Lucas Masunzu- MAKOLE
Mwaka 2017 nduguyetu alikuwa anaishi wilaya mojawapo
inayopatikana Mkoa wa Tabora. Wilayani huko alibahatika kukutana na watumishi
wa umma kadhaa ambao walikuwa wakifanya kazi katika ofisi mbalimbali za umma katika
wilaya hiyo. Kwa muda alioishi na hao watumishi aliweza kubaini kuwa watumishi
hao walitofauti katika umri, vyeo, dini, elimu na hata vimo vyao katika upembuzi
wa mambo walitofautiana. Wenye umri mkubwa ndio watawahi kustaafu, kuruhusu
wengine kuingia kwenye huo utumishi halafu wenye umri mdogo wataendelea kubaki
kwenye foleni nao wakisubiri muda wao wa kustaafu! Hii ni kwa sababu utumishi
wa umma ni wa muda mfupi mno, kipenga cha kuanza kazi kikipigwa kumbuka pia
kuna muda kipenga hichohicho kitapigwa kukuengua kwenye utumishi huo maana tayari
muda wako wa utumishi utakuwa umetamatika.
Miongoni mwa watumishi hao wa
umma, nduguyetu alibahatika kukutana na mtumishi wa umma ambaye ni Shaaban
Mgasi ambaye alikuwa ni mtu mwenye mwili uliojengeka kiasi, mpole, mvumilivu
mno na mwenye kupenda haki. Mbali na utumishi wa umma alikuwa ni mkulima hodari
wa mahindi na miwa. Kiumri mtumishi huyo alikuwa amebakiza miaka michache ili astaafu
katika utumishi, apokezane kijiti na wale wanaoingia katika utumishi huo. Kubakiza
miaka michache na kustaafu ni uneemevu pia ni ngekewa kubwa mno kwenye utumishi
wa umma kuna nongwa na kadhia lukuki, ukikutana na mstaafu asikuache bure ongea
nae anaweza kutengeneza darasa lenye tija kwako, ana mengi mno ya kukusimulia kwa
maana umri wa miaka 60 amekutana na mambo mengi, amefanya kazi na watu
mbalimbali wakiwamo wema na wale wenye nia ovu.
Jumapili moja Nduguyetu
alikuwa amepumzika na nduguze chini ya mti wa mhama ambao ulikuwa karibu na
duka. Kwa mbali alionekana mtu akitembea kwa mguu, akivalia kibalagashia
kichwani kwake. Alipokaribia alikuwa ni mtumishi wa umma aitwaye Shaaban Mgasi
ambapo tulifanya jaliko, tukampisha kwenye benchi ili aketi maana wote alituzidi
umri. Kwa hisani yake mtumishi huyo wa umma aliwanunulia
soda kwenye duka lililokuwa karibu na mti huo wa mhama nao wakanywa. Nduguyetu
na marafiki zake walifurahi sana wakaendelea na mazungumzo yaliyodumu kwa muda
wa saa moja na dakika 49. Kwa kuwa aliwazidi umri na uzoefu, mtumishi huyo alitawala
mazungumzo hayo, huku akituambia;
“Utumishi wa umma una mambo mengi unapofurahia
haki yako katika utumishi huo hakikisha haukanyagi haki za wengine, wawe
wakubwa hata wale unaowaona ni wadogo wapatie haki yao, katu usiwe kizuizi wa
kuikanyaga, wapo wanaokanyaga haki za wenzao kwa hila zao mbaya, kama
mtabahatika kuwa viongozi katu nyie msiicheze hiyo ngoma! Pia, unapokuwa na
cheo kiwe kikubwa au kidogo katika utumishi wa umma ishi na watu unawaongoza
kwa usawa, usifanye upendeleo wa aina yoyote, kamwe usitumie nia yako ovu
kunyanyasa wengine, dunia ni duara. Hata kama utakutana na mabaya yapokee tu ili
maisha yaendelee mengine kashitaki kwa Mungu wako aliyekuumba. Mimi katika
utumishi wangu mpaka sasa sijawahi kutenda hata kufikiria kuyatenda haya mabaya”.
Mazungumzo yalipamba moto,
mtumishi huyo akasema “ngoja niwape nongwa mbili alizokutana nazo rafiki yangu katika
utumishi wake wa umma”. Tulikaa kimya kusikiliza huku tukiendelea kunywa soda
alizotununulia. Alianza kusimulia kisa kilichompata rafiki yake hapo kale.
“Mwaka 1989 rafiki yangu mmoja
(kwa sasa sijui aliko) alikuwa Mkuu wa Shule katika moja ya shule kubwa ya
Wavulana nchini. Siku moja mpishi mmoja wa zamu alibainika kuiba kilo za unga zilipowekwa
kwenya mzani zilikuwa ni zaidi ya kilo arobaini za unga wa mahindi. Kilifanyika
kikao kikakubaliana kuwa hilo ni kosa. Mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo alisema
ndiyo maana watoto wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata mchinjo (chakula kidogo)
kwenye mlo. Mpishi alikiri kufanya hilo, kikao kikaamua mpishi huyo aandike
barua ya kukiri kufanya kosa kwa rejea za baadaye huku wajumbe wa kikao hicho
wakiomba busara itumike kumsamehe mpishi huyo ukizingatia kuwa mpishi huyo amekubali
kufanya kosa hilo. Baadaye kitendo cha kuandika maelezo kilimuuma mno mpishi
huyo aliona kuwa ameonewa na hajatendewa haki, akaamua kwenda kutafuta msaada
anakojua yeye”.
“Mkuu wa shule ananitaka
kimapenzi nimemkataa ameamua kunibambikizia kesi ya wizi wa unga” mpishi huyo
aliamua kupika uongo huo na kila alipopiga hodi mpishi huyo alisema maneno hayo
ili ahalalishe kitendo kiovu alichokifanya.
Mtumishi huyo wa umma
aliendelea kusimulia “utata wa nongwa hiyo ulizidi kukua, masikini alichokiambulia
rafiki yangu ni kuvuliwa cheo chake na kupelekwa kituo kingine cha kazi kama
adhabu”. Ndugu yetu alidakia akasema inawezekana alitafuna pesa za umma ndiyo
maana akaondolewa”. Mtumishi huyo alisema “rafiki yake anamfahamu vizuri ni
mwaminifu mno, dini yake pia kaishika vizuri mno hawezi hakufanya hivyo
abadani! Kuna mengi katika utumishi wa uuma”. Mtumishi huyo wa umma alisisitiza
hivyo.
Jambo la msingi ni lipi kwa siku ya leo?
Mosi, unapofurahia haki yako
katika utumishi wa umma hakikisha haukanyagi haki za wengine. Pili, katika
utumishi wa umma ishi na watu unaowaongoza kwa usawa, usifanye upendeleo wa
aina yoyote vilevile usitumie nia yako ovu kunyanyasa wengine. Tatu, cheo
ulichonacho unaweza kuvuliwa kwa nia ovu za watu katu usikate tamaa endelea
kuwatumikia wananchi kama alivyofanya rafikiye Mgasi.
Nongwa ya pili imebaki
kibindoni, NITAKUSIMULIA SIKU NYINGINE. Kwa heri.
0762665595
2023.
Post a Comment