Adeladius Makwega-MWANZA
“Mti huu umekauka,
ndiyo uliokuwa ukitumika kunyongea watumwa waliochoka, kuumwa na baadhi ya watu
walioonyesha kukaidi Serikali ya Kijerumani hata ile ya Waingereza baadaye.
Madhira haya ni yale ya enzi za biashara ya utumwa na wakati wa utawala wa
wakoloni, wale wote walioupinga walikatishwa uhai wao hapo kwa kunyongwa
hadharani. Baadhi ya Waafrika waliokuwa wabunifu katika uhunzi, ushonaji na
ususi walikatwa mikono chini ya mti huu.”
Hayo
yalisimuliwa na mzee mashuhuri wa jiji la Mwanza ambaye jina lake
limehifadhiwa. Pia, maelezo haya yalishadidiwa na Dkt. Mnata Resani Mkurugenzi
Msaidizi Lugha Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ya Tanzania ambaye pia
alipata kusimuliwa hadithi ya mti huu.
“Watumwa
walipofika hapa walikuwa wanapumzika, wale waliochokachoka walinyongwa ili
wasibaki hai au wale waliokuwa wakisingizia ugonjwa. Hiyo ilikuwa adhabu
madhubuti ili kila mtumwa ajitahidi awezavyo awe mzima hadi mwisho wa safari.”
Bila
hiyana mzee huyu aliyevalia koti la Kaunda lililochujuka ambaye alionekana kuwa
mtulivu sana, muelewa mno, kama aliwahi kuwa mtumishi wa umma ujanani vile,
aliendelea kusema;
“Siyo kisiki
halisi, bali ni kisiki bandia ambacho kilitenengezwa na kampuni moja kama
kumbukumbu ya mti huo uliokuwa ukitumika kunyongea enzi za utumwa, enzi za
wakoloni.”
Mzee huyu alituvuta kando ya kisiki
bandia hicho kama hatua nne za mtu mzima akatuonyesha mti ambao ulikuwa
unachipuka akisema kuwa mti halisi ulikuwa MKUYU huu hapa sasa umeanza kuchipua
majani yake baada ya ule mti mkongwe kuanguka na kuondolewa. Aliendelea kusema;
“Tunachoshangaa
kwa sasa mti huu umeanza kuchipua kidogo kidogo, kuna wakati uliota lakini
ukakatwa na watu kimakosa lakini unachipua tena kupitia mizizi ya mti huo wa
asili.”
Hata
waliojenga hiki kisiki bandia walidhania mti huu umekufa, walifanya hisani
kulinda kumbukumbu ya historia hiyo lakini la kustajabisha mti huo unachipua
kwa kasi.Baada ya maelezo haya Dkt. Julieth Kabyemela ambaye ni Mkurugenzi
Msaidizi anayeshugulikia Urithi wa Utamaduni na Maadili ya Taifa na Lilian
Firimin Shayo Afisa Utamaduni Mwandamizi wote wa Wizara ya Utamaduni , Sanaa na
Michezo na walipiga picha na mti huo kuhifadhi kumbukumbu yake ambapo sasa
unachipuka kwa kasi mno ukiwa na urefu unaokaribia sentimeta 30.
Nilipotoka hapo binafsi nilitafakari mambo mengi juu ya mti huo; kwanza mti huo namna ulivyokuwa ukinyonga watumwa waliokuwa wamedhoofu kihali na kiafya safarini, halafu mti huo huo ulitumika kunyonga watu waliotazamwa kama wakorofi wakati wa utawala wa wakoloni, na wale wabunifu na wadadisi ili kurudisha na kudumaza tekinolojia ya Mwafrika. Tafakari yangu kubwa zaidi na ya msingi ipo katika dhana ya kuwekwa kwa kisiki bandia cha mti huo, sasa mti huo ulioanguka, unachipuka, kuonyesha falsafa za wazee wetu kuwa, Historia huwa haizikwi.”
“Katika dunia
ukifanya baya au zuri usidhani yamepotea yatarudi tu bila ya wewe kufahamu,
ukiwa hai au hata kwa kizazi chako. Ule wema /ubaya utajidhihirisha wenyewe
kama mti huu wa kunyongea sasa unapochipuka tena na kile kisiki bandia
kinapokosa kazi.”
Mwanakwetu anaiweka kalamu yangu chini nikiwa hapa Igoma Mwanza kwa kusema kuwa kumbuka kuchagua ya kutenda yawe mema au mabaya yote ni mbegu. Unapoona katika familia zetu za Kiafrika tunatoa majina kwa watoto wetu kutokana na majina ya wahenga wetu wa awali, hii ni njia ya kuhifandhi historia za wazee wenye majina husika. Mti huu umeitikia tabia za binadamu.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment