MWENYE MAJIBU MAZURI

 

 


 MWENYE MAJIBU MAZURI

Adeladius Makwega-Buigiri

Mtu anaweza kuja kwako akakuomba mkopo wa shilingi 5,000/- namna unavyomjibu ina maana kubwa sana kwa mtu huyo hata kama hautomsaidia jambo hilo, inawezekana wewe pengine ni mtu wa mwisho kuambiwa hilo, majibu mazuri ni jambo jema sana.

“Ndugu yangu hata mimi nimeuwawa, hali yangu si nzuri, ningekuwa nayo ningekusaidia.”

Jibu hilo linatia matumaini mno kwa yule aliyeomba msaada huo kwako. Katika maisha yetu binadamu wengi wanahitaji matumaini katika matatizo na changamoto wanazokutana nazo. Wewe unayekutana na mtu akakulilia shida yako jitahidi mno kuwa majibu ya hekima na majibu yenye dawa kwa shida ya mtu huyo.

Msomaji wangu Mei 16, 2019 mwanakwetu alitenguliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe tukio hilo lilitokea Dar es Salaam, alifika Halimshauri hiyo kukabidhi.

Alipofika hapo alikadhi na kuagana na wakuu wa idara katika kikao cha makabidhiano,

“Jamani mimi naondoka kama mlivyosikia, hayo ni maamuzi Rais John Magufuli kam alivyoteua, leo nafunga mizigo na nitaondoka kurudi nyumbani, nitakwenda kulima, kufuga na kujitolea kufanya kazi ya Ukatekista kwetu kijijini, nawatakia kazi njema.”

Maneno haya yana miaka mitano, kati ya waliokuwepo siku hiyo wapo waliofariki dunia na wapo wengi waliojaliwa uhai mpaka leo hii mioyoni mwao watakuwa mashuhuda. Kubwa mwanakwetu alirudi kijijini na kuanza shughuli zake za ufugaji, kilimo na huku akijianda kupata mafunzo ya Ukatekista.

Panapofanyika utenguzi wa Mkurugenzi Mtendaji, Katibu Tawala wa wilaya / mkoa na hata Katibu Mkuu wa Wizara hizi ni ajira za kudumu inakuwaje mwanakwetu anaamua kurudi kijijini?

Kwa hakika msomaji wangu jibu la hilo ni simulizi ndefu na ya siku nyingine. Kumbuka mwanakawetu anakuomba Mtanzania popote ulipo uwe raia wa kawaida, uwe mtumishi wa umma, uwe kiongozi wa ngazi yoyote nakupa siri heshimu sana Jeshi la Polisi Tanzania.

“Katika uchunguzi wa mwanakwetu alibaini kuwa Polisi mara nyingi wanafanya kazi na jamii kwa ukaribu na kufanya kazi na jamii kunafanya wao muda mwingine kuingia katika matatizo kama kushitakiwa, kulaumiwa, kuumia, kupoteza kazi na hata kuuwawa kwa kuwa wao wanavaa sare, wananamba na wanatambulika kwa haraka. Kubwa mwanakawetu anakuomba Mtanzania wape ushirikiano wa karibu ndugu zetu hawa,Wapo polisi wema sana, waadilifu mno na wanaipenda nchi yao Tanzania na wanapenda haki. Hata wewe wanaweza kukupa ushirikiano na kukulinda maana hiyo ni kazi yao kwa mujibu sheria.Heshimu sana askari anayevaa sare.”

Akiwa kijijini mwanakwetu alipigiwa simu na Lucianna Msofe ambaye ni karani wa Halimashauri ya Mbozi juu na barua yake inayohitaji mtu aipokee je anafanyaje?

“Asante kwa taarifa hiyo, nakuomba muombe Mkwama na Mwaikambo waipokee na wao watanisaidia inifikie.”

Walipoipokea walimjulisha na kumpa Zakayo Mwamahonje ambaye alikuwa Afisa Nyuki ambaye alikuwa safarini Dodoma na walikubaliana wakutane Dodoma ili kumkabidhi mwanakwetu.

Mwanakwetu alimchukua ndugu yake mmoja anayefahamika kama Pajero wakaifanyia service gari yake moja Land Cruzer I hz na kuwa tayari kwa safari ya Dodoma. Hii Land Cruzer 1hz huwa haiwashi mara nyingi, ni gari ya kazi, inatumika kwa dharura hasa kubeba maiti kama rafiki, ndugu, jamaa amefariki, mwanakwetu hii gari ya kazi maalumu.

 


Safari kutoka Kijijini kuelekea Dodoma ilikuwa ya usiku usiku na kufika Dodoma Mjini na kukutana na Zakayo Mwamahonje-Afisa Nyuki wa Wilaya ya Mbozi wakati huo.

“Unatakiwa kuripoti Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama Afisa Habari Mkuu masharti mengine ni kama masharti ya Utumishi wa Umma.”

Mwanakwetu aliripoti wizara hiyo Mtumba Mji wa Serikali na kuonana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu ambaye aligoma kumpokea kwa hoja ya barua hiyo haijapitishwa na Katibu Tawala wa Songwe wakati huo .

“Kweli arudi Songwe ikapitishwe? La haula la Kwata!”

Mwanakwetu aliomba kumuona Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo na alikutana na Naibu Katibu Mkuu ndugu Nicolous Wiliam Mkapa.

Kweli mwanakwetu alipokelewa na ndugu huyu na akamsikiliza vizuri sana,

Akamuita karani wake, akaagiza amtolee nakala barua yake alafu aeleze kilichotokea na ipelekwe masijala ya siri na yeye ataifanyia kazi na atamjulisha.

Katibu Mkuu wa TAMISEMI wakati huo Injnia Nyamuhanga aliipitisha barua hiyo na kumjulisha Katibu Mkuu Habari na baadaye mwanakwetu alijulishwa kupitia kwa Afisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari Maelezo Jonas Kamaleki ambae ni miongoni mwa wanahabari wakongwe na jambo hilo kwisha.

Mpango wa mwanakwetu kusomea Ukatekista ulishindikana baada ya kuwa na majukumu lakini anaamini katika matini hizi zinazoandikwa ni sehemu ya Ukatekista wake.

Mwanakwetu kwa siku ya leo anayarudia maneno ambayo yako mlangoni mwa makala haya,

Mtu anaweza kuja kwako akakuomba mkopo wa shilingi 5,000/- namna unavyomjibu ina maana kubwa sana kwa mtu huyo, hata kama hautomsaidia jambo hilo, inawezekana wewe pengine ni mtu wa mwisho kuambiwa hilo, majibu mazuri ni jambo jema sana.

“Ndugu yangu hata mimi nimeuwawa, hali yangu si nzuri, ningekuwa nayo ningekusaidia.”

Kisa hiki kinaandikwa na mwanakwetu kwa heshima zote kwa kuwa ndugu Mkapa sasa amerudishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kiongozi mwema mwenye majibu mazuri kwa wale anaowaongoza na jambo likifika kwake linapatiwa ufumbuzi.

Mwanakwetu anamtakia kazi njema ndugu Mkapa katika kujenga Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanakwetu upo

Nakutakia Kwaresma Njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257

0/Post a Comment/Comments