Adeladius Makwega-MARA
Wanachuo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo
Kwimba mkoani Mwanza, Mei 26, 2023 wametembelea makazi ya Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere yaliyopo Mwitongo Butiama mkoani Mara, wakisali kando ya kaburi
lake na wakizunguka kuona maisha halisi ya kiongozi huyo wa Tanzania
aliyeliongoza taifa hili kwa miaka 23.
Ziara yao hiyo iliyotumia zaidi ya saa sita kuzunguka katika
makazi hayo, kutembelea maeneo mbali, wakipiga picha kupata maelezo kadhaa na
kuuliza maswali na yaliyojibiwa na wasimamizi wa makazi hayo kwa kina.
Akiambatana na wanachuo wake, mkufunzi mwandamizi wa chuo
hiki Denis Kayombo akizungumza kando ya makazi hayo alisema kuwa kwa sehemu
kubwa wakurufunzi wake wamejifunza mengi juu ya maisha ya Mwalimu Nyerere
katika somo la Historia katika ngazi kadhaa za elimu ya Tanzania, hapa Mwitongo
wapo kuuona uhalisia wa maisha ya Mwalimu Nyerere.
“Kubwa ni kuona baadhi ya kumbukumbu zilizohifadhiwa na
kupata uhalisia wa maisha ya kiongozi wetu.”
Wakurufunzi hao walielezwa kuwa Mwalimu Nyerere akiwa anafundisha
Shule ya Sekondari ya Pugu somo mojawapo alilolifundisha ni Elimu ya Viungo na
Michezo (Phisical Education) ambalo linasomwa na wakurufunzi hao kwa sasa. Huku
Mwalimu Nyerere akifundisha somo Viumbe Hai (Biology) na Historia.
“Watu wengi wanashangazwa ilikuwaje Mwalimu Nyerere alifundisha
masomo ambayo ukiyaangalia hayaendani, lakini sisi tunafahamu kuwa Elimu ya
Viungo na Michezo inalingana fika la Elimu ya Viumbe Hai, kama vile misuli na
viungo vya binadamu inavyofanya kazi.”
Alisema Mkufunzi Monika Kalonga ambaye nayeye aliambatana na
wakurufunzi hao.
Wakiwa katika hatua za mwisho za ziara hiyo hapo hapo Butiama
walifika upande wa Makumbusho ya Baba wa Taifa hapo waliona vifaa kadhaa ambayo
vilitumika na Mwalimu Nyerere; mavazi, viatu, majembe, vigoda na zana nyingine
huku redio kubwa yenye uzito wa Kilogramu 20 ikiwavutia wengi.
“Tumeambiwa Mwalimu Nyerere wakati wa ziara zake zote alikuwa
akitembea na redio hiyo ambayo alipewa huko Ujerumani na akitumia kusikiliza taarifa
mbalimbali za kidunia, kumbe Mwlaimu Nyerere alikuwa mpenzi wa kufahamu
ulimwengu unavyokwenda.”
Haya yanasemwa na Tabu Masele ambaye ni mkurufunzi wa chuo
hiki huku akiwa mratibu msaidizi wa ziara hiyo.
Awali kabla ya kuingia ndani ya makumbusho hayo walipiga
picha ya pamoja iliyotanguliwa na maelezo mengi na marefu yakiulizwa na
kujibiwa maswali kadhaa ambapo Tabu Masele aliuliza kama Mwalimu Nyerere
alikuwa na watoto wengine zaidi ya hawa wanaotajwa? Hilo likiwa swali la maisha
binafsi ya kiongozi huyo. Swali hilo lilijibiwa kuwa Mwalimu Nyerere hana
watoto wengine zaidi ya hawa wanaotajwa nah ata yule asaari aliyefariki katika
vita vya Uganda hakuwa mtoto wa Mwlaimu Nyerere bali alizaliwa katika kijiji
jirani na Mwitongo, huku maswali kadhaa yakiulizwa ambayo yaliibua maelezo
haya,
“Mwalimu Nyerere akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tabora
alipewa mke na familia yao ambaye hakumuoa wala kuishi naye , huku akimtunza kwa
kipindi chote cha uhai wake, mwanamke pekee aliyemuoa na kuishi naye ni Mama
Maria Nyerere.”
Majibu hayo yaliibua maswali ya namna maisha ya Mwalimu Nyerere alivyoweza kumtunza mama huyu ambaye ilielezwa yu hai hadi leo. Huku mjadala huo ukinoga mno kwa Wakurufunzi hao wakiwa ndani ya basi wakisema kuwa kwao Mwalimu Nyerere ni babu, kwa hiyo lazima kufahamu maisha binafsi ya babu yao na kiongozi wao wa zamani.
Post a Comment