KUNA WATU WAMEPENDELEWA
Adeladius Makwega-CHAWA
“Kaka kesho ninakwenda Afrika, naomba uje unisindikize uwanja wa ndege wa Cologne-Bonn kwa maana saa 10 alfajiri natakiwa niwe kiwanjani tunakwenda kurekodi mchezo wa redio wa lugha ya Kiswahili mpaka sasa umesharekodiwa kwa lugha zingine, nitakuwepo na wenzangu kadhaa.”
Haya yalikuwa maelezo ya Pendo Paul mtangazaji mmoja wa DW Kiswahili wakati huo akimwambia mwanakwetu wakiwa Jijini Bonn.
Saa saba kamili ya usiku mwanakwetu akaamka hadi stendi kungoja basi, akiwa pale stendi jirani na makazi yake yaliyokuwa Guten Straze alibaini basi la saba usiku lilishapita hapo kilichofuata ni kungoja basi la saa 8 usiku hapo hapo kwa kuwa Pendo anatakiwa uwanjani saa 10 alfajiri.
Mwanakwetu siku hiyo alibaini kuwa mabasi muda wa usiku yanapishana muda mrefu sana na wakati wa mchana yanapishana dakika chache chache.
Saa nane usiku basi lilifika na mwanakwetu kupanda hadi kwa Pendo na hapo alikutana na watu kadhaa wakimngoja mwanakwetu, wengi wao wakifika kumpa mzigo ya ndugu zao waliokuwapo Tanzania. Haraka haraka wakatoka hapo na kupanda treni kuelekea Cologne.
Safari ya basi na hata hii ya treni mwanakwetu hakulipa chochote kwani alikuwa na tiketi ya msimu, kwa mwezi alikuwa anakatwa karibu Euro 55.Usafiri wa basi na treni ulikuwa wa uhakika kuliko usafiri binafsi. Mwanakwetu alibaini kuwa kila alipokuwa akienda kazini iwe katika basi au treni kukutana na wakubwa wa shirika hili la utangazaji ilikuwa ni kawaida mno. Si kwamba walikuwa hawana magari la hasha bali usafiri wa umma ulikuwa wa uhakika zaidi kuliko usafiri wa mtu mmoja mmoja.
Anakumbuka watangazaji kama Mohammed Abdu-Rahman, Ummy Kheri Hamiduou, Mohamed Darman Karama na Othumani Miraji hawa wote walikuwa wanaishi Cologne umbali wa Kilomita 35 na Jiji la Bonn huku hapo Bonn akiishi ndugu Abdu Mtulya pekee kwa watangazaji wakongwe. Mwanakwetu alibaini usafiri wa umma ukiwa madhubuti sana: kwanza unapunguza misongamano ya vyombo vya usafiri, pili inapunguza kiasi cha mapipa ya mafuta yanayotumika, tatu watumishi wanaondesha vyombo vya moto wengi wao wanajikita katika kuhudumia watu wengi na hapo hata ujira wao unakuwa mkubwa, uchafuzi wa hali ya hewa kwa moshi na kelele unapungua na ajali nazo zinapungua pia.
Umbali huu wa Bonn–Cologne hata hawa watangazaji Waisilamu kipindi cha Ramadhani waliweza kufanya kazi na kuzimaliza na kuwahi kupika futari na kufuturu majumbani kwao kwa wakati. Umbali huo ni sawa na kutoka Dar es Salaam hadi Mlandizi/ Dodoma hadi Chalinze Nyama kwa Tanzania na kwa ukweli wa Mungu kipindi cha Ramadhani abiria huyo lazima atafuru njiani na hawezi kuwahi na kuipika futari hiyo hapo Chalinze Nyama au Mlandizihapo lazima anunue cha kufuturu kabla ya safari.
Kumbuka wapo na Pendo Pauli, Iddi Isimael Sessenga wanaelekea uwanja wa ndege wa Cologne-Bonn na mara wakafika hapo.Wakashusha mizigo hadi uwanjani. Uwanja wa ndege wa Cologne-Bonn hapo abiria wanapanda ndege hadi Amsterdam na ndipo wanapanda ndege kubwa kuelekea Afrika.
Wakiwa uwanjani Pendo alikutana na kikosi kikubwa cha DW kinachoelekea Dar es Salaam Tanzania akasalimiana nao na kumtambulisha mwanakwetu kwa Injini mmoja wa sauti Mjerumani aliyeambatana na mkewe dada mmoja Mreno. Pendo akamwambia mwanakwetu,“Kaka nakuunganisha na dada wa Vasco da Gama, kaka ushindwe mwenyewe kuitembelea Ureno, fanya vimbwanga kama vya Batromeo Diaz walipokwenda kwetu na majahazi, usiache kitu mwanakwetu ukikuta dhahabu beba, ukikuta kipusa beba na ukikuta mtumwa beba.”
Wakati maneno haya yakisemwa walikuwepo wazungumzaji wa Kiswahili wawili Mkenya na Mganda lakini hawakufahamu kazi hiyo anayokabidhiwa mwanakwetu ni ipi? Mwanakwetu akatambulishwa kwa dada wa Kireno mke wa injinia na kuombewa kurudi Bonn kwa gari ndogo aina ya Volkwagen Jetta Sport.
Dada wa Kireno akabaki Ulaya na mwanakwetu huku Injinia Mjerumani anakwenda Afrika, kumbuka mwanakwetu alikabidhiwa kazi na dada yake aliye njiani Afrika. Huyu Dada wa Kireno na mumewe walikuwa wakikaa jirani lakini mwanakwetu alikuwa hawafahamu kabla ya siku hiyo, abiria wakakaguliwa nakuingia katika ndege hiyo.
Mwanakwetu aliingia katika gari ndogo huku sasa akimuona kwa karibu dada huyu wa Kireno aliyekuwa ameumbika sana, katika maisha ya mwanakwetu ya Ulaya huyo ndiye mwanamke pekee wa Ulaya aliyejaliwa kumuona kwa macho ameumbika vizuri, kwa Tanzania mwanakwetu alimlinganisha Mrembo huyu na Faraja Kota ambaye alikuwa Miss Tanzania mwaka 2004.
Akiwa amevalia nguo zake vizuri, huku amependeza mno, nayo roho ya sheteni ikitaka kuinuka kwa mwanakwetu ili atupe neno la mapenzi lakini akiogopa kuivunja nadhiri yake ya ndoa aliyofunga na mkewe miaka kadhaa nyuma na akimuacha mkewe Tanzania amejifungua mtoto mdogo anayefahamika kama Joseph Makwega.
Dada huyu wa Kireno alimsimulia mwanakwetu simulizi nyingi kuwa na yeye ni mwanahabari aliyetokeo Ureno na aliwahi kufanya kazi ya DW idhaa yake ya Kireno ambayo inatangazia mataifa ya Afrika kama vile Msumbiji na Angola. Simulizi zote zilimpa tabasamu kubwa mwanakwetu huku akicheka kilometa zote 35 za kutoka Cologne hadi Bonn na kwa hakika wanahabari hawa damu zao zilipatana sana.
Kweli mwanakwetu alifika mbele ya ghorofa alilokuwa akiishi na kuagana na dada huyu mrembo wa Kireno, mwanakwetu alishuka katika gari hilo kwa bashasha kubwa akisema moyoni kuwa kuna watu Mungu amewapendelea.
Nikuume sikio msomaji wangu na haya yasome kwa sauti ya kunong’ona wavivu wa kusoma wasisikie,
“Mwanakwetu alialikwa chakula cha mchana nyumba kwa mrembo huyu na daa mwanakwetu alijinona sana kwa mapishi ya Kireno baada ya mumewe kurudi kutoka Afrika kurekodi mchezo wa redio.”
Naye mwanakwetu alimsimulia dada yake Pendo Paul namna alivyoshindwa kwenda Ureno kulipiza waliyoyafanya Vasco Da Gama na Batromeo Diaz barani Afrika.
0717649257
Post a Comment