TAI YA MWAKA MPYA

 

 TAI YA MWAKA MPYA

 Adeladius Makwega-CHAWA

 Ndugu mmoja anayefanya kazi katika ofisi moja ya umma jijini Dodoma alialikwa katika kikao kimoja cha kazi, kikao hicho kilifanyika nje ya ofisi yao na mara baada ya kuhitimishwa kila mshiriki alipewa zawadi ya kifurushi chake. Ndugu huyu kwa kuwa siku hiyo alikwenda kumuwakilisha mkubwa wake alichukua zawadi hiyo hadi ofisini kwa mkubwa wake huyo.

 Hapo ofisini siku iliyofuata na kumuandikia ripoti ya kikao kuhusu yalizungumzwa, zawadi na ripoti mbele ya meza ya mkubwa na huo ndiyo utaratibu wa utumishi wa umma nchini Tanzania, ukipewa zawadi ukiifutika na kukaa kimya hilo ni kosa kubwa.

 Zawadi ikafunguliwa mbele ya watumishi kadhaa wa ofisi hii na kubainika kuwa kulikuwa na tai ambayo thamani yake ukiitazama na ilivyofungwa ilikuwa kubwa. Nani anavaa tai hapo ofisini? Kwa bahati mbaya mvaaji wa tai hakuwepo.

 Ikaamuliwa kuwa tai hiyo ihifadhiwe katika masanduku ya ofisini hiyo ya chuma. Muda ulipita tai ikiwa katika masanduku ya chuma hata harufu yake nzuri ya dukani sasa ikawa inanukia harufu ya makaratasi ya ndani ya makabati hayo ya chuma.

 Disemba 30, 2022 jamaa mwingine mmoja alijisemea moyoni mwake,

 “Ngoja niichukue tai hii niende nayo nyumbani maana ninaweza kuombwa na wadau nikaokoe jahazi la kusimamia ndoa kwa Afisa Tawala Wilaya-Bomani au Kanisani, sasa nikiambiwa vaa tai yoyote, nikiwa sina nitaonekana mie wa zamani sana, kuficha aibu hiyo ngoja niende nayo nyumbani tai hii.”

 Ndugu huyo alifanya hivyo akabeba boksi hilo hadi kwake na alipofika nyumbani aliingia na tai hiyo na kuwafundisha watoto wake wanne namna ya kuifunga tai hiyo kwa staili mbili mojaya Muingereza ambayo ni nyepesi kuifunga yenye sambusa ndogo na ya pili ni ya Kimarekani ambayo ni ngumu huku ikiwa na sambusa kubwa.

Kufundisha somo hilo la ufungaji wa tai kwa watoto wake lilitumia kama saa moja na watoto wake hao wakafuzu namna ya kufunga tai kwa staili zote mbili. Watoto wakachukua boksi la tai hilo na kuanza kuchezea maana lilikuwa na umbo kama pochi yenye rangi mbili nyekundu na nyeupe.

 Watoto wanachezea boksi la tai hiyo nje ya nyumba, gafla mama wa watoto hao aliyekwenda kusuka akarudi nyumbani, hapo anawakuta watoto na boksi kama pochi wanachezea, akauliza hilo boksi la nini na mmelitoa wapi?

Watoto wakajibu kuwa boksi hilo baba ametupatia lilikuwa na tai ya baba na leo ametufundisha namna ya kufunga tai hiyo. Mama huyo akakasirika mno midomo ikaachana kulia na kushoto.

Mume alikuwa katoka kidogo, aliporudi akaulizwa hilo boksi umetoka nalo wapi? Jamaa akajibu kama ilivyokuwa, mama huyu akamwambia ahaaa umeshaanza mambo yako ya kupokea zawadi kutoka kwa wanawake wako ehee!

Jamaa akawa anashangaa anatafuta kujitetea, anafanyaje ? Awapigie simu wenzake wa kazini kuelezea tai hiyo ilipatikana wapi? Hilo akiona halina maana atamwaga mtama kwa kuku wengi.

”Hii natambua kuwa ni zawadi uliyopewa siku ya Boxing day na uliificha ofisini kwako na leo umeamua kurudi nayo nyumbani, sasa mimi ninaondoka zangu kesho asubuhi, uendelee kupokea zawadi zaidi za hao wanawake wengine.”

Mama huyu usiku wa Disemba 30, 2022 aliuona mrefu sana na kulipokucha tu Disemba 31, 2022 alidamkia stendi ya basi kurudi huko alipotoka maana anafanya kazi nje ya Dodoma na alikwenda Dodoma kula sikukuu.

“Sintorudi tena hautoiona sura yangu wala wanao tena.”


Jamaa huyu akabaki lakufanya halijui na sasa anauanza mwaka 2023 akiwa njia panda na tai yake ya mwaka mpya.

 

makwadeladius@gmail.com

 

0717649257

(-Mwanakwetu anakutakia heri ya mwaka mpya 2023)

0/Post a Comment/Comments