HAZIWEZI KUDUMU PAMOJA



Lucas Masunzu- MAKOLE

 MAMIA ya miaka iliyopita katika nchi ya wataliano kulikuwa na wapenzi wawili ambao dunia inawakumbuka hadi kesho. Wapenzi hao walikuwa wanatoka katika familia mbili Montagu na Capulet familia ambazo zilikuwa na nguvu kubwa na utajiri mkubwa sana huko Verona, Italia pamoja na utajiri huo familia hizo zilikuwa na uadui mkubwa usioweza kusuluhishwa huku sababu ya uadui huo ikibaki bila kujulikana. Kwenye familia ya Montague alikuwapo kijana Romeo na kule kwenye familia ya Capulate alikuwepo Juliet ambaye alikuwa ni binti mrembo mno. Kipindi uadui wa familia hizi ukichipua na kuendelea kukua taratibu, Romeo hakuwahi kukutana na Juliet wala kuonekana akiwa mstari wa mbele akibeba silaha katika vita vilivyosababishwa na uadui huo isipokuwa alikuwa mtari wa mbele akikaza nati za penzi lake na Rozaline binti aliyekuwa anampenda mno! Wakati huo Juliet alikuwa na umri mdogo wa miaka 13 lakini alikuwapo Count Paris kijana tajiri mkubwa alifanya juhudi ya kumtafuta babaye Juliet akarusha ndoano ya posa majibu aliambiwa kama nia hiyo ipo avumilie binti akue, umri ukamfanya aonge mwamba lakini bado ubembelezi usiofika nchani uliendelea maana alimpenda mno binti huyo tangu akiwa bado mdogo zaidi.

 

Kuna siku familia ya Capulate ilifanya sherehe kubwa Rozaline msichana aliyekuwa anamvutia sana Romeo alipata mwaliko naye Romeo akaweka nia ya kuhudhuria licha ya uhasama mkubwa endelevu uliopo, aliamini mkusanyiko wa watu wengi utamfanya asionekane lakini nia ya Benvolio ambaye ni mjomba wa Romeo ilikuwa ni kumkutanisha Romeo na wasichana wengi zaidi ambao lazima angewapenda zaidi kuzidi hata Rozaline ambaye tayari alikuwa himaya yake. Romeo na nduguze wa ukoo wa Montagu wataingiaje kwenye sherehe iliyoandaliwa na maadui zao wa muda mrefu? Wakaamua kuvaa masks ili sura zisionekane jambo hilo likatimu vizuri hatimaye wakatinga kwenye sherehe hiyo. Romeo aliwazidi mvuto wanaume wote kwenye sherehe, mavazi yake yalimkaa vyema na hapo ndipo kwa mara ya kwanza akaonana na binti mrembo Juliet, hakupoteza dakika hata moja kwa haraka aliunda tabasamu zuri usoni mwake kuashiria anatangaza amani, upole na urafiki kwa mrembo huyo huku moyoni mwake akitambua bayana kuwa tayari tone la uongo  limedondoka kwenye mapenzi yake na Rosaline  maana ni kwa Juliet tu ndipo sasa aliona uzuri wa kweli na siyo kwa Rosaline tena kama ilivyokuwa hapo awali.

 

Akiwa kwenye sherehe ghafla wasiwasi ulimjia Romeo akahisi kuna kitu kibaya kitatokea ambacho kukirekebisha ni vigumu tena kitachukua uhai wake. Lazima ni lazima tu, moyo wa Romeo ukaendelea kumpenda zaidi Juliet uadui wa familia zao hauathiri kabisa hisia hizi za bidii. Tybalt binamu yake Juliet aliyekuwapo kwenye hiyo sherehe akagundua kuna watu kutoka familia ya maadui zao wamezamia. Tybalt alikasirika sana hapo hapo adui yao mkubwa akawa ni Romeo akaanza kumshambulia lakini baba yake Juliet alimkataza. Romeo akafukuzwa kwenye hiyo sherehe maisha ya kutangatanga yakampitia akaenda kwenye bustani iliyokuwa karibu na nyumba hiyo akajificha, akatafuta namna ya kumouona Julieth kwa mara nyingine. Wakati huo naye Juliet alikwenda chumbani kwake akaanza kujisemesha namna alivyovutiwa na Romeo. Ghafla kichakani gizani akaona akitokea Romeo aliyekuwa amejificha bustanini wakazungumza kwa mara ya kwanza, upendo wao uliendelea kuchipua kwa kasi zaidi uadui wa muda mrefu haukuwa pingamizi kwao, wamekutana leo wakaahidiana kuoana na kesho yake wakafanya ndoa ya siri kwa msaada wa Friar Laurence kiongozi wa kanisa lakini kilichofuata kwao baada ya kuoana ilikua ni mitihani na usiku wa giza lililo nene.

Tybalt akajenga chuki kwa Romeo kwa kosa hilo akamtaka aingie nae ulingoni atakaye muua mwenzake ndiye atakuwa mshindi na mwenye haki. Romeo hakutaka kabisa kupigana japokuwa Tybalt alimung’ang’aniza. Romeo akamsihi nduguye aingie ulingoni lakin badaya aliingia maana kukataa kwake ilikuwa ni kudhalilisha familia yao. Piga nikupige zikaendelea baada ya nduguye alijeruhiwa sana Romeo aliingilia akamshambulia lakini kwa bahati mbaya akamsabishia kifo.




Mtawala wa Verona wakati huo Prince Escalus aliwahi kupiga marufuku mapigano na ikitokea watu wakapigana hukumu yao ni kifo. Kwa kuwa ilikuwa ni bahati mbaya Romeo akahamishiwa jiji la Mantua akapigwa marufuku kukanyaga Verona. Penzi lina nguvu kwa hakika Romeo akawa anarudi kwa siri kuonana na Juliet tena kwa kuhatatarisha uhai wake akawa anaingia hadi chumbani kwa Juliet. Familia ya Kapulate waliendelea kupinga mno mapenzi hayo laana na kutengwa ilikuwa ni kitisho alichopewa Juliet japo kilikuwa butu. Mipango ya kuharakishwa aolewe na Count Paris ikaanza. Juliet akaamua kwenda kumtembelea Baba mtakatifu ambaye ndiye aliyewafungisha ndoa ili kuomba msaada. Ili kukwepa ndoa ya kulazimishwa kuolewa na Count Paris basi ikasukwa njama ya kampa sumu ambayo akiinywa atalala usingizi wa kifo kwa siku mbili kisha Lorenzo atampelekea ujumbe Romeo atakuja kumuiba kwenye jumba wanalotumia kama makaburi, watakwenda mbali kuishi na kufurahia penzi lao. Juliet akanywa ile sumu akalala usingizi lakini kwa bahati mjumbe hakuweza kufikisha taarifa kwa Romeo kuhusu njama hiyo. Romeo akasikia taarifa ya kifo cha Juliet bila kufahamu hata chanzo akarudi kushuhudia. Naye Count Paris akaenda kwenye kaburi la Juliet akiwa anahuzuni tele alipofika akamuona Romeo akadhani ni mwizi hapo hapo ugomvi ukatokea mwamuzi wa ugomvi huo alikuwa ni Count Paris kufa.

Romeo alipomwona Juliet aliamini halika huyu amekufa akaona haipo sababu tena ya yeye kuendelea kuishi akanywa sumu na kufa akiwa amelala kando ya Juliet lakini baada ya siku mbili muda wa Juliet kuamka ukawa umefika akaamka Romeo akiwa amekufa kando yake akiwa na chupa ya sumu. Juliet akataka anywe naye ile sumu kwa bahati ikawa imeisha.

Juliet akasikia watu wanakuja akahisi watamkamata wampeleke kwenye yale maisha ya kulazimishwa kuolewa na Count Paris, kwa haraka akachomoa kisu alichokuwa nacho Romeo akajichoma akafa. Familia mbili zenye uadui zilifika kwenye yale makaburi. Simanzi ikawa imetawala Count Paris, Juliet na Romeo wamekufa! Katika hali hiyo watu wamesimama wasijue la kufanya mithili ya chura aliyekuwa anasubiri mvua ije kumbe hakuwa na mtungi wa kukingia maji uadui wao ukafika mwisho huku mtumishi wa kanisa Friar Laurence akafafanua mkasa huu, mengi yakazungumzwa, pia akasema kuwa Juliet na Romeo ni wapenzi wenye nyota kali mbili ambazo zikikutana zinakataana kamwe haziwezi kudumu pamoja kwa amani maishani.

Nduguyetu upo?  Tambua siku zote upendo umezungukwa na uadui, upendo huo huo unaweza kuvunja uadui usioweza kusuluhishwa.

Kwa heri.

theheroluke23@gmail.com

0762665595

2023.



0/Post a Comment/Comments