Adeladius Makwega-MWANZA
Tangu mwaka 2019 hadi Machi 12,
2023 mwanakwetu alikuwa akisali Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya
Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, huku Jumuiya yake ikifahamika
kama Mtakatifu Sesilia inayoongozwa na Mwenyekiti Bernard Lubogo jumuiya iliyo
mkono kulia wa Ikulu ya Chamwino. Katika kipindi chote hicho mwanakwetu amejifunza
mambo mengi ya maisha binadamu yawe ya kimwili na ya kiroho, huku wingi huo
kama yakiandikwa basi yanaweza kujaa kitabu chenye kurasa nyingi.
Siku ya leo msomaji wake
anatamani akusimulie tukio moja ambalo ninaamini jamii ya Wakristo na hata ya wale
Imani zingine wanaweza wakalitazama kama jambo hilo lina umuhimu basi
wakalifanya maana ni funzo kutoka katika Parokia hii ya Chamwino Ikulu.
Je jambo hilo ni lipi?
Ambatana na simulizi hii ya
siku ya leo hatua kwa hatua.
Mwaka 2022 Parokia hii Jumapili
mojawapo ilikuwa ni siku Wanaume Wakatoliki (UWAKA), siku hiyo iliamuliwa kuwa UWAKA
wote ndiyo wawe wahudumu wa kanisani, kabla ya misa na hata wakati wa siku ya
misa hiyo ya dominika. Jumamosi kabla ya misa hii wanaume hao walifika na kufanya
usafi wa kanisa lao na mazingira yote ndani na nje akiwamo mwenyekiti wa
Parokia hiyo Ndugu Komba na Katibu wake Dkt.David Msimbe.
Siku hiyo hakuwepo mwanamke
hata mmoja hivyo kila idara ya kukamilisha usafi na maandalizi ya misa ya
Jumapili wanaume walikuwa kazini, kila mmoja akiwajibika, wapo kanisani,
wengine nje kanisa na wengine walikuwapo vyooni. Kanisa lilifanyiwa usafi vizuri
huku frateri ambaye alikuwa anatokea Kongo(Zaire) akishirikiana na wanaume hao
Wakatoliki tangu mwanzo hadi mwisho.
Wakati zoezi hilo likiendelea
sabuni za kufanyia usafi ikawa imekwishwa, Baba anapokuwa nyumbani kitu
kikiisha anamuuliza nani? Jukumu lake kutoa pesa na kununua.Ndugu hawa waliokuwa
wakifanya usafi chooni wakaamua wakanunue sabuni hiyo dukani ili kukamilisha
usafi wa vyoo vyao vya Kanisa lao. Mmojawapo akaenda kununua sabuni duka
jirani. Hapo kulikuwa na duka nyuma ya kanisa hilo kuvuka Jiko la Nyerere (ambalo
ni jengo lililo jirani na kanisa hilo ikiaminika kuwa zamani wakati wa utawala
wa mwalimu Nyerere eneo hili lilitumika kumpikia chakula chake akiwa Ikulu ya
Chamwino na wakati huo eneo hili likiwa sehemu ya Ikulu). Alikwenda kununua
alijiongeza mno alinunua pakiti kadhaa za sabuni za unga na vipande na pia
alinunua dazeni ya pakiti za sodo za dharura.
Kama unavyofahamu mazingira ya
dukani wateja wanakuwa wanawake kwa wanaume wakawa wanashanga mbona ndugu huyu ananunua
dazeni nyingi za sodo ? Kushangaa ilikuwa haki yao lakini kuuliza walishindwa.Akabeba
mzigo wake hadi Kanisani.
Akafika na kuendelea na kazi
na kuchukua sabuni wakafanya usafi wa vyoo vya wanaume na wanawake ambayo
vilikuwa na vyumba kadhaa.Wakafanyia usafi vyombo vyote vya chooni pande zote
mbili. Upande wa wanawake ulikuwa na jaba mojawapo kubwa likajazwa maji vizuri
alafu mfuko wenye dazeni ya sodo ukaingizwa na kupachikwa eneo mojawapo vizuri.
Kabla ya kuwekwa sodo hizo hapo Katibu wa UWAKA wa parokia alijulishwa
kufanyika kwa jambo hilo.Aliyeshuhudia tukio hilo hakuweza kulikumbuka jina la
kiongozi huyu lakini aiba yake tu ilikumbukwa alikuwa mtu mmoja mrefu, mweusi
mwenye mwili wa uliojengeka. Kazi ikawa imekamilika milango ya vyoo ikarudishwa
vizuri tayari kwa matumizi ya wahitaji siku iliyofuta. Vyoo hivyo vya kisasa vilikuwa
na maji muda wote maana Kanisa hilo lina matenki makubwa ya kuhifadhi.
Jumapili ilifika na misa
kusaliwa vizuri, mama mmoja ambaye anasali hapo alisema sodo hizo zilipata
wahitaji, hoja ya kuandaa kupatikana kwake Zaidi ilianza lakini lilikuwa wazo
la mtu mmoja. Mtu huyo baadaye alijitahidi wakati jumuiya yake inapokuwa zamu
aliweza kushirikiana na akina mama kuweka sodo hizo katika vyoo vya wanawake,
kila jumuiya yake ikiwa zamu.
“Hizi sodo zinakaa muda
mchache maana mtu anaweza kuvutiwa kuchukua awezavyo, lakini hilo linaonesha
kuwa wahitaji wapo.” Mama mmoja wa Jumuiya ya Mtakatifu Sesilia alinukuliwa. Utafiti
ulibani kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa wanapita na kujihudumia siku ambazo
sodo hizo zilipokuwapo, inawezekana wanafunzi hao waliokuwa wanasali hapo waliwauma
sikio wenzao kupatika kwa bidhaa hiyo.
Wahitaji watakuwa wengi na
tendo hili linaweza kuwavutia hata wapita njia na kuona wema kwa walioifikisha
bidhaa hiyo na hata kuvutiwa na imani hiyo pia. Je tendo hilo kufanywa ni baya
au zuri? Huu ukiwa ni utaratibu wa jamii uliojiwekea wenyewe linakuwa jambo zuri
na la heshima kwa mwanamke.
Mwanakwetu mimi na wewe
tumeweza kuzaliwa baada mama zetu kuwa na afya njema ya uzazi, basi wewe na
mimi tufanikishe hilo kwa wahitaji ni kulinda afya njema ya uzazi kwa mwanamke
popote alipo. Tukio hili pengine haliweza kuwa linafahamika na wengi hata wanaosali
katika kanisa hilo la Bikira Maria Imakulata ndiyo maana mwandishi aliyelifuatilia
kisa hiki ameamua leo hii kukisimulia.
Naweka kalamu yangu chini kwa
kusema kuwa kama tendo hili ni la kiutu basi bila kujali imani zetu tuliige na
kama mwandishi amekosea kwa hisani yako msomaji wake anaomba radhi.
0717649257
Post a Comment