MISAMAHA INA MSINGI MKUBWA

 


Adeladius Makwega-MARA

Mei 26, 2023 Mwanakwetu yu umbali mchache na kaburi la Mwalimu Julius Nyerere aliyeliongoza Taifa la Tanzania kwa miaka 23 akiwa ni Rais wa Kwanza wa Tanganyika huru na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazingira ya eneo hilo ni kijani kibichi, huku watu wote wanaofika hapo wakikaribishwa kwa heshima zote na wahudumu wa eneo hilo vijana ambalo kwa kuwatazama hata wao kama walimuona Mwalimu Nyerere basi kwa kipindi kifupi tu  tena cha utoto wao tu.

“Mwalimu Julius  Nyerere Mei 2, 1955 alikwenda Umoja wa Mataifa katika hizo harakati za kuudai Uhuru wa Tanganyika,  akiwa huko Marekami  alitoa  hotuba iliyowasilishwa na ikawa mwiba na iliwakera mno wakoloni Waingereza ambao ndiyo walikuwa watawala wa Tanganyika. Mei 21, 1955 Mwalimu Nyerere aliwasili Tanganyika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na aliposhuka tu alipokonywa kibali chake cha kusafiria na Serikali ya Kikoloni. Alitoka hapo uwanjani kuelekea  kazini kwake  Pugu Sekondari, alipofika huku alikutana na mwiba mwingine wa mkoloni, akaitwa na Mkuu wa  Shule ya Pugu akaambiwa achague moja kama kufanya siasa au kuendelea na kazi ya kufundisha. Mwalimu akiwa mbele ya Mkuu wa Shule mzungu hakujibu kitu, alikaa kimya huku akilini mwake akiwa na jibu la swali hilo la mkuu wake wa kazi na wakala wa Kikoloni. Siku iliyofuata yaani Mei 22, 1955 aliandika barua ya kuacha kazi na baadaye kurudi kijijini kwao hapa Butiama yeye na familia yake, akawa anafanya kazi ya kujitolea kwa Wamisionari hapo hapo kijijini.”

Hayo yanaendelea kusimuliwa huku Mwanakwetu kama baba, kama mzazi na kundi la watu kadhaa ambao walikuwa wakimsikiliza msimuliaji huyo ambaye alitumia lugha ya kueleweka, kwa upole mkubwa mithili ya mtawa wa Kanisa Katoliki aliyeopo katika mimbari ya kanisa siku ya dominika maelezo yake yakisikitisha mno.

Eneo hilo yanaposimuliwa maelezo hayo lilionekana miti kadhaa ya asili ambayo ilivumisha upepo mzuri sana na kuipamba ardhi hiyo na majani yaliyokuwa mapana  sana yaliyokuwa yanaanguka kila sekunde kutoka mitini. sauti ya upepo wa miti hiyo ilisindikizwa na sauti za ndege pili ya ndege Tausi waliokuwa wakilia katika makazi hayo.

“Kumbe nao Tausi wanasauti mbaya hivyo?”



Alisema mtu mmoja kando ya Mwanakwetu, kumbuka msimuliaji yu mbele  huku akiwa amevalia fulani nyeupe na suruali iliyopigwa pasi vizuri, viatu vyeusi akiendelea kusimulia kwa uhodari mkubwa.

 

“Kazi kubwa aliyokuwa akiifanya Mwaiimu Nyerere kwa Wamisionari hapa Butiama ilikuwa ni kuwafundisha Kizanaki na Kikwaya Lugha za asiili za eneo hilo na wakati mwingine alikuwa akifanya tafsiri ya masomo ya  misa  ya siku iliyofuata ya Kanisa Katoliki kutoka Kilatini kwenda Kizanaki au Kikwaya, yaweze kueleweka kwa Wakristo wa eneo hilo.”

Msomaji wa Mwanakwetu kumbuka sasa Mwalimu Nyerere hana kazi kibarua kimepotea yu nyumbani kwao Butiama, msimuliaji anasimulia huku kila mmoja kimya kana kwamba amemwagiwa maji ya baridi japokuwa jua kali linawaka hapa Butiama, mkoani Mara.

“Agosti  1955  Oscar Kambona alitumwa na  wanasiasa wenzake wa TANU kumfuata Mwalimu Nyerere  Butiama maana  wenzake walikuwa hawamsikii tena ndugu yao  ambaye tayari alikuwa hana kazi na amepoteza kibarua kutokana na harakati za  siasa za Tanganyika. Kambona alipofika kwa Mwalimu Nyerere alikabidhi nauli ya Mwalimu Nyerere iliyotolewa na wenzake ili arudi Dar es Salaam kuendelea na siasa, alipopewa pesa hiyo ya nauli na Kambona, Mwalimu alichukua pesa hiyo akampa nduguye aliyefahamika kama Joseph Nyerere akimwabia anunue Ng’ombe. Joseph Nyerere alinunua ng’ombe huyo na kumpeleka kwa Julius Nyerere. Maswali yakiwa je ng’ombe hiyo ni ya kufunga kwa kuwa sasa Mwalimu Nyerere hana kazi au kunasherehe ya ugeni wa mwanasiasa Oscar Kambona? Mwalimu Nyerere alitoa maagizo kuwa achijwe, akaliwa na siku zikawa zinasonga naye Oscar Kambona hafahamu kinachoendelea, je lini wanarudi na Mwalimu Nyerere Dar es Salaam kuendelea na siasa? Oscar Kambona alikaa hapo akachoka, akaamua kwenda Kigoma, Bukoba na Mwanza na baadaye kupanda treni kurudi Dar es Salaam.”

Msimuliaji huyu aliendelea kusimulia kila mmoja akitega sikio,

“Mwaka 1957 Mwalimu Nyerere alipewa  Ubunge kwa  kuteuliwa na Gavana, hapo ndipo akarudi katika siasa kwa nguvu zote akiteuliwa kuiwakilisha Morogoro, Japokuwa hakukuwa  kwao.”

.

 

Kumbuka msomaji wangu hayo yanasimuliwa na mtumishi katika  Makumbusho ya Mwalimu Nyerere hapa  Butiama, akili na masikio ya Mwanakwetu yakimsikiliza kwa umakini mkubwa kwa sababu nyingi, mojawapo  ni kutokana na kutajwa mno kwa  mwanasiasa Oscar Kambona ambaye walitafautiana sana mwishoni wa miaka ya 1960 naye Kambona na kwenda Uingereza.

Swali ambao liliibuka  ni juu ya mahusiano ya Mwalimu  Nyerere kabla ya uhuru na miaka  ile ya awali  hadi  kukaribia  Azimio la Arusha na Kambona yalikuwa ya kidugu, kirafiki , kijamaa mno na ya kuaminiana.

Mahusiano hayo yaliingia shubiri na kuwa mabaya, je  kuna ushahidi wowote ule wa kiserikali au wa kifamilia juu ya Mwalimu Nyerere ambaye sasani Mwenyeheri ambayo ni hadhi kubwa  kwa Kanisa Katoliki kama aliwahi kukutana, kumpigia simu nduguye Oscar Kambona  kusameheana tangu tafauti hizo kutokea hadi kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka 1999?

“Mwalimu Nyerere na Oscar Kambona kwa ukweli kabisa walikuwa na utafauti wa kimitazamo ya kisiasa tu baina yao, ikikumbukwa kuwa Kambona ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa TANU kama waliwahi kukaa pamoja na kuzungumza baada ya kupishana huku hilo halifahamiki.”

Majibu hayo yalitolewa.

Siku ya leo Mwanakweu anasema nini?

Mwanakwetu anaamini kuwa kama kulikuwa na utafauti wa wa kimtazamo hilo si baya lakini utafauti wa kimtazamo je vita, uadui wa viongozi wa milele? Je wanasiasa wetu wa sasa wa Tanzania wanajifunza nini katika kisa hiki ya Mwalimu Nyerere(MKATOLIKI) na Oscar Kambona(PSYAIBATARIAN)?  Pengine wapo Watanzania ambao wanalifahamu zaidi jambo hilo, kubwa utafauti wa kisiasa si uadui wa milele na misamaha ni jambo la msingi.

Mwanakwetu upo? Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

0/Post a Comment/Comments