Adeladius Makwega-MWANZA
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya
Michezo Malya, ndugu Richard Mganga amesema kuwa maendeleo ya chuo anachokiongoza yanakwenda kwa kasi huku
miradi kadhaa ya maendeleo ikielekezwa na serikali kwa miaka kadhaa mfululizo
chuoni hapa.
Hayo yamesemwa Mei 31, 2023
katika kikao cha kawaida na wakurufunzi
wanaosoma chuoni hapa katika kozi
mbalimbali za michezo Uwanja wa Ndani
uliyopo Malya Kwimba mkoani Mwanza.
“Kuna wakati tulikuwa tunapokea
wanachuo 40 tu, kwa kozi mbalimbali lakini kwa sasa tuna makundi ya mamia, wakati
huo tulikuwa tukipokea hao arobaini, tulikuwa hatupokei tena hadi wanachuo hao
wahitimu ndipo tuanze tena kudahili upya, sasa umati huu ni ushahidi kuwa
udahili umeongezeka. Shabaha yetu ni kuongeza udahili wetu na ndiyo maana
kumekuwa na uboreshaji wa mabweni na majengo mengine hatua kwa hatua, mfululizo.”
Akiendelea kuongea katika kikao
hicho huku makofi yakitawala aliwaomba wanachuo hao kutilia maanani mafunzo yao,
akibainisha namna serikali inavyofuatilia chuo hiki kwa ukaribu mkubwa.
“Nawaambieni kuwa tunatarajia ujio
wa Mwenge wa uhuru ambao utaweka jiwe la msingi
katika mradi wa ghorofa tatu wa bweni, huku viongozi wa Kiserikali wanatarajiwa
kufika kuona maendeleo ya chuo chetu.”
Wakizungumza mara baada ya Mkuu
wa Chuo Mganga kuongea, wanachuo hao kwa pamoja wamepongeza serikali kwa
maboresho hayo huku wakiomba juhudi zaidi katika kuinua michezo hapa nchini
hususani katika ujenzi wa miundo mbinu ya viwanja kadhaa nchi nzima.
“Kwa hakika tunapata mafunzo mazuri
lakini hali ya miundo mbinu mashuleni si nzuri, hilo linahitaji maboresho
makubwa ili jamii ya Watanzania waweze kushiriki michezo kikamilifu.Matarajio
yetu sisi tukihitimu hapa tunalo jukumu pia la kwenda kuboresha miundo mbinu hiyo kupitia
wadau.”
Hayo yalisemwa na Baptist Kapinga
ambaye ndiye Mwenyekiti wa Serikali na Rais wa Wanachuo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa
wanachuo hao kuzungumza na Mwadili wao mkufunzi
Epifania Mugaga kwa faragha
Post a Comment