Adeladius Makwega-MWANZA
Miaka ya 2000 mwanakwetu
alikuwa mkaazi wa Iringa Mjini na baadae akawa akienda huko na kuondoka hadi
mwaka 2011, mji huu ambao ulikuwa Ngome ya Mkwawa LILINGA. Katika maisha yake
katika eneo hilo alifahamu mengi ya watu wengi wa eneo hilo lenye historia moja
kubwa ya Tanzania na kidunia. Akikutana na watu wengi wasomi wa mkoa, wanasiasa
na hata wanahabari wa kitaifa na kimataifa waliotapaka ulimwengu mzima.
Mwanasiasa ambaye alikutana
naye kwa karibu na hata kufika nyumbani kwake ni marehemu Josephy Mungai ambaye
alikuwa na urafiki wa karibu sana ni mwanahabari mkongwe Majidi Mjengwa.
Kumbukumbu za mwanakwetu
zinamrejesha wakati huo kuna siku moja alialikwa nyumbani kwa mheshimiwa Mungai
ambaye alikuwa waziri katika serikali kadhaa za awamu hizo. Makazi ya
mheshimiwa Mungai yalikuwa katikati ya Ofisi za CCM Wilaya Iringa Mjini na Chuo
cha Ruaha, jirani na makazi ya akina Abri hawa wafanyabiashara wa Iringa.
Waziri Mungai alikuwa na nyumba yake moja ya kawaida tu haikuwa nyumba ya
kibepari akiishi yeye na familia yake, huku watoto wake wengine wakubwa
waliashanza maisha yao maeneo mengine, hapo akiishi yeye, mkewe na watoto wake
wadogo.
Mwanakwetu alipofika hapo
alibaini kuwa palikuwa na sherehe ya siku ya kuzaliwa ya mtoto wa mheshimiwa huyu
mdogo na waalikwa wengi walikuwa ni watoto labda walikuwa wakisoma na mtoto
huyu. Hapo mwanakwetu alikutana na mwanahabari mkongwe Majidi Mjengwa,
mwanakwetu akasema kumbe hayupo peke yake, akapata mtu wa kuongea naye. Kwa heshima
waliyopewa mwanakwetu na Mjengwa walingizwa sebuleni kwa mheshimiwa Waziri
Mungai. Sebule hii ilikuwa ya kawaida tu yenye makochi machache, mapazia ya
kawaida, meza ya kulia chakula na picha ya mheshimiwa Mungai ukutani.
Kumbuka katika ua wa nyumba ya
waziri ndipo sherehe inafanyika watoto na vijana wakicheza muziki. Mama mwenye
mji huu akaagiza wageni wa Waziri Mungai wapewe vinywaji. Binti mhudumu akapiga
goti mbele ya Mjengwa na mwanakwetu, Mwanakwetu akiwa bado hajaoa lakini
Mjengwa akiwa ana mke na watoto kadhaa. Mwanakwetu alikuwa na ruhusa ya kutia neno
la mapenzi kwa binti mhudumu nyumbani kwa waziri, lakini Mjengwa alikuwa hana
kibali hicho maana kufuri ya ndoa ilimbana.Hata kama Mjengwa angetia neno kwa
binti huyo mwanakwetu akamchoma kwa mkewe mara moja, lakini hili halikutokea.
“Haya tuwaletee nini?” binti huku
kapiga goti alisema, waungwana hawa wakaagiza soda kwa pamoja. Hapo sasa mwanakwetu
akatambua kuwa Majidi Mjengwa siyo mnywaji wa maji yalee.
Waagizwaji wanacheka,
inakuwaje ndugu hawa vijana wenzetu wanakunywa soda? Muonekano wa Majidi
Mjengwa mtu mwembamba alionekana kijana mdogo kumbe alikuwa kaka mkubwa kwa
mwanakwetu.
Kwa mazingira ya Iringa watu
wengi wanakunywa pombe ya ulanzi na pombe zingine, mazoezi ya kunywa Ulanzi
tangu utoto yanampa mtu uzoefu wa pombe na kumbuka Ulanzi una hatua kadhaa
zenye utamu mwingi unavutia mtu kunywa hadi kuwa pombe kamili.
Mama mheshimiwa akasema sasa wageni
wenyewe wa soda waleteeni boksi za juisi kila mmoja.
Msomaji wangu tambua kuwa
mheshimiwa Mungai alikuwa waziri aliyefanya kazi tangu Nyerere, Mwinyi na Mkapa.
Waungwana hao wapo hapo wanakunywa juisi huku wanaongea habari zao, kiongozi wa
mazungumo hayo alikuwa Mjengwa akasimulia simulizi nyingi na ya kwanza ilikuwa
ya Mfalme Umekaa Vibaya simulizi hiyo ikaisha baadaye ikaja simulizi ya Siyo Kila
Anayekupa Kitu Anakupenda.
Dhana ya Mjengwa siku hiyo ilijengeka
katika kisa cha mama mpishi aliyepo jikoni anapika, mandhari ya jikoni sakafuni
yupo paka aliyevutiwa na mapishi ya mama, paka anampapasa miguuni mama mpishi na
huku paka huyu ambaye siye pakashume akivutiwa na harufu ya mapishi ya mama mwenye
nyumba. Mama anampikia mumewe akirudi kazini ale. Paka anamgasi mama na
kumtambaa miguuni. Mama mpishi anakerwa na tabia hiyo huku akimfukuza paka awe
mbali naye lakini paka anaendeleza na vurugu zake, mara kamramba miguu mara kampalamia,
mara kamkwaruza, mama mpishi anarusha miguu na kumsukuma kando paka huyu.
Ghasia hizo zikamkera mama
mpishi hivyo akachukua upawa akachota kipande cha nyama chanye fupa lililokaa
kama kisu na akamtupia paka huyu mwenye uchu na mapishi yanayopikwa mekoni.
Paka alipotupiwa akalifakamia
fupa hilo, likamuunguza na kumkaba kooni. Mama sasa anaendelea na mapishi na
alitoa finyango hilo si kwa kupenda bali kuondoa kero ya kupapaswa, kukwaruzwa
na kusumbuliwa na paka ili aweze kupika vizuri na kumgoja mumewe aje kula
chakula hicho. Fupa lile likamsumbua paka likamnasa koo na kumbana pumzi
likasababisha paka akafa.
Kumbuka hapo juisi zipo mezani
kazi ni simulizi, boksi za juisi zikisafiri kutoka mezani kwenda koonimandhari
ni nyumbani kwa mheshimiwa Waziri Mungai.
Gafla zikasikika hatua za
viatu vya kiume zikishuka ngazi akatokea mheshimiwa Mungai kutokea ngazi za juu
ya nyumba yake hii, akawasalimu huku Mjengwa na mwanakwetu wakisimama kwa
heshimu zote, ukafanyika utambulisho kidogo alafu soga zikapamba moto. Mheshimiwa
Mungai akaagiza waungwana hao waletewe vinywaji Zaidi, hapo sasa boksi za juisi
zilijaa mezani, huku wahudumu wakiwacheka zaidi wageni wa mheshimiwa waziri wanakunywa
juisi ?
Kiongozi wa mazungumzo haya sasa
alikuwa mheshimiwa Mungai huku wanahabari hao wakayanukuu maelezo yake kwa kutumia
kinasa sauti cha mwanakwetu. Sherehe iliendelea hadi saa moja usiku na ilipoisha
Mjengwa aliwakusanya watoto wake na kurudi zake kwake naye mwanakwetu alirudi
nyumbani kwake huko Mwangingo.
Msomaji wangu tambua kuwa
tangu Majidi Mjengwa wakati huo alikuwa akiandika makala, chambuzi na habari mbalimbali
katika magazeti maarufu yote na maelezo haya yalipamba katika vyombo vya habari
mbalimbali baada ya kikao hicho na mheshimiwa Mungai.
Mwanakwetu anasema nini siku
ya leo?
Msomaji wangu tambua kuwa
mwanakwetu amemkumbuka kaka yake Majidi Mjengwa, huku akijenga tafakari ya ule
mwaliko nyumbani kwa mheshimiwa Mungai na pia anakumbuka hiki kisa cha cha mama
mpishi mekoni, kubwa siyo kila anayekupa kitu anakupenda.
Swali ni je Mungu anaweza
kuufilisi ulimwengu na kukosa watu rahimu? Hilo haliwezekani maana wapo watu
ambao wanaweza kumpa mtu kitu huku wakimpenda
Mwanakwetu mpaka leo bado
anakunywa juisi na soda, lakini anajiuliza je kaka yake Majidi Mjengwa katika
kipindi chote cha miaka 20 aliyemwaacha Iringa je Ulanzi ulimshawishi kuunywa?
Kaka Mjengwa je umefuzu kuanza
kunywa maji yale mengine ?
Mwanakwetu upo?
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment