VIATU VYA MVUA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Majuma matatu yaliyopita mwanakwetu alikuwa katikati ya Jiji la Dodoma kuwanunulia wanawe jozi kenda za viatu vya mvua, kwa kuwa alikuwa katikati ya jiji hilo na wanawe wapo Lushoto Tanga alielekea eneo la Makole CBE Stendi ya Basi na kufika ofisi ya basi la Burudani linalofanya safari zake Dodoma Lushoto Dodoma.

Kampuni hiyo ni pekee inayofanya kazi zake njia hiyo, japokuwa yapo mabasi mengi yanyokwenda Tanga Mjini. Kwa mtu ambaye haifahamu vizuri Lushoto, yenyewe ipo Tanga lakini ni mwendo kidogo huku hali ya hewa ya Lushoto ikitafautiana kabisa na ya Tanga Mjini. Kumbukumbu za mwanakwetu zinaonesha kuwa kumekuwa na harakati ya kuanzisha mkoa mpya ukianzia Lushoto na wilaya jirani.Harakati hizo zipo katika makaratasi na makabrasha ya ofisi zetu za umma na vikao kadhaa.

Mtazamo wa Lushoto ikiungana na wilaya zingine jirani kuunda mkoa mpya, majina kama Mkoa Usambaa na hata Mkoa Shambalai yakitajwa. Kijiografia Lushoto inapakana na Korogwe-Tanga huku ikipakana na Same-Kilimanjaro.

Hiyo jiogrfia na mambo ya maofisini, kumbuka mwanakwetu yupo na mhusika wa basi hilo alipokea mzigo huo na kudai shilingi 10,000/- akalipwa na mzigo huo kusafirishwa na kufika salama Lushoto Tanga. Mzigo ulipokelewa walionunuliwa viatu wakakimbilia na kuvivaa. Baada ya kujaribu kila mmoja mwanakwetu akapiga simu kuongea nao mmoja baada ya mwingine. Siku hiyo alizungumza nao kila mmoja kwa siri akiwa amejifungua chumbani ili wenzake wasisikie mazungumzo hayo ili wawe huru hata kama mmojawapo kaonewa asema kwa uhuru.

Mazungumzo yaliyofungua dimba na Joshua Makwega, yeye alisema hana maneno, anashukuru amepata juzi nne za viatu vya mvua bali saa yake ya mkononi ya kimweku mweku imekatika mkanda, mwanakwetu alimjibu kuwa atamnunulia nyingine. Aliufungua mlango wa chumba hicho alichokuwapo na kumuita Joseph Makwega. Nayeye aliingia ndani ya chumba hicho na baada Joshua kuondoka alisema manane haya,

“Baba asante kwa viatu lakini mvua haijanyeshi, natamani inyeshe ili niyavae mabuti yangu shuleni, maana nimepata juzi tano. Huko Dodoma mvua inanyesha? Kama inayesha ningehamia huko ningekuwa navaa viatu vyangu vya mvua kila siku nabadilisha.”

Mwanakwetu akawa anachekea ndani kwa ndani, sauti haitoki lakini miguno inasikika, alafu akasema hata huko Dodoma mvua hainyeshi mwanangu labda mara moja moja tu.

Joseph Makwega ambaye mwanafunzi wa darasa la sita alisema, “Baba kama mvua hainyeshi hivi viatu vyangu vitaharibika.” Mwanakwetu akachekea moyoni alafu akasema mvua itanyesha tu na viatu vyako utavivaa sana. Moyoni mwanakwetu akasema kumbe kweli, kipyaaa kinyemiii...“Baba kumbuka ninafanya mafundisho ya Komuniyo ya Kwanza, sista anaendelea kutufundisha, kumbuka kunifanyia sherehe.”

Mwanakwetu akamjibu kuwa hilo halina neno, sherehe itafanyika bali kumbuka kusoma vizuri maana kuna maswali atakuuliza Padri Kimario Paroko wa Lushoto kabla ya kupewa Komuniyo ya Kwanza.

“Mwanangu tunaandaa sherehe, alafu unakwenda kwa Padri kuulizwa maswali wanasema Joseph Makwega kashindwa kuyajibu? Hapama Baba Sista wetu anatufundisha vizuri nitayajibu vizuri ninayo Katekisimu Yetu.

Simu hiyo akapewa ndugu wa watatu na Joseph kuondoka zake, huyu anafahamika kama Albert Makwega yu darasa la saba yeye alikuja na hoja ya malalamiko ya kukosa viatu vya mvua. Kumbuka jozi zilizonunuliwa ni tisa Joshua kapata nne na Joseph kapata tano. Je Albart kapata nini? “Baba inakuwaje umenunua jozi tisa, alafu mimi nikakosa hata jozi moja?”

Mwanakwetu alitoa majibu kuwa vipimo alivikosea, hilo halikuwa kusudio lake aliomba msamaha na kutoa ahadi ya kumnunulia vingine. Mwanakwetu alimuuliza maendeleo ya shuleni na akaeleza namna wanavyofanya mitihani ya pamoja ambayo inashirikisha shule kadhaa za Lushoto na Mkoa wa Tanga. Pia alimuuliza mwanae huyo juu ya mafundisho ya Kipaimara maana alikuwa anatambua kuwa wanasoma shuleni kwao Saint Catherine Lushoto-Tanga.“Sista Mkuu alikuwa anatufundisha tangu mwaka jana lakini tangu tufungue tumesimama kusoma mafundisho yetu, ametuambia atatufundisha, wenzetu wa Komuniyo wanasoma au Kipaimara nitakwenda kupata nikiwa kidato cha Kwanza?, Au hatusomi kwa kuwa Askofu amefariki? ”

Mwanakwetu alijibu hapana, Kipaimara mtapata tu na sista ataendelea na mafundisho, hayo na anajua amewafundisha sana huku akibakiza kidogo. Mwanakwetu aliendelea kumwambia mwanao huyo kuwa ni kweli Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tanga alifariki mwaka 2020 naye alikuwa ni Mhashamu Askofu Antony Banzi aliliongoza jimbo hilo kwa miaka 26 tangu mwaka 1994 wakati huo yeye alikuwa ni mwanafunzi wa sekondari.

Kabla ya Askofu Banzi alikuwepo Mhashamu Askofu Telephore Mkude aliyehudumu tangu mwaka 1988 hadi mwaka 1993. Nyuma ya Askofu Mkude alikuwepo Mhashamu Baba Askofu Maurus Komba alifanya utume wake kwa jimbo hilo tangu mwaka 1970-1987 lakini Askofu wa kwanza kabisa wa Jimbo hilo alikuwa ni Eugene C Arthur, LC akiliongoza jimbo hilo tangu mwaka 1953 hadi1969.

“Kumbe akifariki anachaguliwa mwingine?” Mwanakwetu alijibu ndiyo.

“Wangemchagua haraka ili tuweze kupata Kipaimara mapema maana tusije tukaenda kusoma tena mafundisho ya Kipaimara tukiwa kidato cha kwanza.”Mwanakwetu akajibu kuwa tuombe Mungu, Baba Mtakatifu Fransiko aliyepo huko Vatikani ambaye ndiye anayewachagua Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki amchague Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tanga.

Mwanakwetu mazungumzo hayo ya simu yalimazika huku akiwa na deni ya kununua viatu vingine vya mvua. Machi 27, 2023 alinunua jozi mbili za viatu hivyo na sasa za kiwekumweku atavituma kwenda Lushoto Tanga.


Mwanakwetu anasema nini leo hii?

Maswali hayo ya wanawe ameona ni busara sana na hekima kama akayaweka katika maandishi ili Askofu Mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatikani nchini Tanzania asome, awasikie walei hao watoto na hamu yao ya kupata Askofu wao. Nayeye Askofu Mkuu Accatino pengine akamuuma sikio Baba Mtakatifu Francisko juu ya jambo hili.

Mwisho kabisa kuiandika simulizi hii mwanakwetu alikumbuka wakati ananunua jozi mbili za viatu hivyo lakini aliponunua alikumbuka Albart Makwega ni mpenzi timu ya Yanga je ataweza kuvaa hii jozi ya viatu vyekundu vya mvua? Hilo ni lake mwenyewe baba mtu katimiza wajibu wake.

Mwanakwetu upo?

Nakutakia Kwaresma Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments