Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu alikaribishwa na
mandhari ya mji mdogo wenye nyumba za aina mbili za zamani-kongwe zenye bati
zilizoota kutu na nyumba bora za kisasa. Alipozitazama alibaini za zamani
zilipigwa bati kitambo hata kuanzia mwishoni mwa mwaka 1969 hadi kuendelea
maana alibaini nyumba moja ambayo ilikuwa na jengo kama ya Waajemi ilikuwa na
chapa ya mwaka 1971, hii ni nyumba ya zamani, kando yake aliona duka la dawa.
Aliingia dukani hapo nakununua
dawa za mafua kwani alipatawa na mafua kutokana na kusafri safari ya vumbi ya
saa kadhaa tangu alipopanda basi ndogo pale Hungumalwa.
“Kaka lipa shilingi mia tano
tu.”
Dada muuzaji wa duka hili alimwambia
mwanakwetu. Hapo dukani alitumia nafasi hiyo kumuuliza mambo kadhaa mhusika
huyu ikiwamo ramani ya Mji wa Malya hasa pande zote za dunia Mashariki,
Magharibi, Kusini na Kaskazini na maswali mengine lukuki, swali la mwisho
lilikuwa pahali lilipo Kanisa Katoliki Malya.Mazungumzo haya na dada wa duka la
dawa yalimpa picha kubwa mwanakwetu juu ya eneo hilo kuwa Malya ipo mpakani mwa
Wilaya/Mikoa miwili ni Maswa(Simiyu) na Kwimba(Mwanza).
Hilo lilimpa picha pia kuwa
mji huo ni wa zamani sana na watu wake wana maandeleo ya muda mrefu hata kabla
ya uhuru maana taswira za nyumba bora za bati zilizopata kutu ni za miaka mingi
na majengo ya zamani inatoa ushahidi huo huku wakijishungulisha sana na kilimo
na ufugaji
Mwanakwetu alitambua kuwa mtu
maarufu ambaye ni mzaliwa wa eneo hilo na yupo katika Utumishi wa Umma ni
Profesa Eliezer Mbuki Feleshi ambaye aliwahi kuwa Jaji lakini sasa ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mwanakwetu alitamani kufahamu tabia ya kiongozi
huyu kwa nduguze wa Malya-Kwimba na Mwanza.Je anafika kama nduguze wakimtafuta
pale wakiwa na shida? “Anapatikana na hata tukiwa na shida tunamueleza na
anatusaidia sana.”
Hilo mwanakwetu aliliuza kwa
hoja moja kubwa, watu wenye nafasi kubwa wajitahidi kuwa wanafikika kwa urahisi
maana wananachi wanaweza wakadhulumiwa haki yao na mtu mwovu, kama yupo mkubwa
serikalini wanamjulisha na hilo linaweza kutatulika kwa haraka.
Wananchi wanapoongea na ndugu
yao iwe wa kabila moja, imani moja au mahusiano yoyote ya karibu wanaweza
kulisema jambo bila woga wala kuhofia chochote. “Ukiwa mkubwa mwanakwetu
anakushauri uwe unafikika kwa urahisi na hata wema/ ubaya wa mtu yoyote
unaanzia nyumbani kwake.”
“Mzee wa Kisukuma akishakuwa
na ng’ombe katika zizi kubwa na watoto wake wa kike kwa wakiume wakiwa wakubwa zamani
walikuwa na desturi ya kukaa yeye na mkewe na kuzungumza,’Mke wangu naona zizi
limekuwa kubwa, mimi nakuaga ninaondoka na ng’ombe 200 wewe baki na ng’ombe
hizi 300 zako wewe na watoto wako, mimi nakwenda kuazisha mji mwingine.’ Mkewe atamuuliza
sasa mimi unaniacha na nani?’Wewe ni mke wangu baki hapa hapa mimi nitakuwa
nakuja.’ Huyu baba anaondoka zake na kwenda kuanzisha mji mwingine huko mbali.”
Mwanakwetu akauliza sasa
kwanini walikuwa wanafanya hivyo?
“Hekima ya Wazee wa Kisukuma
ni kwamba panapokuwepo na mafanikio makubwa shetani huwa anakuwa karibu,
unaweza kushangaa mama kampikia mumewe chakula kizuri alafu akamuwekea mumewe
kitu cha kufisha akafariki. Hiyo ilikuwa ni busara yao ya kukata zizi.”
Wakiwa katika mazungumzo hayo
mara akatokea mama mmoja mtu mzima, mwanakwetu akatambulishwa, mama huyu wa
Kisukuma akauliza huyu mgeni ana mke? Ndugu huyu aliyekuwa na mwanakwetu
akasema mama muulize mwenyewe. Mama huyu akawa anacheka, tafsri ya kicheko
hicho ni kuwa swali limesikika kwa mwanakwetu.
Mwanakwetu kuumaliza mzizi wa
fitna akajibu kuwa nina wake wanne. Mama huyu akacheka mno alafu akasema baba
hata nafasi hamtuwekei? Mwanakwetu akajibu kuwa katika wake zake wanne atampa
talaka mmoja alafu nafasi hiyo atampa yeye. Mama huyu akajibu kuwa hapo haiwezekani,
nafasi gani za kutafuta. Mimi nataka kuwa huru ninaona hapo kwako nafasi
zilishajaa.
Mwanakwetu aliendelea na
shughuli zake hapo Malya akakutana na madaktari wawili falsafa kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, msomi mmojawapo mwanakwetu alimkumbuka kuwa waliwahi
kusoma wote, mwanakwetu alipomuona tu alimkumbuka kwa haraka lakini alikaa
kimya kuona kama na yeye msomo huyo analikumbuka hilo? Hadi mwanakwetu anatokomea
msomi huyo hakukumbuka hilo nadhani ana majukumu mengi ya kusomesha wanafunzi
wetu hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwanakwetu akasema akikutana naye siku
nyengine msomi huyu atamkumbusha.
Uwepo wa mwanakwetu hapo Malya
uliendelea sasa alikutana na mwlaimu kijana ambae alitambulishwa ugeni wa
Kazimbaya Makwega, Mwalimu huyu alishituka sana, baadaye alimuuliza juu Mwalimu
Kazimbaya wa Chilrombora Ulanga Morogoro. Mwanakwetu alijibu kuwa huyu ni baba
yake mdogo.
Mwalimu huyu akaomba mkono wa
mwanakwetu, mwanakwetu akampa mkono, alafu mwanakwetu akauliza mbona umeomba
mkono wangu?
“Yule mzee wakati nikiwa mdogo,
baba yangu alistaafu, akatuacha jirani na shule aliyokuwa anafundisha mwalimu
Kazimbaya. Baba alituagize tukiishiwa pesa tuwe tunachukua kwa Mwalimu
Kaizmbaya, kweli hilo lilifanyika kwa kipindi chote hadi baba akapata pesa zake
kustaafu na sisi tukahama hapo, tukio hilo hadi kesho ninalikumbuka, ndiyo
maana nimekupa mkono kwa heshimu ya Mwalimu Kazimbaya.”
Mazungumzo ya ndugu huyu
yalikuwa ya kidugu mno na baadaye mwanakwetu aliomba nambari ya bodaboda
anayemuamini na kweli mwanakwetu alipewa na kijana huyu kufika hapo na
kumzungusha eneo hilo la Malya na kubaini kuwa hapo kuna mradi mkubwa wa
serikali ulikuwa SGR.Huku Madhari ya ujenzi wa madaraja na tuta la njia za reli
na barabara ujenzi ukiendelea.
Kumbuka msomaji wangu mwanakwetu
yupo akizunguka katika eneo hili la Malya, Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza.
Je mwanakwetu leo anasema
nini?
Kubwa ni umuhimu wa kufanya
wema popote ulipo, watu wanaweka kumbukumbu, kumbuka wema wa Profesa Eliezer
Mbuki Feleshi kwa ndugu zake. “Anapatikana na hata tukiwa na shida tunamueleza
na anatusaidia sana.”. Pia mkumbuke mwalimu wa Chilombora Ulanga Morogoro,“Baba
alituagize, tukiishiwa pesa tuwe tunachukua kwa Mwalimu Kazimbaya.”
Mwanakwetu upo?
Kama mema yanawekewa kumbukumbu,
kumbuka hata mabaya yanaweza kuwekewa kumbukumbu pia lakini mwanakwetu anasema kumbuka
kulipa ubaya kwa wema.
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment