KULINDA GOLI NA KUSHAMBULIA
Adeladius Makwega-CHAWA
Disemba 30, 2022 mwanakwetu ameshuhudia filamu moja fupi ya mwanahabari Deudatus Balile akizungumzia maneno haya,“Wote(sote) tunafahamu kipindi cha miaka sita tulichokipitia, wapo watu ambao hawajaamini amini, uhuru wa vyombo vya habari ni suala la msingi, lakini ukiona Mheshimiwa Rais ni muumini wa uhuru wa vyombo vya habari, Makamu wa Rais pia lile kongamano la habari Iringa alivyoshiriki na akasema kuwa vyombo vya habari ni muhimili wa nne wa taifa, akasema tusimame wanahabari, tusimamie mazingira na mambo yaende vizuri katika nchi hii. Waziri Mkuu amesimamia mikutano kadhaa ya wanahabari inaonesha ana nia ya dhati. Waziri (Habari) kwamba ndiyo usiseme, kwamba amekuwa muumini wa kweli wa uhuru vyombo vya habari na ametuchagiza mara kwa mara tufanye habari za uchunguzi ili kuibua yale yaliyofichika.”
Maneno ya mwanahbari huyo yalimkumbusha mwanakwetu alipokuwa anasoma Same Sekondari kati ya mwaka 1994 na 1995, shule hii ilikuwa na Mkuu wa Shule aliyefahamika kama Mwalimu Musa, mwalimu huyu alikuwa mpole sana huku akiabudu makanisa ya Pentekosti hapo hapo Same.
Shule hii wakati huo ilipokea kundi la wanafunzi wa Tambaza kati ya 50-60 na vijana hawa walikuwa watundu mno na wakimpa kazi kubwa mwalimu wa nidhamu aliyefahamika kama Mwalimu Mzirai, kwa hiyo kusimamishana na kufukuzana shule hilo lilikuwa sawa na kumsukuma mlevi tu.
Siku moja muda mchache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa miongoni mwa hao 60 waliotoka Tambaza anayefahamika kama Samora Machel alifanya kosa na kupewa adhabu ya kudeki bwalo zima la chakula peke yake. Adhabu hiyo ilikuwa kubwa na kuleta malalamiko mengi kwa wanafunzi 60 waliotoka Tambaza lakini walijitahidi kumsaidia ndugu yao. Katika kumsaidia huko ilibainika kuwa ndugu Samora alisaidiwa kudeki bwalo hilo na wenzake. Maamuzi ya mwalimu wa nidhamu ilikuwa ndugu Samora apewe adhabu ya kurudi nyumba kwa miezi kadhaa.
Jambo hili lilileta simanzi mno, kwa wanafunzi waliotoka Tambaza waliokuwa wameokoka kama Mwalimu Musa walitoa ushauri na kumsalisha Sala ya Toba ndugu Samora Machel na kumchukua Samora hadi kwa mke wa Mwalimu Musa nyumbani kwake kumueleza kuwa ndugu Samora Machel ni kweli alikuwa kondoo aliyepotea lakini sasa amepatikana, wakimuomba mama huyo amuombe mumewe amsamehe ama adhabu ya Samora Machel ipunguzwe. Kweli mke wa Mwalimu Musa alipoambiwa hoja hiyo aliipeleka kwa mumewe na Samora akapunguziwa adhabu ya kurudi nyumbani na akaambiwa arudie kudeki tena bwalo la shule hiyo yeye mwenyewe na hilo lilifanyika. Tukio hili ni la miaka 27 iliyopita.
“Wote(sote) tunafahamu kipindi cha miaka sita tulichokipitia” Haya ni maneno ya Balile Hilo halina ubishi lakini je ndugu Balile katika utekelezaji wa majukumu ya umma kazi hufanywa na mtu mmoja? Kwa sasa kulisonta kidole kaburi si sahihi kwa maana kaburi ni sehemu ya walio hai mimi na wewe.Yoyote anayelikana kaburi la nduguye anafanya makosa makubwa mno. Tusifanye hivyo, Kaka balile mwanakwetu anasema wewe nayeye ni makaburi yajayo isiye kutokea kukanana tena na tena hapo kesho. Mwanakwetu anamuheshimu sana Balile kama anavyomuheshimu mwanahabari mkongwe nchini Tanzania Evarist Mwitumba. Kwa hilo la uhuru wa habari mwanakwetu anasema analiweka kiporo hadi Mei 6, 2023 Mungu akimjalia uhai.
Mwanakwetu anaomba kwa hisani yako msomaji wake asimulie kisa hiki cha kweli cha mwaka 2017/2018. Wakati huo Rais Magufuli alifanya ziara ya Mkoa wa Tanga na kutembelea wilaya kadhaa za mkoa huo ukiongozwa na Martine Shgella huku ikiaminika kuwa angeweza kutembelea wilaya ya Lushoto. Kabla ya ugeni huo Waziri Ummy Mwalimu wakati huo akiwa Waziri Afya, Maendeleo ya Jamiii , Jinsia, Wazee na Watoto alifika kata ya Mwangoi na hapo alifanya mkutano wa hadhara akiongozana na viongozi wa serikali wa wilaya hiyo na Mbunge wa Mlalo Rashidi Shangazi. Mheshimiwa Shangazi mbunge mmoja makini na mnyenyekevu alimkaribisha Waziri Ummy aongee na nduguze ambapo wakati huo Waziri Ummy alikuwa pia Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga ndiyo kusema wanawake wa UWT baadhi yao waliompigia kura walikuwepo. Alipomaliza kuongea waziri huyu ilitolewa nafasi ya wananchi kuuliza maswali, swali mojawapo lilikuwa ni juu ya wananchi wa eneo hilo kuiomba serikali imrudishe kazini Mganga Kiongozi wa Kituo cha Afya Mwangoi ambaye aliondolewa kwa kuwa cheti chake cha kidato cha nne kuwa na hitilafu.
Waziri alimuuliza mwanakwetu suala la cheti cha tabibu huyu lilikuwaje? Alijibiwa kuwa tabibu huyo jina lake ni miongoni mwa majina kadhaa yaliyotajwa katika kadhia ya vyeti feki na Waziri wa Utumishi wakati huo Angela Kairuki. Huku mafunzo yake ya utabibu akiyapata ughaibuni katika chuo kinachotambulika vizuri tu na akifanya kazi kwa uhodari mkubwa. Waziri Ummy Mwalimu alisimama na kulijibu swali hilo,“Jamani ni kweli mnamuhitaji tabibu wenu na wangu pia. lakini maamuzi dhidi ya wenye vyeti feki msimamo wa serikali umetangazwa na majina yametajwa, mimi siwezi kubatilisha hilo mpokeeni tabibu mpya aliyeletwa hapa.” Mkutano huo uliisha na Waziri Mwalimu kuondoka zake na kwa bahati mbaya Rais Magufuli hakuweza kufika Lushoto.
Daktari huyu alipoondolewa watu wa Mwangoi kwa kuwa walimpenda na kumuamini mno walimtafuta kijana wao mwenye uwezo wa pesa wakafungua zahanati binafsi na kuanza kutoa huduma, huku watu wengi wa Lushoto wakawa wanakwenda kutibiwa hapo wakiwamo watumishi wa umma na Idara ya Afya aliyokuwa akifanyia kazi. “Mimi nina mdogo wangu alikuwa na ujauzito, niliamua kumleta hapa Lushoto ili ajifungulie na kazi hiyo nilimpa tabibu huyo kwa kuwa anafanya kazi yake kwa uhakika, alifanyiwa upasuaji na mtoto akatoka salama na mama huyo kushonwa vizuri mno.” Haya yalikuwa maneno ya Muuguzi Mfawidhi wa eneo hilo wakati huo na akaongeza haya. “Hata watoto wa kiume wanaokwenda kufanyiwa tohara kwake tabibu huyu ni bingwa wa kuzitengeneza nanga vizuri mno huliko tabibu yoyote yule.”
Wazee wa Lushoto waliokuwepo katika mkutano huo siku ile ya Waziri Ummy anajibu swali wapo waliowahi kuwa mawaziri, wabunge na makatibu wakuu wastaafu wa zamani walimwambia mwanakwetu kuwa kama hoja ni tabibu huyo hakuwa na cheti cha kidato cha nne, mbona wakati wa UJAMAA kulikuwepo na RMA Rural Medical Assistant na wakunga wengi walioweza kutoa huduma za afya kwa jamii yetu kwa kiwango hicho cha elimu? Hilo lingeshauriwa tu kwa mheshimiwa Rais Magufuli.
Nakuuma sikio mwanakwetu wakazi wa eneo hilo mpaka sasa wanatibiwa na tabibu huyo na kila wakikutana na mwanakwetu wanamwambia maneno haya,“Haya sasa kama mnaweza mfuateni huko tulipompeleka, huyu ana uwezo mkubwa, huyu ana siri zetu , hawezi kukaa kijiweni tunamtazama na mkimchokoza huku alipo tutawaloga mchana kweupe.” Mwanakwetu aliambiwa hayo huku akiwaanacheka tu.
Sasa kwa leo hii mwanakwetu ana hoja gani? Unapokuwa katika nafasi ya utekezaji wa mambo ya umma ni jambo zuri sana kama unapokea maelekezi lakini na wewe toa ushauri wako kwa manufaa ya walio wengi, ukiona hilo linashindikana unaweza kutumia mbinu ya wanafunzi wale waliotoka Tambaza waliokuwa Same Sekondari kama kisa cha mwanafunzi Samora Machel, wewe pitia kwa mtu anayeaminiwa sana na ndugu huyo mambo yatakuwa mepesi tu.
Kwa ndugu yangu Deudatus Balile atambue kuwa baadhi ya mambo yanaweza kwenda mrama kwa kuwa baadhi yetu ni mabingwa wa kulinda goli tu tukiwa na nafasi tukiogopa kusema chochote kumbe tunatakiwa kulinda goli na kushambulia.
0717649257
Post a Comment