MWANAKWETU BINI KSAVELI–VI Kampuni ya Uwakili ya Geee Nangi

 

  

MWANAKWETU BINI KSAVELI–VI

Kampuni ya Uwakili ya Geee Nangi

Mwanakwetu alipochukua barua yake akaiweka mfuko na kutoka geti la Shiuta, hapo getini alikutana na mlinzi mmoja wa zamu na kuagana nae.

Mlinzi huyu mshika dini alisikitishwa na kilichotokea, akimwambia Mwanakwetu Bini Ksaveli kuwa haki Mungu ulipa na hata dhuluma ina malipo yake.

Alipotoka hapo alipanda basi la Mbagala na kufika nyumba aliyokuwa amepanga Mbagala-Misheni. Eneo hilo kwa asili linafahamika kama Mbagala Msalabani maana Wamisionari waliweka msalaba mmoja mkubwa enzi wakati wakielekea huko mikoa ya Kusini mwa Tanganyika kuupeleka Ukristo. Hapo msalaba ulianza kuwepo kabla ya ujio wa Misheni na ndiyo kusema Mbagala Misheni ilikuja baadaye na kujengwa kanisa dogo katika eneo hilo.

Mwanakwetu alipofika nyumbani kwake alimjulisha mkewe kilichotokea, maji yakishamwagika hayazoleki. Walikubaliana kurejesha nyumba waliyopanga kwa kuwa mke wa Mwanakwetu, Rozina Binti Yusufu wakati huo alikuwa amechaguliwa kujiunga na masomo ya Shahada ya Uzavivu wa Sheria (PHD) Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustone Ruaha Iringa hivyo kugharamia nyumba mbili mbili ingekuwa gharama kubwa.

Sambamba na hilo Rozina Binti Yusufu alikuwa na ujauzito wa miezi kadhaa, vyombo vilifungwa vizuri na kupelekwa nyumbani kwa Lyotela Bini Ksaveli mdogo wa Mwanakawetu na safari ya kuelekea Iringa iliwadia.

Wakafika Iringa naye Rozina Binti Yusufu alianza masomo yake vizuri na kwa siku za awali waliishi katika nyumba ya wageni karibu majuma mawili. Wakiwa hapo Mwanakwetu aliwatafuta rafiki zake kadhaa wa Iringa ambao ni walikuwa makada wa chama tawala hao wakiwa wenyeji wake hapo Iringa mmojawapo ni Mama Frank wa Mwangingo na alipoonana nae alimueleza juu ya kutafuta nyumba ya kupanga, pia alikutana na rafiki yake mwingine Mama Philipo wa Semtema na yeye alimjulisha juu ya kutafuta nyumba ya kupanga. Mwanakwetu alikwenda mbali zaidi na kumtafuta Bi Zainabu Kufakuonga mwenyekiri wa Mtaa wa Semtema naye alimueleza pia na yeye juu ya kutafuta nyumba.

Mwanakwetu katika maisha jitahidi sana kuwa na watu wengi ambao umekaa nao vizuri hao ni walinzi wako katika hali zote za maisha.

Kwa pamoja Mwanakwetu alipata nyumba tatu kwa Zainabu Kufakunonga, Mama Frank wa Mwangingo na Mama Philipo kwa kuwa nyumba hizo zilipopatikana Mwanakwetu alipata fursa ya kuchagua na alihamia nyumba ya Mama Philipo huku akiwashukuru mno Mama Franki wa Mwangingo na Bi Zainabu Kufakuonga kwa wema wao na nyumba hizo mbili Rozina Binti Yusufu mke wa mwanakwetu aliwaambia rafiki zake anaosoma nao waliohamia humo, ndiyo kusema nyumba zote tatu zilipata wapangaji.

Hapo sasa Mwanakwetu na mkewe wakawa wakazi wa Iringa nyumbani kwa Chifu Mkwawa Lilinga ngome isiyoingilika.

Maisha mapya ya Iringa yenye baridi ya kuvaa masweta na makoti yalianza, akiwa anatafakari hilo Mwanakwetu alikumbuka barua yake ya kuondolewa kazini ilikuwa na nafasi ya kukata rufaa,

“Unaweza kukata rufaa katika tume ya Usuluhishi na Maamuzi ndani ya siku 45 kuanzia tarehe uliyopokea barua hiii.Tunakutakia maisha mema.”

Hapo zikiwa zimeshapita siku 20, Mwanakwetu aliwakumbuka wanasheria watatu ambao alisoma na nduguze wa karibu, hawa wanasheria walikuwa na uwezo mkubwa wa kisheria tangu wakiwa wanachuo kwa bahati mbaya mmoja alifariki mara tu baada ya kumaliza chuo. Ahmadi kibindoni, Mwanakwetu sasa alikuwa na marafiki zake wawili wanasheria walio hai katika ulimwengu huu. Lakini kando alikuwa na mwanasheria wa nyumbani ambaye ni mkewe Rozina Binti Yusufu lakini alikuwa mjamzito hivyo harakati ya kuhudhuria mashauri ya Usuluhishi na Maamuzi aliona ni kumchosha.

Mwanakwetu alimtafuta mwanasheria msomi Mbikina Msumina lakini kumpata ilikuwa kazi kubwa hata namba yake ya simu alipoitafuta hakupatikana. Mbikina alikuw mwanasheria makini huku akiwa miongoni mwa warembo wa Tanzania wakati Mwanakwetu akiwa kijana. Alipowauliza marafiki wa Mbikina walimjibu kuwa Mbikina ameolewa na siku hizi anatawa na mumewe hataki kabisa awasiliane na watu. Duniani kuna watu wana wivu mkubwa kama huu wa mume wa Mbikina.

“Mbikina anafundishaa Chuo Kikuu cha Tumaini hapo Kurasini, wewe nenda chuoni waulize wanafunzi wanaosoma sheria wakupe ratiba yake ya vipindi alafu utaweza kumuona.” Rafiki wa mmoja wa Mbikina alimwambia Mwanakwetu.

Mwanakwetu alifika Kurasini na kukutana na wanachuo wa kitivo cha sheria alipowauliza walitoa ushirikiano na kumpa namba ya Mbikina japokuwa hazikupatikana. Kizuri walimjulisha ratiba yake wakimwambia arudi hapo chuoni hapo kesho yake.

Wakati anatoka hapo chuoni aliamua kupitia uhamiaji wilaya ya Temeke kusainisha fomu yake ili aweze kuhuhisha kibali chake cha kusafirisha akiwa Kando ya Uwanja wa Benjamini Mkapa alikutana na mwanasheria Geee Nangi akitokea mahakama ya Wilaya ya Temeke ambaye alisoma na mwnakawetu, yeye ni miongoni mwa mwanasheria waliofaulu katika kiwango cha juu mno huku kidato cha nne, kidato cha sita na hata Chuo Kikuuu alikuwa miongoni mwa wanafunzi bora vinara katika kitovo cha sheria.

Mwanakawetu aliyafahamua hayo tangu akiwa mwanachuo maana alikuw amjumbe wa kikao kimoja cha elimu hivyo jina la Mbikina Msumina na Gee Nangi yalikuwa majina vinara.Mwanakwetu alishusha pumzi na kusema Mungu Bahati ,“Huyu atanisaidia.”

Hapo alimsimulia kilichotokea Gee Nangi ambaye ni mmiliki wa Geee Nangi Advocates ambayo ni kampuni kubwa ya uwakili Afrika na Asia alisema wazi kwa Mwanakwetu “Wewe hauna pesa za kulipa kuendesha shauri hilo lakini nitakusaidia bure. Kesho saa 8 alasiri njoo na nyaraka zote ofisini kwangu pale Mtaa wa Ohio tuliweke sawa jambo hili.’

Siku iliyofuata alifika ofisini hapo na nyaraka zote na kujazwa fomu maalumu za ufunguzi wa shauri hilo katika tume ya Usuluhishi na Uamuzi Ilala Dar es Salaam na shauri hilo kufunguliwa kwa wakati na kupangia siku ya kusikiliza nyaraka za wito wa pande zote zilitolewa na nakala moja kupelekwa Shiuta.

Je kipi kitaendelea subiri sehemu ijayo.

0/Post a Comment/Comments