Adeladius Makwega-MWANZA
Mei 25, 2023 Mwanakwetu alipigiwa simu ya rafiki yake mmoja anayeitwa
Ustadh Kuandika kutoka Lushoto, Mwanakwetu alipoona simu ya Shekhe Kuandika
aliamini kuwa msomi huyu wa dini ya Kiisilamu alikuwa akiuliza kutaka kununua
nyumba moja ya Mwanakwetu ambayo ipo jirani na msikiti wao, ambapo mara nyingi
mawasiliano na shekhe huyu huwa ni ushawishi wake kwa Mwanakwetu kuuza nyumba
hiyo.
Mara zote Mwanakwetu anamwambia Shekhe Kuandika kuwa nyumba
hiyo si yake, bali ni mali ya watoto wake, kama Shekhe Kuandika anaweza
kuwashawishi vijana wa Mwanakwetu wamuuzie, hilo litakuwa kazi kwake.
Shekhe Kuandika mara zote anacheka sana akisema,
“Tunahitaji nyumba ile, ili wageni wa msikiti wetu wakifikie
pale wawe jirani na nyumba yetu ya ibada, siyo kukaa mbali mno, maana tunapata
wageni kutoka mbali mno hadi Arabuni, yaani wageni wa Arabuni tunawaweka nyumba
za wageni zinazokaliwa na kila mtu? Kwa heshima ya msikiti wetu na dini yetu
lazima tuwe na makazi jirani.”
Shekhe Kuandika aliyempigia simu
Mwanakwetu leo hii, awali akisema mengi,
“Umetupa mtihani mzito, hivi Shekhe Makwega jukumu la
kuwakusanya watoto wako wote, alafu tuongee nao, hilo jukumu zito. Tunaweza
kuzungumza na wawili, kumbe wako wanne, siku wakiibuka hao wengine? Hapo itakuwa
kesi, alafu tuonekane siye tumedhulumu? Sisi tunaendelea kuombea dua jambo
hili.”
Kwa hiyo haya mara zote simu hiyo ikipigwa hoja ya shekhe ni
manunuzi ya nyumba hiyo tu lakini simu ya Mei 25, 2023 ilikuja kivingine, huku
ikiwa simu ya kwanza ya Ustadh Kuandika kwa Mwanakwetu.
Msomaji wa Mwanakwetu ni vizuri kuelewa kuwa urafiki wa
Mwanakwetu na Ustadhi Kuandika unatoka mbali kidogo , Shekhe huyu alidhulumiwa
eneo lake biashara na mtu mmoja , kwa hiyo Mwanakwetu alipelekewa hoja hiyo na
suala Ustadhi huyu likakamilika.
Mwanakwetu alikuwa pia anampenda sana Ustadhi Kuandika kwa
hoja nyingine kwa kuwa Wilaya ya Ulanga kuna kina Kuandika Wapogoro iweje
Ustadhi Kuandika awe Msambaa? Utani wa Mwanakwetu kwa Ustadhi Kuandika ulikuwa
ni kwamba pengine Mpogoro wa Mahenge alifika Lushoto na kuoa wamama wa Kisambaa
ndipo Shekhe Kuandika akazaliwa.Hilo likikataliwa kabisa na shekhe huyu.
Shekhe huyu ni mfanyabiashra mkubwa wa bidhaa za dini ya
Kiisilamu kama vile marashi, vitabu vya juzuu, Udi, Korani, tasbii, kanzu ,
kofia nakadhalika, kuna wakati Mwanakwetu aliwapeleka sunna watoto wake,
alipita kwa Ustadhi Kuandika kuwanunulia kanzu za kuvaa kipindi hicho, huku
Shekhe Kuandika akisema,
“Wanao wawe wanavaa kanzu kila siku, siyo siku ya sunna tu.”
Kumbuka msomaji wangu hayo yote ni maelezo ya awali juu ya
Ustadhi Kuandika na ujirani wake na Mwanakwetu, mara zote ukimwona shekhe huyu
huwa amevalia kilemba kikubwa, kanzu maridadi na joho moja kubwa sana lenye
nakshi nyingi.
Je Mei 25, 2023 Mwanakwetu
alipokea simu hiyo ya Ustadhi Kuandika ikiwa na maneno gani?
“Wewe ndugu yangu tunafahamiana miaka mingi, leo nina shida
moja inanisumbua, kuna kijana wangu mmoja, katika maisha yangu ya umasikini
nimewasomesha vijana wangu wengi elimu ya dini na elimu ya dunia vizuri sana,
kijana wangu mmoja niliyemsomesha alipata kazi ya ualimu katika Halmashauri moja
huko Handeni Tanga. Sasa ni mwaka wa nane unakwenda hali yake ya maisha si
ngumu mno. Hivyo nimechunguza nimebaini kuwa Handeni huko ametekwa na mambo ya
kidunia. Nimefika huko na nimeongea na majirani zake akiwamo mkuu wake wa shule.
Nilibaini kuwa anahitaji kuwa karibu na
familia yake ili awe na maendeleo yake na familia . Nimebaini kuwa Handeni siyo
eneo sahihi kwake maana anahitaji kuwa jirani nami kwa uangalizi zaidi, maana
kwa Handeni ametwekwa na maisha ya kidunia huku mama mmoja wa Mzigua Handeni na
mama mmoja Mchaga wa Marangu wamemteka. Shida yangu kukupigia unipe ushauri
nataka kumkomboa mwanangu hivi nafanyaje ahamishiwe Lushoto? Na je nikiwafuta
wakubwa wake watanielewa?”
Mwanakwetu alipomsikiliza nduguye
huyu akamwambia pole kwa hayo yote, akisema kwa kuwa dini yako ya Uisilamu inaruhusu kijana wako
kuwa na mke zaidi ya mmoja kwanini usimuozeshe hao mabinti awe na wake watatu akiwamo
yule Msambaa wa Lushoto, huyu Mchaga na huyu wa Mzigua wa Handeni.
“Ni kweli dini yangu inaruhusu hilo, lakini nimebainia kuwa
kijana wangu bado hana maendeleo binafsi ndani ya miaka hiyo nane ya utumishi
wake na ndiyo maana nataka awe chini ya himaya yangu kwa uangalizi zaidi.”
Mwanakwetu akamwambia hilo suala la
kijana wake kurudi Lushoto linaweza kuwa ngumu maana kijana wake ni mtu mzima
anaweza akagoma kurudi nyumbani hata kama akimuona mwajiri wake, inawezekana
kijana wake akawa na shida lakini je shida hiyo anayoiona kwa kijana wake kama mzazi
je mtoto mwenyewe anaiona kama ni shida?
Mwanakwetu akasema unapotaka
kumkomboa mtu ambaye unadhani yupo katika shida kuna ulazima wa huyo aliye katika
shida anawajibu wa kutambulishwa kuwa yu shidani ili atoe ushirikiano wa kumnusuru
kutoka shidani.
Mwanakwetu simu hiyo ilikatika na
baadaye Ustadhi Kuandika walikubaliana jambo ambalo kubwa lilikuwa nusura kutoka shidani kwa kijana wa ustadhi
huyu.
0717649257
Post a Comment