Adeladius Makwega-MWANZA
Kijana mmoja alikuwa akifanya biashara katika Mji wa Lushoto,
mkoani Tanga Tanzania. Kwa utaratibu wa biashara za mji huo wafanyabiashara wana
maduka mjini, vijijini na kwenye magulio yanayozunguka kama yalivyo maeneo
mengine duniani.
Mizigo yao inapomalizika basi wao hufunga safari katika miji
mbalimbali kufungasha bidhaa hizo na kusafirisha mizigo hiyo hadi Lushoto eneo
lenye milima na mabonde.
Ufungashaji huo huwa Zanzibar, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro,
Arusha, Mombasa na hata Ulaya na Asia.
Siku moja kijana mmoja bidhaa zake zilikuwa zinakaribia
kuisha hivyo alikusanya fedha kutoka kwa watu aliyokuwa wamekopesha na kununua kwa
mali kauli au taslimu. Zoezi hili lilipokamilika safari ya kwenda kuchukua
mzigo wake iliwadia, huku maamuzi yalikuwa afunge safari hadi Tanga.
Kweli alifika Tanga na kununua na kufungasha mizigo yake
vizuri akiwa katika kununua bidhaa hizo hapo kwa tajiri huyo alikutana na
mwenye mali binti mmoja mrembo, alipomtazama alivutiwa na urembo wake kijana wa
Kisambaa akatia neno la mapenzi. Usumaku wa mapenzi uliwateka wote na pingamizi
la mapenzi hayo halikuwepo.
Urafiki huo wa kijana huyu aliona una tija sana kwake akivutiwa
na binti huyu namna anavyofanya biashara nyingi. Sasa biashara ziliendelea na
huku mapenzi yakiendelea, sasa kijana huyu alituma pesa kwa mabasi yanayofanya
kazi Lushoto Tanga na dada huyu kuzipokea na kumfungashia mzigo na kutumwa na
kumfika bila shida yoyote ile. Jambo hilo lilisaidia mno kupunguza gharama za
kusafiri , kulala na chakula.
Jambo hilo likawasaidia biashara zao kushamiri huku binti
huyu akiunganishwa na wafanyabaishara wengine wa Lushoto waliokuwa na urafiki
na kijana huyu na wakawa wateja wa binti huyu.
Biashara ikaendelea na huku mahusiano hayo ya kimapenzi
yalipamba moto, binti huyu wa Tanga sasa akawa anafika Lushoto kwa mpenzi wake
katika makazi ya familia ya kijana huyu yaliyopo kando ya Deustch iliyokuwa shule
ya Wajerumani.
Wakati mahusiano hayo yanapamba moto yanayokwenda sambamba na
biashara binti huyu mfanyabiashara aliamua kumueleza neno kijana huyu wa
Kisambaa.
“Mpenzi wangu nashukuru sana kwa kunipenda, lakini sasa siku
zinasonga mbele , mimi nakufahamu wewe , wazazi wako, ndugu zako na kwenu
Lushoto lakini wewe haukufahamu kwetu hivyo nakuomba sasa umewadia wakati
sahihi na wewe ukapafahamu nyumbani kwetu na kwa wazazi na ndugu zangu ili
tuweze kufunga ndoa.”
Kijana huyu mfanyabiashara wa Lushoto alivutiwa mno na kauli
hiyo,
“Hilo ni jambo sahihi kabisa kwani wapendanao ni kufahamiana
na kujua nyumbani kwa mpenzi wako, maana kwenye mapenzi kuna uzima na mauti
linapotokea shida kila mmoja anakufahamu kwa mwenzake na vibaya kuishi bila
ndoa.”
Kweli walikubaliana na kijana huyu alimwambia mpenzi wake
kuna atakuwepo Tanga juma linalofuata ambapo atafungasha na mzigo, akimaliza
mzigo utatumwa Lushoto na yeye atakwenda huku kwa ndugu wa mpenzi wake.
Msomaji wangu sasa kijana huyu alikuwa na maduka kadhaa
katika maeneo yote yaliyochangamka katika Wilaya hiyo huku maisha yake yakiwa
bora kuliko awali.
Siku zilisonga na kijana huyu kufika Tanga na kufunga mzigo
vizuri na kuituma kwa Malori yanayokwenda Lushoto Milimani.
Binti huyu akamwambia mpenzi wake,
“Leo nakuomba tulale katika nyumba ya wageni alafu kesho
tutaondoka kuelekea nyumbani kwetu maana muda umeshasonga itakuwa si vizuri
kufika nyumba kwetu wakati jua limezama.”
Mwanakwetu hilo lilifanyika hivyo hivyo
wakala chakula na wakaenda kulala katika nyumba ya wageni.
Wapendanao sasa wapo katika nyumba ya wageni , watu wenye
mahusiano ya mapenzi ya muda mrefu wamezoeana na kuaminiana kabla ya kulala
binti huyu aliingia kwenda kuoga bafuni. Kijana huyu nayeye kama siku zote alitamani
aoge pamoja na mpenzi wake huko bafuni huku joto la Tanga likiwashawishi waoge
maji ya baridi.
Binti huyu aliingia bafuni naye kijana huyu akasogelea mlango
wa kioo wa bafu hilo la kisasa,
“Siku ya leo nataka nioge mwenye, naomba nisubiri huko
kitandani nimalize kuoga na wewe utakwenda kuoga baadaye.”
Kijana huyu alirudi kitandani baada ya kupewa ilani hiyo
mpya, akajilaza kitandani, kwa kuwa alikuwa na uchovu wa safari na kazi kubwa
ya kufungasha mizigo siku nzima, akiwa hapo kitandani usingizi ulimpitia
akalala fofofo.
Akiwa amelala kwa saa kadhaa gafla mbele akashituka mbona
nipo mwenyewe? Mwezangu yu wapi? Mbona nasikia maji kama mtu anaoga? Kweli
tangu muda ule anaoga tu? Kijana huyu alimuita jina lake dada huyu hakuna
aliyeitika, akaamka kitandani na kwenda bafuni kuchungulia kulikoni?
Mwanakwetu huyu alipofungua mlango alibaini kuwa yule binti
alikuwa bado anaoga, lakini cha kustajabisha katika sinki la kupigia mswaki
chooni aliona kuna vitu vimerundikwa , alipotazama vizuri aliona moyo , maini
figo na matumbo ya binadamu, huku tumbo la binti huyu likiwa wazi , binti huyu
akiendelea kulisafisha sehemu ya wazi ya tumboni tu .
“Eee mwezangu vipi? Bado unaoga tu, kulikoni tena mbona
hivyo? Hayo mazingaombwe gani?”
Kijana huyu alistajabu anachokiona.
Binti huyu alimtazama kwa jicho kali alafu akamwambia ,
“Si nimekwambia leo naoga mwenyewe kitu gani kimekuleta huku
bafuni?”
Kijana huyu alishituka mno na akarudi kitandani katika namna
ya ajabu bila yeye kufahamu. Akapatwa na usingizi wa ajabu bila ya kutaka kama
mtu aliyechomwa sindano na nusu kaputi. Gafla alijiona yupo katika ulimwengu
mwingine kabisa chini ya bahari na yupo na huyu binti akimtambulisha kwa
nduguze.Kijana huyu alishangazwa na mandhari hayo ya kuzungukwa na maji mengi,
wakati yeye amezoea mandhari ya mabonde na milima ya Lushoto huku maji yakipita
katika vijito tu.
“Huku ndiyo kwetu na hawa ni ndugu zangu na hawa ni wazazi
wangu, kama nilivyokwambia tunakuja kwetu ndiyo hapa chini ya bahari, si unaona
samaki wale wakubwa kwa wadogo hao ni jamaa zetu hawana madhara na sisi. Usinione
kule dukani, huku ndipo ninapotoka. Sasa hapa hapa tunafunga ndoa.”
Kweli ndoa hiyo ilifungwa chini ya bahari, muda huo huo na
huku kijana huyu akijiuliza mbona wazazi wangu kule Lushoto hawafahamu kama
ninafunga ndoa? Lakini alijipa moyo kuwa wazazi na ndugu zake wanamfahamu binti
huyu kwa muda mrefu?
Harusi hiyo ilipomalizika kijana huyu alishituka kutoka katika usingizi huo wa ajabu na kumekucha ni asubuhi wapo kando ya bahari yeye na huyu binti. Kijana huyu sasa anashangaa anamuuliza huyu binti mbona tupo hapa? Si tulikuwa tupo hotelini na wewe ulikuwa unaoga? Binti akamjibu huku tunatoka kwetu kama nilivyokueleza na tumeshafunga ndoa.
“Mbona inu n’deuzi ni ya mazingaombwe!”
Kijana huyu alijisemea moyoni kwa Kisambaa kwa kustajabu akimaanisha kuwa mbona ndoa hii ni ya mazingaombwe.
Kijana huyu akawa amekasirika kwa anachokiona siku hiyo,
wakagombana hapo ufukweni, binti akimwambia kijana huyu warudi hotelini lakini
kijana huyu akagoma akisema kuwa yeye anarudi Lushoto nyumbani kwao. Alifika
sehemu yanaposimama malori ya mizigo ya Lushoto hapo alikutana na Lori
linapakia mzigo, lilipomaliza alipanda mbele na wenzake kuelekea Dochi. Alipofika
hapo alimfuata mama yake mzazi ambaye alikuwa mama mtu mzima sana, mama huyu
aliamfuata Sharifu na kumueleza kilichotokea kama kilivyo kwa kijana wake, hiyo
sasa ilikuwa usiku wa siku hiyo aliyotoka Tanga.
Sharifu alimwambia kuwa kesho yake asubuhi kukicha tu jambo
lake la kwanza aende akanunue ubani Sokoni alafu afike nyumbani kwa Sharifu
akiwa yeye na mama yake ili mambo wayamalizwe.Kweli kulipokucha mama huyu alitangulia
kwa Sharifu huku kijana huyu alidamkia sokoni, akanunua ubani na kupanda vigari
vidogo akafika eneo linalofahamika kama Mbura na Kushuka sasa ili aenze safari
ya kwenda kwa Sharifu.
Aliposhuka hapo kulikuwa na mtu yupo upande wa pili wa barabara
alimuona akasema ngoja nimsalimie, akavuka barabara akamsalimia akamuaga na
wakati anavuka barabara ili aelekee kwa Sharifu, kijana huyu aligongwa na gari
hapo hapo akafariki dunia.
Kumbuka mama yake yupo kwa Sharifu wanamgonja kumbe kijana
wake amegongwa na gari na kufariki dunia. Mama huyu alijulishwa hilo huku ubani
ulimwagika katika ajali hiyo na hata kilichotaka kufanywa hakikufanyika. Nyumba
kukawa na msiba na kijana huyu akazikwa.
Kweli alizikwa huku mama yake akisimulia kilichotoikea
ndunguze kama kilivyosimuliwa na mwanakwetu hapo juu.
Unapotaka kuwa na kitu kuwa makini sana, zipige picha kwa
umakini mkubwa nia zako je zinalingana na nia za upande wa pili? Je hakuna nia
ovu kwa mwenzako? Je mwenzako huwa anatabia yakuwa na nia ovu katika mambo
yake? Kwa kufanya hivyo kunaweza kukusaidia kutojiingiza katika matatizo kama
ya huyu kijana.
Kibinadamu unaweza kuyaona manufaa ya leo tu katika mahusiano
yoyote na mtu, kikundi, taasisi au upande mmoja na mwingine. Baadhi ya mambo
yanaweza kukuaminisha kuwa upande fulani ni wema kumbe hilo ni chambo tu kama yalivyotumiwa
mahusiano ya kimapenzi na biashara katika kisa hiki.
Mwanakwetu tuwe makini kwa maana jambo hilo wengi linawashinda
kung’amua.
Nakutakia siku njema
makwadeladius @gmail.com
0717649257
Post a Comment