Adeladius Makwega-MJI WA SERIKALI
Disemba 23, 2022, siku hii ilianza ya kiwingu wingu na mwanakwetu alipita Mji wa Serikali katika eneo linalojengwa Wizara ya Katiba na Sheria hapo alikutana ndugu zake kadhaa wa Mbagala ambao wanafanya kazi za vibarua vya kujenga katika jengo hilo ambapo kuna siku ndugu zake hawa aliwahi kuwasimulia walipopata changamoto ya malipo yao.
Ndugu zake hawa siku hii walikuwa na furaha sana maana walilipwa pesa yao ili waweze kula sikukuu kwa amani, na kuonesha kwamba wamelipwa walimnunulia mwakawetu chai, maandazi mawili, maharage na soda moja na jumla kuu ikiwa shilingi 1800/. Katika kundi lao kila mtu alimnunulia mwanakwetu kitu kimoja, mwanakwetu alipata ofa ya Noeli na kuwashukuru mno ndugu zake hao kwa wema wao.
Watu wa Mbagala kwa desturi na namna walivyo ni watu wakweli sana, siyo watu vinyongo na watu wenye simulizi nyingi, wanaweza wakagombana asubuhi mchana wanacheka. Aliyepata bahati ya kukaa, kuoa/kuolewa, kutembelea na kufanya kazi eneo hilo atakuwa shahidi.
“Jamaa kama walijua kutulipa nusu, maana kama wangelipa pesa yote tunayoidai saa hizi mwanakwetu usingetukuta hapa tungekuwa tunaitafuta Ubena Zomozi, safari ya kurudi Mbagala Majimatitu, Mbagala Charambe, Mbagala Nzasa, Mbagala Mangaya na Mbagala Kizinga.”
Mwanakwetu akawauliza je pesa hiyo nusu waliyolipwa wamewatumia wake zao majumbani ?
“Ahaaaa kaka ! Mzaramo, Mndengereko, Mmatumbi, Mkwele, Mngindo kaka hapa zingepigwa simu mpaka zingewaka moto. La kwanza lilikuwa hilo tumewaroga na uchawi wa kizungu, pesa uchawi wa kizungu kaka ! Sasa tuna amani. Afadhali ya Chochoro (miongoni wa hao vijana) yeye kaoa mke wa Kimakonde, mkewe hana maneno na yeye mwenyewe Chchoro ulevi wake soda tu.”
Mwanakwetu akawaalika ndugu zake hawa waende kula pilau la Krisimasi kwake Chamwino. Ndugu hawa wakamuuliza mwanakwetu kweli anakula Krisimasi Dodoma ? mwanakwetu akajibu ndiyo. Akiwaalika nyumbani kwake wakale pilau ya bata maana mwanakwetu atachinja bata madume mawili.
“Mwanakwetu unachinja bata ! Chinja mbuzi na sie tuje kujinoma.” Mwanakwertu akawaambia kuwa yeye ameshapanga kuchinjia bata wawili na huo ndiyo uwezo wake maana kuku nyama ya uchoyo na kununua mbuzi gharama yake kubwa mwanakwetu inamzidi kimo.
“Sasa mwanakwetu hakikisha shemeji anapika pilau mapema na sisi saa sita kamili tutakuwa tumefika kwako, tutapiga ubweche alafu tutaelekea kusherehekea maeneo mengine.” Mwanakwetu akajibu naam kwa ndugu zake hao.
Mwanakwetu aliagana na nduguze na kuelekea kwa akina pangu pakavu tia mchuzi kujiandaa na maandalizi ya sikukuu ya kuzaliwa kwa Bwana.
0717649257
Post a Comment