SHANGA ZA KATAMBUGA

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Aprili 30, 2023 Mwanakwetu alipokuwa Kanisani misa ikikaribia kumalizika umeme ulikatika, kanisani kukawa giza, lakini mshumaa wa pasaka na mishuma miwili ya altare iliokoa jahazi, Padri alitoa baraka ya mwisho na waamini wote kutoka kanisani kurudi majumbani mwao.

Hapo Mwanakwetu alishindwa kufanya kazi zake katika kompyuta yake, hivyo aliamua kwenda katika soko la Malya kuhemea. Akilini mwa Mwanakwetu akiwa njiani sokoni alisema,

“Eneo hili umeme unakatika sana.”

Alipofika sokoni aliona kuwa siku hii ilikuwa kuna gulio, huku vitu kadhaa vikiuzwa, Mwamakwetu alivutiwa mno kununua makatambuga ambayo yanatengenezwa kwa kutumia matairi ya gari, misumari na shanga.

Alipouliza bei kijana muuzaji alisema yanauzwa kati ya shilingi 2000/=-4000/=, Mwanakwetu alitoa shilingi 2000/= hapo hapo lakini muuzaji alikataa fedha hiyo kwa kuwa ilikuwa imeungwa.

“Kaka nikipokea pesa hii nitagombana na bosi wangu na atanikata katika malipo yangu ya siku ya leo jioni, nakuomba kama una pesa nyingine nilipe .”

Mwanakwetu alitoa pesa nyingine na kurudishiwa chenji yake, alichagua makatambuga hayo alafu akaanza kuondoka. Kijana muuzaji ambaye aliongea Kiswahili chenye sarufi nzuri lakini chenye matamshi ya Kisukuma alimuita na kusema haya,

“Wewe ni mgeni wa Malya na mgeni wa makatambuga. Ukinunua haya unawajibu wa mimi kukurekebishia, ona hii misumari imesimama, ukivaa itakuumiza bure.”

Msomaji wangu kijana huyu alifanya hivyo vizuri sana na kuvikabidhi viatu kwa Mwanakwetu. Mwanakwetu alimuuza kijana huyu je kwa siku anauza katambuga ngapi? Kijana alijibu kuwa inategemea na hali ya soko lakini ni kati ya 10-20 na ana jozi 500 ndani ya mifuko miwili.




Mwanakwetu alimuuliza maswali mengine: ; Je ameanza kazi hiyo lini? Na analipwa kiasi gani kwa siku?

“Ninalipwa shlingi 10,000/= huku shilingi 6000/= ni yangu, 1000 ni ya chakula cha mchana na huku 2500/= ni ya kupakia katika lori kwenda na kurudi gulioni. Kazi hio nimeanza baada ya kumaliza mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, maana sasa nangoja kwenda kidato cha tano na nimefanya vizuri .”

Mazungumzo hayo na kijana huyo alisema bayana kuwa amesoma shule ya kanisa, amepata daraja la kwanza na atasoma kidato cha cha tano Fizikia, Kemia na Hesabu. Mwanakwetu akaagana naye na kwenda zake.

Mwanakwetu akiwa anarudi njiani alikutana na mama mmoja mtu mzima sana, akacheka mno kwa Mwanakwetu kununua makambuga aliyokuwa ameyashika mkononi, alafu akamuuliza sasa mbona hawajakupa mfuko wa kuwekea? Pole, sasa umekuwa msukuma. Mama huyu mwenye mvi akavichukua viatu vya Mwanakwetu alafu akasema unaona viatu hivyo vimevishwa shanga tatu? Mwanakwetu akajibu ndiyo, akaulizwa je unaelewa maana yake? Mwanakwetu akacheka, alafu akasema sielewi.

“Sasa lazima uwe Msukuma, Shanga tatu maana yake viatu hivyo vinavaliwa na watu watatu; Baba, Mama na mtu mwingine, huyo mwingine akilini kichwani mwako. maana hivi ni viatu vya kuogea.”

Mwanakwetu alicheka sana, alafu akamuuliza jina lake bibi huyu ambaye kwa umri kwa mtazama ni kati ya miaka 70-80 akataja jina lake alafu akisema yeye ni mwalimu mstaafu.

Mwanakwetu aliagana nae mama huyu na kuelekea nyumbani kwake, hata alipofika kwake umeme ulikuwa bado haujarudi hadi saa nane ya mchana ndipo ulirejea. Umeme uliporudi akaamua kuandika hekima hii ya shanga za katambuga na mgeni wa katambuga.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments