DADA MKUU MWENYEKITI KIKAONI

 

(Jemedari Said . Mwalimu Nyerere & Habib Halahala)

Adeladius Makwega-KILIMATINDE

Kuna wakati Shule ya Sekondari ya Ndanda ilijengewa bweni na Baba Abate wa Wabenediktine wa Ndanda ambalo lilijengwa kuokoa jahazi baada ya bweni la wasichana la shule hii ambalo lilikuwa jirani na makazi ya watawa wa kike kupata uharibifu wa mafuriko ya mvua kubwa za mwaka 1990 eneo la Ndanda , Jipite  na sehemu kadhaa za wilaya Masasi wakati huo.

Mvua hizo zilileta madhara makubwa na hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi kutembelea na kukagua eneo hilo na kuwafariji Watanzania waliokumbwa na madhara ya mvua hizo.

Kama ilivyo sasa Rais hufunga safari na msululu wa watu ikiwamo wasaidizi wake.

Rais Mwinyi alipofika Jipite ambapo madhara makubwa ya mafuriko hayo yalionesha namna maji yaliyosomba makazi, miti na kubomoa madaraja kadhaa huku watu kadhaa wakifarki dunia. Rais Mwinyi akiwa katika hedikopta walishuka kwa nia mbili; kwanza kuona madhara hayo kwa ndimi zake na pili kutoa pole kwa jamii iliyokumbwa na mafuriko hayo.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema;

“Marehemu Rais Ali Hassani Mwinyi alitumia usafiri wa helikopta, kuelekea Kusini mwa Tanzania,ambapo usafiri wa gari ilikuwa ngumu. katika msafara huo alikuwepo pia ndugu Habibu Halahala-Mwandishi wa Habari wa Rais sasa ndiyo hii Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Walipofika eneo la tukio, Helikopta ilipotua tu miongoni mwa watu wa mwanzo kushuka ni Habib Halahala, yeye aliwahi kushuka ili kupiga picha nzuri ya Rais akishuka kwenye helikopta hiyo na anapofanya ukaguzi na kutoa pole kwa wahanga wa mafuriko hayo.

Kwa bahati mbaya wakati anashuka, panga boi za helikopta bado zilikuwa zinazunguka kwa kasi, bila kujua Habib Halala anataka kuwahi kutekeleza majukumu yake, kwa bahati mbaya Habib Halahala ambaye alikuwa Mwandishi wa Habari Mahiri na Nguli Mpogolo wa Ulanga hakuinamisha kichwa chake, hapo hapo lile panga boi la helikopta likamkata shingo, akafariki hapo hapo.”

Msomaji wangu Mwandishi wa Habari Mahiri Habib Halahala akafariki akiwa kazini, Rais Mwinyi alitekelea Majukumu yake haraka haraka na kurudi Dar es Salaam. Mwili ulibebwa hadi Hospitali ya Ndanda na baadaye kuzikwa kwao.

Kwa ambao hawamfahamu marehemu Habib Halahala wajue kuwa alichaguliwa na Rais Julius Nyerere kuzifanya kazi za Habari-Ikulu na kwa bahati nzuri Ali Hassan Mwinyi aliendelea kufanya naye kazi.

Nakuomba msomaji wagu fahamu kuwa tukio hili lilitokea mwaka 1990 Mwalimu Nyerere aling’atuka Urais mwaka 1985.Tambua kuwa wakati Marehemu Halahala anafariki dunia tayari alishafanya kazi na Rais Mwinyi kwa karibu miaka mitano na alishafanya kazi na Ikulu ya Magogoni miaka sita kuelekea saba.

Simulizi ya tukio hilo Mwanakwetu aliikuta Shule ya Sekondari Ndanda miaka sita baada ya kutokea.

 (Ndanda Sekondari & Ndanda Abbey)

Madhara ya mvua hizo yalilikumba pia sehemu makazi ya watawa hawa Wabediktine likiwamo eneo la bweni la wasichana la Shule ya Ndanda. Kumbuka msomaji bweni wasichana la Ndanda lilikuwa jirani na watawa wa kike kwa kuwa shule hii awali ilikuwa mali ya Kanisa Katoliki kabla ya kuchukuliwa na AZIMIO LA ARUSHA.

Bweni limepata uharibifu baadaye watawa hawa waliokoa jahazi la ujenzi wake. Ujenzi wa bweni hilo ulipokamilika kabla ya ufunguzi wanafunzi wa kike wa shule hii ya walihamishwa na kukaa katika mabweni hayo mapya ambayo yalijengwa pembezoni mwa shule hii kongwe.

Bweni hilo jipya liliongeza idadi ya mabweni kutoka mabweni ya awali; Mawezi, Kibo, Mtandi na Ilulu ambayo ni mabweni tangu enzi za akina Benjamin Mkapa walipokuwa wanafunzi.

Wanafunzi wa Ndanda walilibatiza jina bweni Hilo Jipya SHELATONI

Wakati ujenzi wa bweni la wasichana unakamilika Mwanakwetu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha sita. Maamuzi ya wakubwa wakati huo walisema kuwa mahafali ya mwaka 1998 yatumike kulifungua bweni hilo jipya.

Nakuomba msomaji wangu ukumbuke hili,

“Kabla ya mahafali hayo shule hii ilikumbwa na uhaba mkubwa wa walimu, hivyo wanafunzi wengi waliochaguliwa kidato cha tano tangu mwaka 1995, 1996 na hata 1997 walihama, kwa hiyo walibaki wanafunzi wachache mno akiwamo Mwanakwetu.

Katika kuhama huko waliondoka hata viongozi wa serikali ya wanafunzi akiwamo Kaka Mkuu. Nafasi kadhaa za viongozi wa wanafunzi zilijazwa ikiwamo Kiongozi wa Chakula na nafasi hiyo alichaguliwa Jemedari Said(Bin Kazumari), Jemedari alikuwa mwanamichezo tangu wakati huo akishiriki mashindano ya UMISETA-KITAIFA kwa bahati mbaya Kiranja wa Michezo alikuwepo-hakuhama, hivyo Jemedari Said aliyehamia Ndanda kutoka Lindi Sekondari kwa kuwa alikuwa na ushawishi mkubwa shuleni lazima awe kongozi, hivyo akachaguliwa akawa kiongozi wa chakula.

Mwanakwetu alikuwa kiongozi wa Afya na Mazingira. Kumbuka nafasi zote zilijazwa isipokuwa Kaka Mkuu hilo lilifanywa kwa nia njema kuwapa nafasi wanawake ya kuongoza bila bughuza.”

Kabla ya kufanyika mahafali, uongozi wa wanafunzi huu wa akina Bin Kazumari  uliokuwa unamaliza muda wake na Dada Mkuu wao ulifanya mchakato wa kuwapata viongozi wanaoachiwa serikali ya wanafunzi na hoja kubwa ilikuwa namna kumpata Kaka na Dada Mkuu, hapo unafanyika mchujo ndani ya kikao hicho Mwanakwetu alikuwepo na mjumbe halali wa kikaoni.

“Chini ya kikao kinachoongozwa na Dada Mkuu mjadala unafanyika, kumbuka Kaka Mkuu alihama na nafasi ya Kaka Mkuu haikujazwa ili kuwapa nafasi wanawake waongoze bila bughuza.”

Majina kadhaa yalipendekezwa na kujadiliwa huku maoni kadhaa yakitolewa na kikao hicho kikakubaliana bila shaka na kwa kauli moja majina ya wagombea wawili kwa nafasi ya Kaka Mkuu Mpya.


 Michezo ya UMITASHUTA na UMISETA

Mjadala ulihamia kwa mapendekezo ya Dada Mkuu, majina yaliyopendekezwa yalijadiliwa kwa kina, huku mwenyekiti wa kikao hicho-Dada Mkuu anayemaliza muda wake akipata changamoto kubwa kutoka kwa wajumbe juu ya jina moja pendekezwa.

Wajumbe kadhaa waliokuwepo katika kikao hicho, wengi wakiwa na mawazo tafauti juu ya jina moja pendekezwa la Dada Mkuu kikaoni ilionesha kuwa Dada Mkuu anayemaliza muda wake alitamani huyo arithi nafasi yake.

“Kwa wajumbe kulipinga jina la Dada Mkuu pendekezwa ilitoa tashira mbaya kwa Dada Mkuu anayemaliza muda wake maana lilikuwa chaguo lake, hapa sasa kama vile wajumbe wanampinga Dada Mkuu na Mwenyekiti wa kikao hicho.”

Madai ya wajumbe yalikuwa mengi dhidi ya jina hilo, wakisema jina hilo lina tuhuma ya kujihusisha na mahusiana ya kimapenzi na baadhi ya walimu. Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa mkali mno akitaka ushahidi wa hoja hiyo kutoka kwa mjumbe aliyeibua jambo hilo.

Mjumbe alijibu;

“Kama tuhuma hizo ni za uwongo, kwanini tuhuma hizo akubebeshwa mtu mwingine? Mbona majina yalilopendekezwa kwa Kaka Mkuu hakuna tuhuma hata moja iliyotajwa?”

Mwenyekiti(Dada Mkuu) alikuwa mkali mno, akisema mbona tuhuma hizo nzito mnawabebesha wasichana ambao ni dada na mama zenu?

Mjadala ulipamba moto na mjumbe mmoja kusimama na kueleza ushahidi wake wa mazingira kadhaa aliyowahi kuyaona ya jina pendekezwa na mwalimu aliyetuhumiwa. Ushahidi huo ulimnyima raha Mwenyekiti wa kikao hicho lakini hakuwa na namna maana kikao hicho lazima kije na maamuzi yake na yapelekwe katika kamati ya walimu,  hapo Katibu Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi aliyekuwa Kapteni  wa JWTZ ananukuu kila mchango wa wajumbe na kuwekwa katika muhtasari.

Mwenyekiti alisimama na kusema kwa hasira;

“Kuna watu wanakuwa wakali mno na kulikataa jina pendekezwa kwa hoja zisizo na ukweli, hilo siyo jambo zuri, kwanza sisi tunahitimu kidato cha sita mwaka 1998.Kwani wanaobaki hapa ni ndugu zetu? Acheni mambo yenu.”

Mjumbe mmojawapo aliinuka na kusema,

“Hata wewe Mwenyekiti mwenendo wa tabia zako tunazitilia shaka mno, hata wewe una shida hizo hizo zinazolalamikiwa kwa jina hilo pendekezwa. Hatusemi mengi kwa kuwa tunaondoka, tunatamani tuondoke salama na wanaobaki wabaki salama, hiyo ndiyo nia ya maoni ya wajumbe kikaoni.

Hatumchagui Dada Mkuu awe wakala wa kuwatoa usiku dada zetu kutoka SHELATONI(bwenini) na kuwapeleka mitaani, tunamchagua Dada Mkuu wa kuwalinda dada zetu hao, wawe wa damu na hata hawa tunasoma nao pamoja.”

Kikao hicho kilijadili kwa muda na kwa bahati nzuri mwisho wa siku iliamuliwa kwa nafasi ya Dada Mkuu agombee binti mmoja wa Kidato cha Tatu wakati huo aliyefahamika kama Bahati Gwambasa . Kweli kikao cha walimu wa Shule ya Sekondari Ndanda kilikubaliana na hoja zote za maamuzi ya Serikali ya Wanafunzi na Bahati Gwambasa alishinda na kuwa Dada Mkuu kumalizia muda hadi walipofika kidato cha tano Julai 1998. Hivi sasa Bahati Gwambasa ni askari wa JWTZ

Siku ya mahafali ilifika na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara wakati huo Kanali Nsa Kaisi alifika na kufungua bweni hilo na kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya shule ya sekondari Ndanda ambayo ni shule ya umma nchini Tanzania.

Mahafali yalipokwisha kidato cha sita walifanya mitihani yao na kuondoka zao, wengine walipanda mabasi na wale Dar es Salaam akiwamo Mwanakwetu walienda hadi Mtwara na kupanda boti ya Canadian Spirity naye Dada Mkuu aliyemaliza muda wake na mwenyekiti wa kikao alipanda ndege ya ATC kurudi zake Dar es Salaam.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Msomaji wangu nakuomba ukumbuke haya,

Mosi ;

“Kwa ambao hawamfahamu marehemu Habib Halahala wajue kuwa alichaguliwa na Rais Julius Nyerere kuzifanya kazi za Habari-Ikulu na kwa bahati nzuri Ali Hassan Mwinyi aliendelea kufanya naye kazi.

Nakuomba msomaji wangu fahamu kuwa tukio hili lilitokea mwaka 1990 Mwalimu Nyerere aling’atuka Urais mwaka 1985.Tambua kuwa wakati Marehemu Halahala anafariki dunia tayari alishafanya kazi na Rais Mwinyi kwa karibu miaka mitano na alishafanya kazi na Ikulu ya Magogoni miaka sita kuelekea saba.”

Mtu anapoteuliwa kushika nafasi kubwa, haji kufanya kazi tu na anayemteua bali anakuja kufaya kazi na jamii inayomzunguka na hata wanaokuja kuchaguliwa baadaye, Kama umri wake unaruhusu na Mungu akimjalia uhai, hili Mwanakwetu anaomba litiliwe maanani katika utumishi wa umma wa Tanzania

Pili,

“Katika kuhama huko waliondoka hata viongozi wa serikali ya wanafunzi akiwamo Kaka Mkuu. Nafasi kadhaa za viongozi wa wanafunzi zilijazwa ikiwamo Kiongozi wa Chakula na nafasi hiyo alichaguliwa Jemedari Said(Bin Kazumari), Jemedari alikuwa mwanamichezo tangu wakati huo akishiriki mashindano ya UMISETA-KITAIFA kwa bahati mbaya Kiranja wa Michezo alikuwepo-hakuhama, hivyo Jemedari Said aliyehamia Ndanda kutoka Lindi Sekondari kwa kuwa alikuwa na ushawishi mkubwa shuleni lazima awe kongozi, hivyo akachaguliwa akawa kiongozi wa chakula.”

Jemedari Said sasa ni mwanahabari , akichambua michezo, huyu jamaa ana uzoefu mkubwa katika michezo. Ameshiriki mashindano ya kitaifa ya Shule za Msingi na hata Kitaifa ya shule za sekondari , amecheza soka la Tanzania Ligi Kuu na amecheza Timu ya Taifa ya Vijana na amecheza mechi za kimataifa kadhaa, amekuwa kocha wa timu kadhaa na kiongozi wa soka Tanzania.

Katika makala haya Mwanakwetu nimeleza namna Jemedari Said alivyokuwa kiongozi wa wanafunzi pale Shule ya Sekondari Ndanda akishiriki kikao kigumu kama hicho akitoa michago muhimu sana.

(Marehemu Kanali Nsa Kaisi)
 

Mama Tanzania mtumieni huyu ndugu. Hivi sasa ndugu huyu anazeeka, Mwanakwetu ninawaambieni mapema mtumieni atawasadia, anaifahamu michezo kwa kuicheza na anaufahamu uongozi kwa kuongoza.

Yapo mengi katika makala haya msomaji wangu lakini mengine yatafakari mwenyewe .

Mwanakwetu Upo?

Dada Mkuu !

Mwenyekiti Kikaoni.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 (Mawaziri wa zamani wa Michezo Tanzania)

 

0/Post a Comment/Comments