KUTOKUWAPENDA WATANZANIA NI KUWAHUZUNISHA MARAFIKI

KUTOKUWAPENDA WATANZANIA NI KUWAHUZUNISHA MARAFIKI

 Lucas Masunzu-MAKOLE

Mwaka 2013 nilikuwa ninaishi Kisii nchini Kenya ambapo shughuli zangu za kila siku nilikuwa nafanyia katika ghorofa ya pili pale Nyatero. Mara nyingi kifungua kinywa nilikuwa ninapata kwenye hoteli moja iliyokuwa karibu na Nyatero. Kwa kuwa kuku mgeni hakosi kamba mguuni, wenyeji wa maeneo hayo waliweza kunitambua kwa haraka sana kwa kuwa sikuwa raia wa Kenya hata nilipokwenda hotelini mara kwa mara wahudumu wa hiyo hoteli walitaka kufahamu kaunti(wilaya) ninayotoka.

Nikiwa katika shughuli zangu za kila siku nilibahatika kukutana na ndugu Dadius Okwonyo ambaye ni Mkenya, alikuwa akifanya kazi shule ya moja ya wasichana huko Sironga-Nyamira huko huko nchini Kenya. Kadri siku zilivyozidi kuongezeka niligundua kuwa Dadius alikuwa ni mtu mwema sana hata nilipohitaji kubadilisha shilingi ya Tanzania kuwa shilingi ya Kenya mara nyingi alinipatia msaada katika benki moja jirani. Dadius alipenda kunitambulisha kwa nduguze na marafiki zake, kwa tabia yake njema ya kunitambulisha kwa ndugu ilifikia hatua tukafahamiana na baadhi ya nduguze, kuna kipindi alipata msiba ilinibidi niambatane naye kwenda kushiriki maziko.

Kuna siku Dadius aliniomba nipange ratiba niende nikamsalimie shemeji yangu (mkewe) aliyekuwa anaishi Nyamira, nilipanga ratiba yangu nikatimiza jambo hilo. Familia ilifurahi sana wakaandaa chakula kwa ajili yangu, nililala hapo kesho yake ndipo niliweza kuondoka. Kadri siku ziliyokuwa zinaongezeka, urafiki kati yangu na Dadius ulizidi kuwa imara na kama kamba basi iliendelea kukaza. Siku nyingine tena rafiki yangu huyo alinipeleka kwenda kumsalimia bibi yake aliyekuwa anaishi mji wa Eldoret ulio umbali wa takribani kilometa 140 kutoka mji wa Kisii, kwa Tanzania umbali huo ni  ni sawa na Dodoma–Manyoni Singida au sawa na kutoka Morogoro Mjini hadi Mlandizi Pwani. Mapokezi yalikuwa mazuri sana, kila mtu aliyeambiwa ninatoka Tanzania alipata shauku ya kufahamu mambo mbalimbali yaliyopo Tanzania, huku wanafunzi wengi wakitaka kufahamu mambo mbalimbali kuhusu chuo kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na kati Chuo Kikuu cha Dodoma kinachopatikana Tanzania.

Ilikuwa jioni wakati tumewasili nyumbani kwa bibi yake rafiki yangu, “Good evening uncle” kijana mmoja alinisalimia kwa Kiingereza na mimi nikaitikia, huku nikiwa naelekea sebuleni kwenda kuketi kwa haraka nilibaini familia nzima walikuwa wakiwasiliana kwa kimombo. Nilipoingia sebuleni alikuwapo bibi mmoja ameketi kwenye sofa, nywele zake zote zilikuwa nyeupe kuonesha kuwa amekula chumvi nyingi. Kabla hata sijaambiwa niliwaza kichwani mwangu kuwa bibi tuliyekuja kumsalimia ndiye huyo. Nilimsogelea na kupeleka mkono wangu kumsalimia, tuliposhikana mikono aliniambia nimsalimie kwa Kiswahili maana anafahamu Kiswahili. “Shikamoo bibi” nilisalimia hivyo, familia yote iliangua kicheko kikubwa huku nikiulizwa “Huyu ni bibi yako?”  nikiwa bado nasubiri jibu la salamu yangu kicheko kilitulia ndipo bibi huyo akaitikia salamu yangu. Nilimuuliza rafiki yangu kwa sauti ya chini “Kwa nini nimemsalimia mkacheka?” alinijibu kuwa huku kwetu Kenya neno “bibi” lina maana ya mpenzi wako ndiyo maana tumecheka kuona wewe ni mpenzi wa bibi yetu!

Nikawa nipo sebuleni hapo ninapiga soga na huyo bibi, ni kawaida kwa familia nyingi za Kiafrika kuweka picha mbalimbali sebuleni hasa za wanafamilia, hata katika sebule hiyo kulikuwa na picha mbalimbali za wanafamilia lakini kulikuwa na picha moja ilinivutia zaidi. Picha hiyo ilikuwa ni ya Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta wakiwa pamoja na Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Tukiwa tunaendelea kupiga soga bibi huyo aliniambia jambo hili “Ninawapenda Watanzania kwa sababu rais wenu wa kwanza na rais wetu wa kwanza walikuwa marafiki sana, marafiki hao walipendana sana, kwetu sisi KUTOKUWAPENDA WATANZANIA NI KUWAHUZUNISHA MARAFIKI, watazame hapo kwenye picha wanacheka na majina yao wote yanaanza na herufi J-JOMO & JULIUS kama pacha sisi ni ndugu.”. Niliitazama picha hiyo ni kweli marais hao meno yao yalikuwa nje maupe pee kama sufi.

Bibi huyu alifahamu mengi ambayo sikuwahi kuyasoma hata kwenye somo la Historia. “Marafiki hawa ambao wote walikuwa watoto wa kichifu waliwahi kuzungumza kuhusu uwezekano wa kuunda serikali ya Muungano wa Tanzania na Kenya ambapo Nyerere alikubali kumwachia Kenyatta nafasi ya urais” aliniambia hivyo bibi huyu. Aliendelea kuniambia kuwa “Matamanio makubwa ya marafiki hawa yalikuwa ni kuona kuna amani, utulivu na maendeleo ya bara zima la Afrika” nikiwa katikati ya mazungumzo hayo aliniambia kuwa jina Kenyatta linatokana na mkanda aliopenda kuuvaa ambao ulitengenezwa kwa shanga, Wakikuyu wanauita kenyaata. Baadaye niliitwa kwenda kupata chakula lakini nilikuwa bado ninatamani kuendelea kupata simulizi hizo, niliinuka kuelekea sehemu ya mlo.

Kwa kuwa ilikuwa Disemba zilikuwa zimebakia siku chache tusherekee sikukuu ya mwaka mpya, bibi huyo alinipa mwaliko wa kurudi kushiriki sikukuu ya mwaka mpya nyumbani kwake lakini kutokana na uelewano wa marafiki hao (Nyerere na Kenyatta) aliniambia ataniandalia zawadi ya mwaka mpya. “Tuombe uzima, nitakuja” niliahidi hivyo.

Siku ya mwaka mpya ilipofika nilitimiza ahadi yangu, bibi huyo alifurahi sana kuniona tena, nimerudi nyumbani kwake, tulisherekea vizuri sikukuu hiyo. Baada ya mlo bibi aliniambia nijiandae kupokea zawadi yangu, nilikabidhiwa binti mmoja ambaye ni mjukuu wake, nifunge naye pingu za maisha halafu nirudi naye nyumbani Tanzania. Binti huyo alikuwa mpole, maji ya kunde mwenye sura isiyokuwa na haya, alikuwa akifanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenyatta nchini Kenya. Nikiwa bado sijajua la kufanya nilikumbuka kuwa nilikuwa ni mwanafunzi hivyo uanafunzi ukawa ni pingamizi iliyofanya nishindwe kupokea zawadi hiyo. Bibi alinisisitiza kuwa pamoja na pingamizi hiyo kama kuna jambo tunatakiwa kulifanya kwa mwaka huo mpya ni mahusiano bora na watu. Mahusiano yanaishi hata maisha yakikoma. Tuliagana vizuri nikarudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu za kila siku.

theheroluke23@gmail.com

0733346877

2023

 

0/Post a Comment/Comments