ITAZAME TANZANIA KIHALMASHAURI

 



 Adeladius Makwega-MWANZA

Aprili 25, 2022 jioni Mwanakwetu aliongea kwenye simu na rafiki yake mmoja ambaye aliwahi kufanya kazi katika Halmashauri Misenyi, hivi sasa ndugu huyu ni mfanyabiashara. Ndugu huyu sasa kibindoni anao uzoefu wa utumishi wa umma na ufanyaji wa biasahra binafsi.

Ndugu huyu anasema kuwa watu walio wengi huwa wanatazama mambo na kuyaona katika mtazamo wa kimjini mjini tu kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Tanga na Mbeya ambapo hali ya maisha ya majiji siyo hali ilivyo katika maeneo mengine ya Tanzania ya vijijini.

Ndugu huyu anasema kuwa ukitaka kuifahamu Tanzania jaribu kufanya kazi katika halmashauri, bila hiana anasema kuwa hata neno lenyewe HALMASHAURI lina shida, kwani linatokana na neno la kiarabu AL-MASHAUR yaani ni eneo ambalo kuna mambo mengi.

Ndugu huyu akiwa Misenyi anasema anakumbuka mambo makubwa mawili ambayo hakuwahi kuyaona maishani mwake.

 

“Siku moja nilidamka kwenda kazini, nikiwa katika majukumu hayo nilipita hospitalini, nikiwa hapo niliona maiti inatolewa hospitalin, ikawekwa katika baiskeli, ikawa imekalishwa, ikawekewa ubao, huku nikiona kama mtu aliye hai amekaa katika kitako cha nyuma cha baiskeli hiyo kwa nyuma,ikafunga mikanda ya mpira na kufunikwa  khanga, jamaa akapiga pedeli na kuondoka na mwili huo.”

Ndugu huyu lilimshangaza mno tukio hilo , akilinganisha na maisha yake aliyotokea yaani Arusha Mjini anasema alitumia mwezi mmoja na ushehe hadi taswira hii ya kubeba maiti kwa namna hiyo kuondoka kichwani mwake. Tukio ili lilisababishwa ashikwe na bumbuwazi kubwa, akisema anaota au anaona tukio la kweli? Mwanakwetu hilo lilikuwa tukio la kweli.

Hivyo ndiyo ilivyokuwa, kweli maiti ndani ya baiskeli kwenda nyumba, alafu kuzikwa. Maisha yake ya Misenyi yaliendelea Mungu akamuonesha tukio lingine la pili akiwa katika shughuli zake vijijini kama mtumishi,

 

“Kuna siku nilikutana na watu wawili wanaotoka katika kata moja inaitwa Ruzinga walikuwa wanatembea kwa miguu wanakwenda katika zahanati liyopo katika kata nyingine inayofahamika kama Bugorora huko huko Misenyi. Huku tukiwa tumepanda bodaboda na mwezangu na kati kati ya kata hizo mbili za Ruzinga na Bugorora palikuwa msitu mkali. Tukiwa na bodaboda hiyo kwa mbali tukawaoma watu hao kwa mbali kama wamebeba kitu, tulipowasogelea tukaona kochi la mbao, kocho la watu wawili (love seat) mmoja akabeba mbele na mwingine kabeba nyuma wanakwenda kidogo kidogo.Tulipotazama tukasema hawa jamaa wanahamisha kochi lao, kumbe walikuwa wamebeba mgonjwa, mahututi mno wanakwenda zahanati ya jirani.Hapo walimfunga mgonjwa wao kama nilivyosema wakitoka Ruzinga kwenda Bugurora kwa miguu.”

 

Msomaji wangu kwa mujibu wa google map umbali kutoka Ruzinga hadi Bugurora ni Kilometa 42.7 kwa miguu unatumia kati ya saa 8-9 na kwa gari ni kati dakika 55-70. Haya ni maelezo ya Mwanakwetu kwa mwaka 2022 msomaji wangu.

Kwa mujibu wa ndugu huyu alikuwa anaifahamua hiyo zahanati waliyokuwa wanakwenda,

 

“Hata hiyo zahanati ilikuwa na muhudumu wa afya (medical attendant) mmoja tu.”

Ndugu huyu alisema cha kusikitisha hapo katika zahanati huyo muhudumu wa afya ndiye alikuwa anayefanya kile kitu. Ndugu anasimulia kuwa walifunga kochi hilo katika pikipiki yao na huyu dereva wa bodaboda alitangulia nae mgonjwa hadi hapo zahanati na baadaye aliwafuata yeye na ndugu wa mngojwa na kuwaacha zahanati na yeye na boda boda kuondoka zao.

Ndugu yake huyu Mwanakwetu alimalizia kumsimulia kwa kusema kuwa ukitaka kuielewa nchi hii usitazame Ki Dar es Salaam, Ki Mwanza, Ki Mbeya, Ki Tanga, au Ki Arusha, anasisitiza kuwa itazame Tanzania Ki-Halmashauri kuna mengi ya kutisha na ya kusikitisha.



 Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Inawezekana wananchi wa eneo hilo sasa wanapata hudumu za afya, pengine huduma zipo jirani, pengine mhudumu wa afya ameongezewa nguvu-Mwanakwetu anasisitiza neno labda katika hilo, maana ni vizuri kutamka maneno mema alafu hayo mema yakaja kweli.

Watanzania walipo vijijini ni ndugu zako wewe unayesoma matini haya, ndugu zake mwandishi wa matini haya na ndugu zetu sote mimi , wewe na yule, la msingi popote ulipo watazame sana Watanzania walipo vijijini na itazame Tanzania Kihalimashauri.

 makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

0/Post a Comment/Comments