IBADAZA KARABAI ZA KUAZIMA

 

 

 

  IBADA ZA KARABAI ZA KUAZIMA

 Adeladius Makwega-Buigiri

Jumapili ya Januari 23, 2022, mwanakwetu aliamka mapema kidogo ili kuwahi misa ya kwanza ya siku hii. Kwa siku hii ukweli na kwa Mungu hadi anafika kanisani alikuwa amechelewa dakika 10.Japokuwa alichelewa dakika hizo kilichofanya achelewe ni kunyesha kwa mvua kubwa usiku mzima kwa hiyo hadi alfajiri hiyo mvua kubwa ilikuwa ikinyesha na matope yalikuwa mengi, mwendo wake ulikuwa wa uangalifu ili kuepuka kuanguka na kuvunja miguu.

 Alipokaribia ngazi za kanisani alisikia wanakwaya wakiimba wimbo lakini kanisani kulikuwa giza bila ya kujua kulikoni. Akilini mwake ilikuja hoja kuwa labda wanakwaya wanafanya mazoezi na Padri kachelewa kidogo. Wakati tukio kama hilo huwa ni jambo la nadra sana kulishuhudia kanisani, mtu unaweza kuzaliwa hadi kufariki na usishuhudie Padri kuchelewa misa.

Mwanakwetui ameshuhudia mara mbili, mara ya kwanza ilikuwa Kigango cha Mkuranga miaka ya 1980s ambapo Padri alikuwa akitoka Parokia ya Mbagala, Parokia ya Kurasini au hata Parokia ya Mtakatifu Joseph na kwenda kusalisha huko. Hakukuwa na simu, mawasiliano yalikuwa ni barua tu. Habari za Padri kwa walei wake ilikuwa wajibu wa Katekista kupita parokiani Dar es Salaam kujua Padri gani kama atafika huko vigangoni.

Kila jumapili ya tatu ya mwezi Padri alikuwa anafika huko na kusalisha misa, Padri wa akina mwanakwetu wakati huo alikuwa Agustino Fernandese huyu alikuwa mchanganyiko wa Baba-Goa na mama-Mmamkonde. Padri Fernandese alijulikana asili yake kwani alipofika hapo kusalisha alikuwa akikizungumza Kimakonde vizuri sana na Walei wengi ambao walikuwa Wamakonde, Wamatumbi na makabila mengine ambao walienda huku kufanya kazi kama watumishi (miongoni mwao walikuwa wazazi wa mwanakwetu)

Kuna wakati ilifika jumapili ya tatu ya mwezi wanamgonja Padri aje kusalisha muda ukawa unaenda Padri hatokei, ikabidi Katekista asalishe ibada bila padri, hadi ibada inakwisha padri hajafika. Katekista siku inayofuata alipanda basi hadi Dar es Salaam kuulizia parokiani ndipo alipojulishwa kuwa Padri alipata ajali ya pikipiki hii ilikuwa ni vigango vya Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati huo na huyu Padri aliyepata ajali alikuwa ni Padri Fernandese, alitibiwa na kupona

Mara ya pili ilikuwa ni Parokia ya Makere Kasulu-Jimbo Katoliki la Kigoma, Padri aliyepaswa kusalisha mwanakwetu anamkumbuka alikuwa Padri Balikumutwa, parokia hii ilikuwa na mapadri wawili huku wakipeana zamu, mmoja vigangoni mwingine parokiani. Padri alipata dharura na kujisikia vibaya, baadaye Katekista alifanya mawasiliano naye kwa kuwa alikuwa anaishi hapo hapo, baada ya nusu saa alikuja kuendelea na misa, hii ilikuwa mwaka 2000.

Kumbuka sasa mwanakwetu anaingia Kanisani la Bikira Maria Imakulata Parokiani Chamwino Ikulu-Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, nyimbo inaimbwa, Padri aonekani kwa sababu ya giza lakini mishumaa inawaka, kuna taa moja kanisani yenyewe ni ishara uwepo Yesu nayo haiwaki lakini mishumaa mwanakwetu inawaka.Waamini wapo lakini wachache kama watu 15-20 wanakwaya kama watano hivi, mwanakwetu akakaa katika benchi la katikati ambapo hiyo si kawaida yake. Kwa kuwa aelewi kinachoendelea basi wimbo ukaisha akaamka dada mmoja kuelekea kwenye marufaa ya kusoma somo akasoma somo la pili kwa kutumia tochi ndogo, nadhani ilikuwa ya simu kwani mwanga wake ulikuwa hafifu mno

Mwanakwetu akasema hii ni misa au ibada imeanza na hili ni somo la pili? Kwa hiyo akakaa mkao wa kusali. Msomaji wa somo alipomaliza, kwaya ikaimba wimbo wa kuelekea kwenye injili. Padri aliamka katika kiti chake kwa kuwa kulikuwa kiza ilishindwa kumuona awali, alipofika katika marufaa akachukua tochi yake akasoma injili huku vijana wahudumu wa misa wakimulika kitabu cha kusomea. Alipomaliza kusoma injili alianza kuhubiri.

Spika hazikuweza kufanya kazi, kwa hiyo mahubiri hayo mwanakwetu aliyasikiliza vizuri kwa sababu alikuwa katikati ya kanisa, nadhani mtu wa mwisho ilikuwa vigumu kuyasikiliza kwa ufasaha. Misa ilifanyika vizuri huku kwaya wakijitahidi kuimba kwa sauti ya juu ambayo kidogo ilificha ule uhaba wa umeme kanisani.

Alisimama mwenyekiti wa parokia alizungumza kwa kirefu sana juu ya umuhimu wa kutoa zaka na kusisitiza kila mlei kutambua umuhimu huo, aliyasema hayo huku akitolea mfano parokia ya Nkuhungu ambayo alidai kuwa imefanya vizuri katika Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma kwa mwaka 2021. Hata mwenyekiti huyu wa Parokia ya Chamwino Ikulu  alipotaka kusoma karatasi fulani ya nukuu ya maelezo yake alishindwa, ilibidi vijana wahudumu wamulike karatasi hiyo kwa tochi na akaweza kusoma.

Mwanakwetu akajiuliza moyoni ni kweli kanisa letu LUKU imekwisha? Akupata jibu. Lakini kila muda ulivyokuwa unasonga ndivyo mwanga wa kupambazuka ulivyokuwa unasaidia walei kuonana kanisani. Hoja ya kwanini leo tunasali bila umeme ilikuwa bado ipo kichwani na kwa umri wa mwanakwetu anatambua parokia haiwezi kukosa umeme kwa kuwa maandalizi ya misa/ibada ijayo yanaanza mara baada ya misa/ibada jumapili iliyotangulia kwisha. Lakini ikaja hoja kuwa labda umeme umekatika, mwanakwetu akalijibu hilo swali moyoni mwangu mbona nyumbani kwake ameacha umeme upo?

Padri alihitimisha misa hii kwa Amani ya Bwana.Hadi misa inamalizika hakuna umeme na nje ya kanisa hilo mvua kubwa ikinyesha.Mwanakwetu alitoka zake hadi Chamwino Stendi ili kumtumia pesa jamaa yake mmoja. Alipofika hapo simu yake iliishiwa chaji, kwa hiyo akamuomba kijana wa stendi amuwekee simu kwenye chaji ilikuisoma namba ya ndugu huyu ambaye anamtumia pesa

“Kaka umeme kwetu hakuna tangu jana, labda nikusaidie, toa lini yako uweke kwenye simu hii ndogo.” Aliambiwa mwanakwetu na kijana huyu wakala.

Hapo ndipo mwanakwetu akakumbuka kuwa hata kanisani umeme haukuwepo kisa umeme umekatika kwa siku mbili.Mwanakwetu alituma pesa hiyo kwa jamaa yake na kuondoka zake nyumbani kwake huko madongo poromoka.

Akiwa njiani alikumbuka miaka ya 1980 huko vigangoni Mkuranga wakati wakisali ibada za usiku wa sikukuu ya Krisimasi za bila Padri huko wakitumia Karabai za kuazima, huku ibada hizo zikiongozwa na Katekista wao.

 makwadeladius@gmail.com

0717649257.

 

0/Post a Comment/Comments