifugo hao siku hiyo , sasa jua linazama, natakiwa kurudisha wanyama nyumbani nikamkumbuka beberu huyu niliyekuwa naye siku hiyo sikuliona, nafanyaje ? Nikamsaka kwenye korongo sikumuona. Nikaamua kuwaswaga kurudi nao nyumbani huku nikilia, mama beberu amepotea! mama beberu amepotea! Mama beberu amepotea.
Baba yangu akaniuliza unalia nini? Nikamjibu beberu amepotea, mzee akaniadhibu kwanini unapiga kelele mbele ya mgeni? Akaniambia unapokuwa machungani kuwa makini. Mama akatoka na mimi kwenda kumtafuta beberu huyo na baba kubaki na mgeni, huko hatukufanikiwa kumuona beberu wetu. Mama akiniambia mwanangu umempoteza mbuzi wa zawadi ya mgeni, itabidi achinjwe mwingine. Kweli hilo lilifanyika tukila sana nyamaa kwa sababu ya mgeni huyu baada ya kuchinjwa beberu mwingine.
Baba aliwajulisha wanafunzi wake shuleni juu ya kupotea kwa beberu wake, baada ya siku mbili mwanafunzi mmoja alikuja naye beberu huyo ambaye alisema walimkuta katika kundi lao, beberu aliyepotea alipatikana.
Huyu alikuwa bado yupo nyumbani na mgeni kila siku akiamka mapema sana, akiuliza dira ya eneo hilo yaani kaskazini, mashariki, magharibi na kusini ni wapi, kisha anaondoka zake kuelekea vijiji jirani akiwa amevalia mavazi ya kawaida mno. Mgeni huyu alikaa siku kadhaa alafu akaondoka zake na mimi kuendelea na maisha yangu ya kuchunga ndama na vimeme, kulea wadogo zangu huku nikingoja kuanza darasa la kwanza. Kumbuka mwanakwetu lawama ya kupoteza mbuzi wa mgeni nilibaki nayo lakini Mungu bahati beberu huyo alipatikana.
Kwanini nimekikumbuka kisa hiki na huyu mgeni alikuwa ni nani?
Oktoba 24, 2022 saa 11.20 jioni nilipigiwa simu nikapokea, nikaita haloo! nikajibiwa , mimi ni ndugu Pinda, nikashituka nikamsalimu shikamoo! Akanijibu Marahaba! kidogo nikauliza mko wengi, wewe ni yule Naibu Waziri wa Sheria? Akasema hapana mimi ni yule babu, yule mzee kabisa kabisa, mwanakwetu ikanitoka shikamoo nyingine akanijibu marahaba.Mwanakwetu hii ni simu ya mtu mzito , mtu mzito mzito. Nikajua ni Mizengo Pinda, huku sasa masikio yangu yakikumbuka sauti yake, mzee huyu alipokuwa Waziri Mkuu akijibu kiungwana maswali ya wabunge bungeni.
“Mheshimiwa Spika, inawezekana mheshimiwa Mbowe unashahuku kutaka litokee hilo, lakini lakini mambo haya yanategemea ndivyo Mungu kapanga au hapana, najua umeingiza mambo mengi katika jambo hili, kubwa ni hilo ulilomaliza nalo, ningeweza nikajaribu kujibu, lakini sina sababu ya kufanya hivyo,sina sababu ya kufanya hivyo,kwa sababu suala lenyewe ndiyo subject ya mjadala hapa bungeni ambao unaanza leo, nafikiri ni jambo la busara, tusubiri mjadala utakavyokwenda naamini na mimi nitapata nafasi ya kusema mawili matatu, mwisho bunge linaweza kufika mahali ambapo tutasema kwa uhakika hatua sitahiki namna gani inaweza kuchukuliwa.”
Haya yakiwa majibu ya mheshimiwa Mizengo Pinda kwa Mwenyekiti wa kambi ya upinzani Bungeni mheshimiwa Freeman Mbowe miaka karibu 8 iliyopita baada ya sakata la Escrow ambapo siku hiyo mimi nikiwa na mtangazaji mwezangu wa TBC Taifa Mpendwa Mgweno tulikuwa katika matangazo ya moja kwa moja ya redio.Haya niliyafikiria haraka haraka huku nikiongea naye mzee wetu huyu.
Mwanakwetu tuliyazungumza mambo mengi kubwa ni masuala ya imani na kanisa yalikuwa mazungumzo muhimu sana katika masuala ya kiroho. Baada ya kumaliza mazungumzo naye nikamkumbuka mzee wangu huyu tangu akiwa mwalimu wa kwaya na mwanakwaya katika Kanisa la Mtakatifu Antony wa Padua Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Slaam wakati huo na ndipo alipofahamiana na ndugu zangu hadi aliwahi kufikia nyumbani Shule ya Msingi Berege na huyo ndiyo yule mgeni ambae nilimpoteza beberu wake aliyepaswa kumla alipofika Mpwapwa mpaka akachinjwa beberu mwingine.
Mzee wetu Mizengo Pinda binafsi nakushukuru kwa wema wako, kwanza kwa kunikumbuka, pili kwa kuitafuta nambari yangu ya simu na tatu kwa kuipata na nne kwa kunipigia simu hiyo. Simu hiyo imenipa faraja kubwa sana ndiyo maana na mie mwanakwetu si mchoyo wa simulizi nikaamua kusimulia kisa hicho cha ugeni wa mheshimiwa huyu nyumbani kwetu miaka 42 iliyopita nilipompoteza beberu wa mgeni.
makwadeladius@gmail.com
0717649257.
Post a Comment