Hivi karibuni
mwanakwetu alizungumza na rafiki yake mmoja ambaye alitaka kujua kwanini hasemi
chochote juu ya kiongozi mmoja mkubwa wa taifa moja kutembelea taifa letu?
Mwanakwetu alijibu ni kweli hataki kuzungumzia kabisa jambo hilo kwa kuwa kwa miaka
zaidi ya kumi nyuma anafahamu msimamo wa chama kinachotawala katika taifa hilo
katika kuunga mkono mahusiano ya jinsia moja. Anachoamini yeye hata kumtaja
jina lake, kumuandika au kupachika picha yake kiongozi huyo kwa namna yoyote
ile ni kuunga mkono msimamo wao katika hilo.
Je inakuwaje kujisogeza
jirani naye?
Hilo mwanakwetu
hana jawabu lakini anavyoamini yeye ndiyo hivyo.
“Mafiga yanayopachikwa
chungu lazima yalingane, kinyume chake chungu hakiwezi kukaa mekoni na chakula vigumu
kupikwa na kuiva.”
Mwanakwetu alimuongezea
nduguye huyo.
Ili kumfahamu huyu
ndugu huyu yeye ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu ya Sheria, akisema mwanakwetu
umezungumzia suala la maadili, hilo ni jambo la msingi mno kwa watoto, vijana
wetu na taifa letu pia.
Mazungumzo hayo
yalipamba moto na baadaye mwanakwetu kusimuliwa kisa hiki cha kweli cha mtoto
wa msomi huyu.
“Nina kijana wangu
anasoma Chuo Kikuu sasa, yu mwaka wa tatu, mwaka jana nilishangaa anaingia
nyumbani kwangu yupo yeye na binti amebeba mtoto. Kama baba nilishangaa, ebo
sasa nimepata mjukuu? Mbona sijashiriki kulipa mahari na harusi? Nikawauliza
hapo hapo huku wamesimama, haya kulikoni? Chuoni kwema? ‘Baba ni kwema huyu
ninasoma naye chuoni na nilikuwa nakaa nae, tukapata mtoto, ndiyo hivyo tena na
leo nimekuja naye hapa nyumbani’ Hiyo ndiyo digrii niliyokutuma ukasome? ‘Baba
hapana, nimekosa, naomba msamaha.’ Haya na wewe mama hiyo ndiyo kazi waliyokutuma
wazazi wako ukafanya huko chuoni? ‘Hapana baba ilikuwa ni bahati mbaya tu.’ Ndugu
yangu mwanakwetu nilikaa kimya kwa dakika tano huku wao wamesimama, mke wangu
ananitazama na wanangu wadogo wako pembeni, nikawauliza jina la huyu mtoto, walivyokuwa
washenzi wamempa jina langu, nikawaambia nani kawaruhusu kumpa jina langu mtoto
wenu? Hakuna jibu lililotolewa. Nikasema kumbe sasa mwanangu umekuwa mkubwa na
umeyaanza majukumu, nakupa hongera sana (hongera ya dhihaka alisema moyoni baba
huyo), sasa wewe, mkeo na huyo na mtoto wenu sitaki kuwaona katika nyumba hii
ninayolala mimi, mke wangu na wanangu wadogo. Nakuomba sasa hivi beba kilicho
chako ukakae kule nje katika banda la uani na kuanzia leo uanze kujitegemea
maana maisha unayaweza na ndiyo maana umemchukua binti wa watu unakaa naye
unyumba, sintakupa chochote, sasa anza kujitegemea.”
Msomi huyu alisema
kuwa Kweli kijana huyu alichukua vitu vyake na kuhamia katika kibanda hicho na
kuanza maisha huku wakifanya vibarua vidogo vidogo akimtunza binti huyu
aliyezaa naye. Walikaa hapo hadi likizo ilipoisha walirudi chuoni.
“Kaka wakirudi tena
likizo ya pasaka nafungisha ndoa waendelee na maisha yao.”
Ndugu huyu alimwambia
mduguye mwanakwetu, hizi tabia siyo nzuri na lazima wazazi tuwe wakali katika haya
mambo ya haki za watoto yana shida sana leo na hata kesho yao badala ya kusoma
vizuri sasa wana majukumu ya kutunza mtoto
Mwanakwetu
akamwambia hilo ni sahihi maana hata wanao wadogo watakuwa wamejifunza kuwa wakijaribu
kuingia huko balaa kama hilo linaweza kuwambuka kama la kaka yao. Ungefanya kosa
kubwa kama ungekaa kimya na pale unapomuambatanisha mtu mwema na mtu mwovu,
hoja itakuwa kama ile ya mafiga jikoni chakula hakiweza kupikika.
Mwanakwetu akasema
mara zote jamii inachukizwa na tabia mbaya na inavutiwa mno na mtoto/kijana mwenye
tabia nzuri. Kama anavyofahamika mtu mwovu na hata mwema huwa anajulikana na
kupendwa na wengi kwa mwenyewe kufahamu au kwa kutokufahamu. Mwanakwetu akaamua
kumsimulia ndugu huyu simulizi hii,
“Kaka Kati ya mwaka
2005-2008 nilikuwa mwanachuo cha Tumaini Iringa nikisoma na wanachuo wengi,
kuna nyumba moja alikuwa akiishi rafiki yangu anayefahamika kama Hendry Msaki,
ndani ya nyumba hiyo walikuwapo wapangaji kati 25-30 wanachuo tupu wakike kwa
wakiume wenye tabia tofauti. Nyumba hii nilikuwa nikienda kuwatembelea rafiki
zangu kadhaa. Miongoni mwa wanachuo waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo
alikuwepo dada mmoja anayefahamika kama Deborah ambaye alikuwa anasoma Shahada
ya Kwanza katika Uongozi wa Biashara (BBA). Binti huyu alikuwa na sifa kubwa nne
ya kwanza ni mtulivu mno, pili ni mshika dini, tatu alikuwa anajiheshimu sana na
nne alikuwa na umri mdogo kuliko wote katika nyumba hiyo. Msaki na mwanakwetu
hawakupenda Deborah aonewe na mtu yoyote yule awe chuoni, awe anarudi anapokaa au
katika makazi hayo maana upole wake, utulivu wake uliwavutia mno kaka zake hao.
Deborah akiwa mwanachuo gafla ilisikika amefunga ndoa, wengi walitamani kujua Deborah ameolewa na nani? Mbona hatukumuona huyo mchumba wake kaja kumtembelea? Mbona
hatukuona pete ya uchumba? Lakini Deborah alikuwa sasa ameolewa. Kumbe kaka yao
akina mwanakwetu, waliokuwa wanafanya naye siasa ndugu Addo Novemba Mwasongwe ndiye
aliyefunga ndoa na Deborah Binti Mtulivu.”
Mwanakwetu alipomaliza
kumsimulia nduguye huyu msomi wa sheria yeye alisema kuwa watoto/vijana wengi wanapotea
sana kwa kutokuwa makini na maisha yao huku wakivutiwa na maisha ya kimaigizo
ya wazungu. Kweli mazungumzo haya yalimalizika na kila mmoja kuendelea na
ratiba yake ya siku hiyo.
Swali ambalo lilibaki
wakati huo lilikuwa huyo aliyemuoa Deborah alimfahamia wapi? Mbona hakuwa mwanachuo?
Mwanakwetu akamwabia rafiki yake Hendry Msaki ambaye sasa ni marehemu kuwa kama
kinavyofahamika kibaya na wabaya na hata kizuri kinafahamika zaidi na wazuri. Hilo
walifahamiana wapi litabaki kwao wenyewe Deborah na mumewe Mchungaji Addo
Novemba Mwasongwe. Deborah huyu anayezungumziwa leo hii ndiye Mke wa Mchungaji huyo.
Mwanakwetu kwa heshima zote ametumia kisa cha Deborah Mama Mchungaji kujenga
matini yake juu ya maadili kwa vijana wetu popote walipo baada ya kukiacha tu
kisa cha wanachuo waliopeana uja uzito kusimama pekee. Kwa hoja moja kubwa
mazuri lazima yasemwe zaidi. Mwanakwetu kwa matini haya anatawakia maisha mema
ya ndoa ya familia hiyo ya Mchungaji Addo Novemba Mwasongwe popote walipo siku
ya leo.
Kwako wewe msomaji wangu
kumbuka kuwa, “Mafiga yanayobeba chungu yanafanana.”
Nakutakia siku
njema.
0717649257
Post a Comment