Adeladius Makwega-MWANZA
Ndugu huyu alikuwa akihamahama na familia yake kutoka eneo
moja kwenda lingine, kumbukumbu za mwanakwetu zinanukuu uhamisho wa awali
ulikuwa ni wa kutoka Tambi kwenda Berege alafu ukaja uhamisho wa kutoka Berege
Kuelekea Sagara. Hayo yakiwa ni majina ya vijiji vilivyopo kwa sasa katika
Wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma.
Maisha yake katika vijiji vya Tambi na Berege huko mwanakwetu
alikuwa mtoto mdogo, hapo hakumbuki kitu lakini alipohamia Sagara sasa mwanakwetu
alikuwa kidogo akijitambua. Mtoto anayejitambua si vizuri kushinda nyumbani na
kuwinda vipepeo na ndege, iliamuliwa awe anakwenda shuleni kujifunza kusoma,
kuandika na kuhesabu na wenzake.
“Hapo sasa walimu wake walikuwa wakimsaidia kuumba herufi na
kurekebisha silabi na irabu zilizokuwa zinapiga tikitaka.Wakiandika angani , ardhini
na baadaye katika vibao vyeusi.”
Shule ya Msingi Sagara ilikuwa na wanafunzi wengi kutoka
maeneo ya vijiji kadhaa wengine wakitoka milimani huku wengine wakitoka
mabondeni. Eneo hili lilikuwa na hali ya hewa ya tafauti na maeneo mengi ya
Dodoma maana mvua zilikuwa zinanyesha huku vyanzo kadhaa vya maji yaliyosambazwa
maenneo jirani, hilo liliambatana na kiimo cha nyanya vitunguu, kabichi na
mboga mboga zingine.
Hiyo ilikuwa mwkaa 1981, mwanakwetu anakwenda shuleni kusoma
lakini hajaandikishwa kuanza darasa la kwanza nia aweze kujua mbinu za shuleni.
Wanafunzi wote wa Shule ya Msingi Sagara walifanya mitihani yao ya kufunga
shule muhula wa kwanza, walimu wakaipa alama mitihani hiyo na siku ya kufunga
shule ilifika. Utaratibu ulikuwa ikifika siku ya kufunga shule wanafunzi wote
na walimu wanakutana pamoja katika Baraza la Shule na mara nyingi eneo lenye kivuli
au kwenye mti mkubwa, walimu wakikaa katika meza na madawati machache mbele,
huku wanafunzi wote wakikaa chini katika mchanga.
“Jukumu la kikao hicho lilikuwa kwanza kuyasomwa matokeo yote
ya shule nzima kutoka darasa la kwanza hadi la saba, alafu ikiambatana na
kutaja wanafunzi wa kwanza hadi wa tatu wa kila darasa wakipewa zawadi mbalimbali
kama vile mikebe, madaftari kalamu za risasi na kalamu za wino wa kujovya,
zawadi hizo na zingine nyingi zilitoka katika stoo ya shule ambazo zililetwa na
serikali mashuleni nchi nzima jukumu la mwanafunzi/mtoto ilikuwa kusoma tu yeye
na kichwa chake.”
Mkuu wa Shule alipomaliza kufanya zoezi hilo aliwapongeza waliofanya
vizuri na kutaja tarehe ya kufungua shule.
Kwako msomaji wangu ngoja nikuume sikio kuwa siku hiyo ndugu
yetu mwanakwetu alikuwa mwanafunzi wa 72 katika darasa lililokuwa na wanafunzi zaidi
ya 100. Hii msomaji wangu ni siri kubwa kaa nayo moyoni, usimwambie mtu. Mwanakwetu
shule hiyo ilifungwa, wakiwa katika likizo baba wa mwanakwetu alipata uhamisho
aliouomba ili aweze kurudi kwao Pwani huku yeye na mkewe wakiwa watumishi wa
umma. Kweli mizigo ilifungwa huku wakiuza mifugo kadhaa kama vile mbuzi, kondoo
na ng’ombe waliokuwa wakifungwa katika vijiji vya Berege na Sagara .
Walisafiri kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, wakafika Mbagala nyumbani kwao na kukaa kidogo na baada ya siku kadhaa walianza safari ya huko Mkerezange Kisarawe Mkoa wa Pwani. Walipanda basi hadi Kimanzichana na hapo wakashuka na mizigo yao akiwepo baba, mama na wadogo wawili mwanakwetu.
Wakiwa Stendi ya Kimanzichana kugonja usafiri wa kwenda Mkerezange ambacho ni kijiji lilichopo kati ya Kimanzichana na Mkamba lilinunuliwa tunda mojawapo ambalo lilikuwa na vipele vipele. Baba wa mwanakwetu akachukua vipande kadhaa na kumgawia mwanakwetu na wengineo. Mwanakwetu alichukua punje ya njano ya tunda hilo na kuanza kula tunda moja.Baba wa mwanakwetu akasema ,
“Mwanangu hizo mbegu usizile, wewe kula nyama ya njana na
mbegu ngumu unaitupa, hizo mbegu huwa zinaliwa kama zinachemshwa, ni tamu kama
gimbi au kiazi mviringo , mbegu yake ni chakula kamili chenye wanga.”
Tunda hilo likamshinda mwanakwetu kula kabisa maana lilikuwa na
sukari nyingi. Hapo akamrudisha baba yake . Kwani tunda hilo linaitwajwe? Alimuuliza
mama yake. Mama yake akamwambia muulize baba yako hata mimi limenishinda kula.
“Hili tunda linaitwa fenesi linatokana na mti unaoitwa mfenesi
linaliwa likiwa limeiva, unaweza hata kulila na uji na chai, yanastawi mno
katika mikoa ya Pwani yenye joto na mvua kiasi japokuwa hata katika maeneo baadhi
yenye baridi mfenesi unastawi. Mti mmoja unakuwa na matunda kati ya 100-200
ambapo tunda moja lina KG kati ya 20-30. Wanagu haya siyo matunda ya uchoyo,
ukipanda mti wake utakula na wengi na ndiyo matunda ya Pwani. Kama zilivyo furu
Dodoma. Kama limewashinda leo kulila mtalizoea tu haya ndiyo matunda ya kwenu.”
Baba huyu aliyeyasema maneno hayo kwa hakika kwa sehemu kubwa ya utoto alikulia Mbagala na
Kilindoni Mafia hivyo matunda kama fenesi, matope tope , mabungo, mastafeli
madoliani yalikuwa si mageni kwake, shida ilikuwa kwa mama wa mwanakwetu
mzaliwa wa Kilimatinde Manyoni Singida ambaye hapo alikuwa anaambatana na
mumewe kuhamia Pwani.
“Mwanamke akiolewa, kwake ni ada kumfuata mumewe popote alipo
labda kwa makabila mengi ya Lindi na Mtwara ambayo ukoo ni wa mama, je hiyo
inatambulika Kiserikali kwa mwanaume kufuata mkewe?”
Kumbuka mwanakwetu hapo alikula fenesi kwa mara ya kwanza,
baadaye alizoea mno akila zaidi na zaidi huku akibaini kuwa mti huu una asili
ya India na mbao zake zinatumika kama kuni na hata kutengenezea samani
mbalimbali za majumbani.
Maisha ya Mkerezange yaliendelea vizuri, hiki kilikuwa kijiji
chenye matunda mengi kama machungwa, machenza, ndimu nyingi, minazi na
mikorosho. Sagara na Mkerezange zilitafautiana kiasi. Sagara wakiwa na mifugo
wakati Mkerezangu haikuwepo, Mkerezange walikuwa na matunda ya pwani lakini Sagara
walikuwa na zambarau na matikiti mengi.
Wazazi wa mwanakwetu walikaa hapo kwa muda mchache na
kuhamishiwa Kijiji cha Kimanzichana ambacho kwa hakika kilikuwa kijiji
kilichochangamka mno kuliko kijiji chochote kutoka Mbagala maana wakati huo
biashara mbalimbali zilifanyika saa 24.
Je hali hiyo ipo mpaka
leo?Hilo mwanakwetu anajiuliza na hajafika huko muda mrefu.
Hapo mwanaketu ilikuwa ni mwaka 1983 na aliandikishwa darasa
la kwanza na kuanza kusoma rasmi maana mkono wake ulikuwa sasa umeshika sikio
vizuri bila ya kujilazimisha.
Masomo ya darasa la kwanza yaliendelea vizuri huku mwanakwetu
akimkumbuka rafiki yake Mohamedi Kindundusi (Kindundusi-Mfupi) na Tatu Ali,
hapa sasa muhula wa kwanza ulikuwa unakaribia kumalizika, walifanya mitihani ya
darasa hilo katika masomo matatu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Mitihani
ilipomalizika walimu walisahihisha na kujiandaa kuyasoma matokeo katika Mkutano
wa Baraza la Shule.
Mwalimu Mkuu aliyefahamika kama Mwalimu Sitta ambaye alikuwa
na mkewe mama mmoja mwalimu Mpare aliongoza mkutano huo wa kufunga huku wanafunzi
wote kukusanyika na kukaa chini huku wengine wakiwa wamechuchumaa. Utaratibu ulikuwa
ule ule wa kusoma matokeo ya mwanafunzi wa kwanza hadi mwisho . Ukianzia na
darasa la kwanza ambalo ndilo darasa la mwanakwetu wakati huo.
“Mwanafunzi kwa kwanza kwa darasa la kwanza ni Tatu Ali akipata 100 ya Kusoma, 100 ya Kuhesabu na 100
ya Kuandika, mwanafunzi wa pili ni Mohammed Kindundusi yeye amepata 100 katika
Kuandika, 100 katika hesabu na 95 katika kusoma na jina la kumi ni mwanakwetu amepata
Kusoma katika 0, 100 Kuandika na 100 katika kuhesabu.”
Hapo mwanakwetu alistajabu inakuwaje nimepata sifuri katika
kusoma ambalo ndilo somo jepesi kuliko yote? Akasima na kuanza kulia mbele ya Mkutano
wa Baraza la Shule
“Hapo haiwezekani, alama niliyopewa siyo yangu , mimi kusoma
ninafahamu, inakuwaje niweke sufuri?”
Mkutano mzima wa Baraza la Shule kimya,
Mkuu wa Shule Mwalimu Sitta akaelekeza mwalimu wa darasa la pili azungumze na
mwanafunzi huyu mara moja. Hapo pia wakafika walimu watatu wa kike.
Somo la kusoma nilisoma vizuri maneno
yote sikukosea hata neno moja, mwanakwetu alisema. Mwalimu aliyepewa jukumu
hilo alimuliza je unakumbuka hata neno mojawapo ulilopewa kusoma? Mwanakwetu
alijibu kuwa ni neno JOGOO.
Mwalimu wa darasa la kwanza aliombwa
kuuleta mtihani huo wa kusoma mara moja hapo upenuni na kuingia ofisini huku
Mkutano wa Baraza la Shule unaendelea.Hapo sasa walikuwapo mwalimu wa nidhamu,
mwalimu taaluma, mwalimu wa darasa la pili na mwalimu wa darasa la kwanza. Mwanakwetu
alisoma maneno yote vizuri bila ya kukosea hata neno moja
Matokeo mbele ya walimu hao alikuwa
amepata alama 100 ya kusoma lakini tayari Mkutano wa Baraza la Shule ulikuwa
umemalizika. Mwalimu Mkuu akafika walipo walimu hao akauliza ehee imekuwaje? Kweli
mwanafunzi wetu ameyasoma vizuri nadhani mwalimu mwenzetu alipitiwa kuipachika alama
0 na kusahau kuiweka nambari moja na sufuri ili iwe 100.
“Mwalimu kuwa makini, jitahidi sana usiwe unapanda gari ya dhuruma,
yenyewe uwa inapinduka sehemu ambayo hauitegemei. Mwanafunzi wetu nenda
nyumbani matokeo tumeyasharekebisha.”
Alipotoka nje na hapo mwanakwetu alimkuta rafiki yake Mohamedi
Kindundusi akimgoja na alipokuwa akirudi nyumbani alimsimulia kilichotokea
upenuni na ofisini.
Kumba kuliko yote ni kuyakumbuka mno maneno ya Mwalimu Mkuu
Sitta,
“Mwalimu kuwa makini, jitahidi sana usiwe unapanda gari ya dhuruma
yenyewe huwa inapinduka sehemu ambayo hauitegemei.”
Mwanakwetu kama unautamani usalama
wako katika maisha ya ulimweguni na akhera ogopa sana kulipanda gari hilo la
dhuruma. Kumbuka haki ni sawa na kulila fenesi mara zote huwa linapandwa na mtu
mmoja lakini huliwa na wengi ukitaka kula mwenyewe lazima litakushinda tu maana
fenesi ni tunda la wakarimu .
Mwanakwetu upo?
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment