TUA HILO BEGI

 TUA HILO BEGI

Adeladius Makwega-Buigiri

Siku ya moja mwanakwetu alisafiri kutokea Lushoto kuja Dodoma na kwa bahati nzuri alipata usafiri kwani tiketi alikata mapema siku tatu kabla ya safari yake hiyo kuepukana na changamoto ya usafiri katika siku za mwisho wa mwaka. Kulingana na tiketi yake alipaswa kukaa kiti namba 13 lakini kwa kuwa basi hilo lilipoanza safari Lushoto kuna abiria waliopanda ambao walikuwa wakishuka Korogwe kwa hiyo pahala alipotakiwa kukaa alikaa abiria mmoja ambaye aliona siyo busara kumnyanyua, atakaposhuka angekaa nafasi hiyo isitoshe viti vingi vilikuwa wazi.

Walipoanza safari kutokea Lushoto Mjini alidhani basi hilo lipo tupu lakini walipofika Korogwe abiria waliingia wengi na kusababisha kweli basi hilo kujaa, hapo hapo na nayeye kuhamia katika kiti chake alichopangiwa na mkataji tiketi.Safari ilianza na kuondoka Korogwe vizuri kwa mwendo wa kiistarabu wa dereva wao wa siku hii.

Muundo wa viti vya basi hili ulikuwa ni viti viwili viwili kila upande na katikati ni njia ya kupita, kwenye kiti cha mwanakwetu alikaa yeye na mama mmoja na upande wa kushoto kwake alikuwepo mama mmoja mtu mzima na kijana mmoja.

Kumbuka mwanakwetu ameanzia safari Lushoto bali huyu mama amepanda Korogwe na alipopanda tu alibaini kuwa ni mama makini kwanza alikuwa amevalia barakoa vizuri sana na huku akiwa na kipukutishi na kila mara alikuwa akijimiminia mikononi angalau awe salama. Alipokuwa akijimiminia kipukutishi hicho kilisababisha na mwanakwetu kupiga chafya sana sana ambapo kabla ya hapo hakuwahi kupiga chafya yoyote kwa miaka mingi.

Katika viti hivyo vine hakuna mtu mwingine aliyekuwa kavalia barakoa zaidi ya yeye. Wakaendelea na safari alipomuangalia vizuri alibaini kwa umri wake alikuwa ni bado mdogo bali alikuwa amevalia baibui vizuri sana na kutokana na joto la safari alikuwa sasa anajifungua na mwanakwetu alikuwa anamkodolea kwa wizi angalau aweza kumuona vizuri. Basi lilipokuwa linazidi kwenda alibaini kuwa mama huyu alikuwa ni mweupe na alisuka twende kilioni.

Kwa kuwa safari za mwisho wa mwaka usafiri unakuwa mgumu, basi hili lilipata abiria zaidi kwa hiyo baadhi ya abiria walikaa katikati huku wakipatiwa ndoo/vigoda vya kuketi. Kwa sasa katika mstari ule wa kushoto na kulia abiria wawili wawili abiria mmoja wa kati kwa hiyo kulikuwa na abiria watano katika kigoda au ndoo hapa kwa mwanakwetu abairi wa katikat alikalia ndoo ya lita kumi..

Huyu mama jirani yake yeye tangu alipokuwa amepanda Korogwe alikuwa na begi mgongoni alipokaa akalipakata juu ya miguu yake huku akipata nalo tabu kweli kweli, tangu anaingia basini Korogwe alikuwa na nafasi ya kuweka katika sehemu ya kuweka mizigo lakini hakufanya hivyo, aliendelea kulibeba safari yote.

Basi liliendelea na sasa lilifika Msata ambapo kuna mizani, lilisimama na abiria kushuka na kwenda kujisaidia na kurudi kuendelea na safari yetu.

Dereva aliendelea kuendesha vizuri na sasa wakawa wanakaribia kufika Morogoro, huku mwanakwetu na abiria mwezangu ambaye kwa hakika alikuwa anaheshimu masuala ya afya haswa haswa lakini ana mzigo ameubeba na mzigo huo unaonekana ni mzito na unamchosha lakini kaendelea kuupakata mithili ya mtoto mchanga, atawezaje kuambiwa auweke chini?


 

Pengine ameweka fedha zake zikiibiwa itakuwaje? Pengine kaambiwa na mganga wa kienyeji hilo begi unaposafiri haupaswi kulishusha, likae mapajani mwako tu mwanzo mwisho. Maana kila mtu na imani yake. Mwanakwetu aliendelea kuwa kimya na kumtazama ndugu huyu anavyoteseka.

Walfika Msamvu na abiria kadhaa walishuka nadhani hao walikuwa wakielekea mikoa ya Mbeya na Ruvuma, wakati mwanakwetu na mama mpakata mabegi wanaelekea Dodoma. Mara baada ya abiria hao kushuka, basi lilipitia hoteli moja walikula chakula na kuendelea na safari. Mpaka muda huo mama mpakata mabegi na wale abiria wengine wa viti vya mkono wa kushoto na kulia nadhani wote walikuwa abiria wa Dodoma kwa hiyo hakuna aliyeshuka Msamvu.

Safari iliendelea hadi Gairo, huku mama mpakata begi akiwa amechoka kweli kweli, sasa mama wa upande wa kushoto katika kiti cha kushoto alimueleza,

“Sasa wewe huoni unateseka na begi ukiwa umelipakata tangu Korogwe hadi huku kana kwamba umebeba mtoto? Kweli unadhani utafika salama Dodoma? Na hata ukifika salama unaweza kupata madhara ya kiafya.Jihurumie kama ulivyovaa barakoa na unavyojipaka kipukutishi kujikinga na Korona.”

Kweli eeh? Aliuliza huyu mama mpakata mabegi mapajani. Mama wa kando alimjibu kweli.

“Unajua humu nimeweka kompyuta, nilidhani inaweza kuharibika.”

Mama huyu alimwambia. “Sasa hiyo kompyuta na hilo paja lako kipi cha thamani kwako? Hiyo kompyuta ikifa utanunua nyingine lakini huo mfupa wa paja ukivunjika?”

Basi mama huyu mpakata begi alisimama na kulichukua begi lake na kuliweka chini ya kiti nayeye kukaa kwa amani tangu Gairo kuelekea Dodoma.

Alipoutua mzigo huo mama huyu alihema kwa nguvu na mara jasho linamtoka baada ya mwili kuondoa mzigo mzito uliolala mapajani mwake kwa saa karibu saba.

Hoja ya leo ni moja tu, katika maisha wapo watu ambao wanakuwa na mizigo wameibeba wakidhani kuwa ina thamani kubwa kumbe haina lolote bali imekuwa ikiwaumiza na kuwatesa pengine bila ya wao kufahamu hilo. Wapo watu wanaoona kuwa hapa mwenzetu ameelemewa na huo mzigo lakini hawakwambii kwa hofu nyingi tu, ah pengine mganga wake kamwambia alishikilie/pengine kuna fedha na vitu vya thamani ndani yake, ngoja mimi nikae kimya tu. Kumbe mwezenu anaumia. Kuna madhara ya moja kwa moja wakati huo huo lakini yapo madhara ya baada ya kumaliza safari.

Kwa bahati nzuri mama huyu alipoambiwa kuutua mzigo alikuwa muelewa kwa haraka na mzigo aliutua muda huo huo. Je wewe mwanakwetu umepakata nini?

“Tua hilo begi, liweka chini ya kiti ili uweze kusafiri kwa salama na amani.”

Ndugu huyu saa kadhaa amepakata begi, angalia usivunje huo mfupa wa paja. Ukimaliza safari unafika nyumbani unachechemea unakutana na talaka juu ya meza. Kwa mwanakwetu anaiishia hapo, anaendelea kuzaliwa pamoja na Bwana. Anakutakia Mwaka Mpya mwema.

 makwadeladius@gmail.com

0717649257.

 

0/Post a Comment/Comments