Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu hivi karibuni alisafiri
kupitia katika vijiji kadhaa vilivyo katika tumbo la mikoa mitatu; Mwanza, Simiyu
na Shinyanga huku akifaidi mno pale alipotumia bodaboda kwani katika ardhi hiyo
ndiyo anafika kwa mara ya kwanza tangu azaliwe.
Safari hii kwa hakika ilizidi
kumpa picha ya hali ya hewa na mwenendo wa matokeo ya mvua za mwaka huu wa 2023
katika mashamba ya wakulima wetu. Safari ya bodaboda ndiye ilimpa picha ya wazi
mno huku macho yake yakikaribishwa na majani makavu ya mahindi yenye kimo
kifupi yaliyokauka kana kwanza wakati wa kuvuna umekaribia lakini hayakuonesha
kubeba chochote .
Hali hiyo ilianzia Malya huku
mwanakwetu akienda eneo la Hungumalwa, hayo yakiwa majira ya jioni. Barabara
ilikuwa ya vumbi lakini inayopitika vizuri sana ilimpa picha labda ilikuwa
ikingoja mkandarasi aje kuweka lami.
Sasa walifika Kijiji Cha Lyoma,
njiani walikutana na makundi matatu ya mifugo yenye ng’ombe wengi, mbuzi na
punda wachache. Walitoka kijiji hicho walikwenda mwendo kidogo na kufika Kijiji
Cha Busule na hapo pia walikutana na makundi mawili ya mifugo mingi wachungaji
wakiwa nyuma yao.
Wakafika Kijiji cha Mwakulilinga
alafu wakafika Kijiji cha Mwakulyambiti hapa walikutana shule moja nzuri ya msingi
yenye majengo imara na mazuri yaliyojengwa zamani .
“Mna shule nzuri za msingi, zenye
majengo mazuri, uzoefu wangu wa kuzunguka katika katika maeneo mbalimbali huwa
naikosa mandhari hii ninayoiona leo hii.”
Mwanakwetu alimwambia kijana
huyu wa bodaboda.
Safari iliendelea na walifika
Kijiji cha Mwamakoye hapo hawakuona kundi la mifugo barabarani lakini makundi
mengi yalikuwa yanaoneka mashambani. Kijana wa bodaboda akasema kuwa unayaona
yale makundi ya mifugo hayapo barabarani bali yanalishwa mashamba ya mahindi
maana mahindi mwaka huu yamegoma kabisa. Malisho haya si hapo tu bali tangu
kule Malya.
Kijana huyu akasema kwa miaka
mingi ambayo kilimo kinakuwa vizuri ni vigumu mfugaji kuweza kupitisha mifugo
mashambani msimu huu maana hilo litakuwa hatari kubwa kwake na mifugo yake.
Kumbuka msomaji wangu inaendelea
wakafika sehemu wakakutana na watu wakianua juani choroko zao na kuziweka
katika magunia, tayari kusafirishwa, hapo zilionekana gunia kama nne hivi. “Hawa
jamaa wamebahatisha mno kupata hizo choroko zao, wanatakiwa kuzitunza sana
zitawafaa mno hapo baadaye.” Kijana wa Bodaboda alisema.
Sasa iliendelea wakawa wanakaribia
Hungumalwa, kabla ya kufika hapo walipita sehemu walikutana watu wanakunywa
pombe katika baa moja, kijana huyu wa bodaboda akasema kwa hali ilivyo mwakani inawezekana
hata vilabu vya pombe vikapungua maana hayo mazao ya kupika pombe yatatoka
wapi?
Wakafika mbele kidogo
wakakutana na kundi la ng’ombe kubwa barabarani, hapo mchungaji wala
hakuangaika kuwasogeza ng’ombe zake pembeni.“Kaka unajua matajiri wa ng’ombe wanaogopa
magari tu si kinginecho na ndiyo maana hawahaingaiki kuziswaga kando.”
Bodaboda haiwezi kumpa madhara
ng’ombe labda wewe ukimgonga ndiyo utaumia mwanakwetu alimwambia.
Safari iliendelea na baada ya
muda midogo mwanakweru alifika Hungumalwa ambapo alibani safari hiyo ilikuwa ya
saa nzima. huku akiambiwa kuwa kwa basi ni safari ya saa moja na nusu na kwa baiskeli
saa tano na kwa miguu ni safari ya siku nzima.
Kumbe ujio wa bodaboda umeokoa
saa 11 za kutembea kwa mguu kutoka Malya kwenda Hungumalya.Kwa kuwa mida huo
ulikuwa Jioni kuelekea usiku mwanakwetu alifika Hungumalwa na kulala.
Kwa hakika mandhari aliyoiona
katika vijiji alivyovitaja na vingine vingi ambavyo majina yake hakuweza kuyanukuu
vizuri hali ya hewa inachangamoto. Kwa yule mwenye ndugu zake maeneo hayo kama
atapigiwa simu kuelezwa juu ya hali ya hewa ilivyo atambue kuwa hilo ni la
kweli. Kwa mazingira aliyoyaona watu kunywa pombe ni kwa muda tu na pengine mazao
ya mwaka jana ndiyo yanayotumika kufanya hivyo.
Mwanakwetu anatambua kuwa
kuyasoma, kuyasikiliza na hata kuyaona haya ni hatua ya kwanza na kuyatatua ni
hatua nyingine.
0717649257
Post a Comment