WAO KUENDELEA NA SAFARI

 


 

 WAO KUENDELEA NA SAFARI

Adeladius Makwega-CHAWA

 

Mwaka 2002 Chuo cha Ualimu Kasulu kilipokea wanafunzi wa kozi za Stashahada na Astashhada ya Ualimu na wakati huo mwanakwetu alikuwa ndiyo anaingia mwaka wa pili kwa kozi ya Stashahada ya Ualimu. Chuo hiki kilikuwa na Mkuu wa Chuo Alphonce Mbonigaba akiwa mkali sana lakini Mungu alimjalia huruma pale anapofanya maamuzi ya mwisho dhidi ya mwanachuo au mkufunzi.

 

Mwaka huo chuo hiki kilipokea wanachuo wengi wa tabia tofauti zilizovumilika na zingine kidogo ilikuwa ngumu kuzivumilia zilihitaji mno utu, uugwanya na uvumilivu si kwa mkuu wa chuo na wakufunzi tu bali hata kwa wakurufunzi(wanachuo waliosoma ualimu)

 

Katika tabia hizo zisizovumilika kwa wote alipokuwa kijana mmoja ana akili mno darasani, ana afya (pumzi) njema lakini kila ikifika mwisho wa wiki au mapumziko yoyote yale yeye alifunga safari hadi vilabuni na kunywa pombe sana na akirudi anapiga kelele mabweni yote akisema maneno mbalimbali.

 

Jambo hilo lililalamikiwa kwa wanachuo kwanza na likafika katika uongozi wa wanachuo na mkufunzi aliyekuwa anasimamia nidhamua. Kwa hakika vyuo vya ualimu wakati huo malezi ya wakurufunzi yalikuwa kama ya wanafunzi wa sekondari nia ikiwa nzuri kwani hawa wakurufunzi wakihitimu wanakwenda kulea watoto na wanafunzi mashuleni.

 

Mkuu wa Chuo Mbonigaba akamuita mwenyekiti wa wanachuo ambaye ni mwanakwetu akamuuliza sasa huyu ndugu yenu hafai kabisa kuwa mwalimu, mwenendo wake siyo mzuri tunamfukuza chuo. Mkuu wa chuo akamuuliza mwanakwetu hilo unakubaliana nalo? Mwanakwetu akajibu ndiyo lakini huyu mwezetu ana changamoto kidogo. Mkuu wa Chuo akauliza kwani ana shida gani huyu kijana wangu ?

 

Mwanakwetu akaijibu kuwa kijana huyu hana shida yoyote ila akipata upenyo wa kunywa pombe hapo ndipo shida zinaanza, mwanakwetu alimwambia Mbonigaba kuwa alizungumza na viongozi wake wa bweni, viongozi wake wa dhehebu la dini hapo chuoni wamekubaliana suala hilo wanalifanyia kazi na wameliweka katika maombi. Mwanakwetu akamuomba Mkuu wa Chuo ndugu huyu asifukuzwe chuo Mungu bahati anaweza kubadilika na kuwa mtu mwema.

Mbonigaba akasema,“Sisi hatupo hapa kuwatenganeza malaika kutoka mbinguni, tunafahama kila binadamu ana shida zake, wengine ukiwaambia wanabadilika haraka na wengine wanabadilika taratibu na huo ndiyo ubinadamu, mwenyekiti nimekusikia tunalifanyia kazi suala la ndugu huyu-mwambieni abadilike.”

 

Kwa bahati nzuri Mbonigaba hakumfukuza chuo ndugu huyu japokuwa sheria na kanuni za chuo zilikuwa zimevunjwa, ushahidi wa kufanya hivyo ulikuwepo na mashahidi tulikuwepo. Mwaka 2003 mwanakwetu alihitimu na kuondoka zake na huku huyu ndugu akibaki nyuma darasa moja ya mwanakwetu, mwaka 2004 ndugu huyu alihitimu salama salimini na kufaulu masomo yote bila ya kurudia somo hata moja. Mkono wa Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu wakati huo, Alphonce Mbonigaba haukumkwamisha huyu ndugu.

 

Miaka 15 baadaye mwanakwetu akaletewa kesi juu ya vurugu za mwalimu mmoja wa sekondari vijijini, maamuzi yalikuwa gari lilimfuata na askari, akapelekwa hosptali ya wilaya akapimwa na ushahidi ulipatikana kuwa alilewa saa kazi na kushindwa kutekeleza majukumu yake hoja iliyofuta ni vikao vya kinidhamu tu dhidi ya mwalimu huyo hakuna aliyeweza kuvumilia tabia zake si wanafunzi, wazazi, wanakijiji, walimu wenzake na viongozi wa elimu wilaya.

 

Mwanakwetu akasema kabla ya yote mleteni huyu ndugu nimuone, nimfahamu nijue ana shida gani? Alipofika ofisini alipo mwanakwetu mwalimu huyu ambaye mavazi yake yalionesha kuwa ulevi umemvaa akilini na mwilini lakini aliwashangaza watu huku akilia akisema,“Nipelekeni kwa mwanakwetu maana yeye ananijua vizuri kuliko nyinyi na nina hakika atanisaidia tu.” Hilo likawashangaza wengi hata akina mama wawili Fatuma na Beatrice ambao walikua ofisi moja na mwanakwetu. Wakati huo mwanakwetu hapo ni mgeni wa eneo hilo mbona huyu bingwa anajiingiza katika mdomo wa mamba mwenyewe?Watu walisema.

 

Mkuu wa Shule, Mratibu Elimu Kata, Askari, Afisa Elimu Wilaya Sekondari walifika kwa mwanakwetu,“Mkuu tumemleta huyu ndugu yetu ambaye kazi imemshinda.” Fatuma akiwa na faili lake huyu ndugu mkononi na likieleza mwenendo wa tabia ya ndugu huyu.Mwanakwetu akamuuliza haya ndugu yangu shida nini kazi ya watu inakushinda?

 

“Mwanakwetu wewe unanifahamu kuliko wote hawa si Mkuu wa Shule, si Mratibu Elimu Kata, si Askari , si Afisa Elimu. Tumesoma wote na ulikuwa mwenyekiti wangu naomba unisaidia,  mwenyekiti wangu wa chuoni nirudi nyumbani nina amini huko nitabadilika.”

Ndugu huyu anaendelea kulia huku akiyataja majina ya mwanakwetu, mwanakwetu akaomba wote walioingia humo watoke abaki na ndugu huyu na Fatuma na Beatrice akalitazama fili la ndugu huyu kweli alihitimu Ualimu Kasulu 2004, hapo hapo kumbukumbu za mwanakwetu zikakumbuka tukio lile la miaka 15 nyuma lo salale!

 

Je mwanakwetu anatia mkono wake ndugu huyu akufuzwe kazi ? Huku akiwa na mke na watoto kadhaa?

 

“Kama mwaka 2002 niliweka mkono wangu kumuokoa, 2016/2017 ninaweza kumzamisha? KAMA TUDINU TUDANI.” Mwanakwetu alijisemea moyoni akimaanisha kuwa kama unavyowapimia wenzako, ndivyo na wewe utakavyopimiwa-Ukipima haki utalipwa haki, ukipima dhuluma utapimiwa dhuluma, haya mwanakwetu aliyakumbuka kwani aliambiwa na Waislamu wa Mbagala enzi hizo.

 

Mwalimu huyu alipewa uhamisho haraka sana na kuhamia Halimashauri nyingine ya nyumbani kwao. Tangu siku hiyo ndugu huyu alibadilika kabisa na kuwa mwalimu mwema huku akiendelea kuwasiliana na nduguye mwanakwetu.

 

Maisha yanaendelea mwaka huu(2022) mwanakwetu begi lake mgongoni, yupo njia panda Mji wa Serikali anagonja basi kurudi zake Chamwino, gafla akashangaa gari la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na bendera yenge rangi nne imefungwa inapigwa na upepo papa-pa…papa-pa…(Dodoma kuna upepo mkali) breki nyuiiii, mwanakwetu akadhani kuna mtu anashuka, kweli mtu huyo akashuka akamsalimia mwanakwetu.

 

Ndugu huyu mchozi ulimtoka, mbele ya mwanakwetu na boda boda pale njia panda ya Mji wa Serikali, bodaboda wanashangazwa na kilio hicho. Hapo njia panda yupo mama mmoja anauza soda na maji mwanakwetu akanunua maji akamwambia nawa uso, usilie ndiyo maisha yalivyo, wenzako ndani ya gari wasione dalili ya wewe kulia.

 

Afisa Huyu Mkubwa alimuuliza mwanakwetu anakwenda wapi? Akamjibu anakwenda nyumbani kwake Chamwino, kweli walimbeba mwanakwetu hadi kwake na wao kuendelea na safari.

 

makwadeladius@gmail.com

 

0717649257

 

(NB-Mwanakwetu anakutakia heri ya Noeli na Mwaka Mpya 2023.)

0/Post a Comment/Comments