UCHOYO WA MBUGANI

 


(Profesa Melubo Kokel aliyeweka mkono tumboni akiwa na rafiki zake) 

Adeladius Makwega-MWANZA

Mei 27, 2023 Mwanakwetu alikuwa akisafiri kutoka kwake kuelekea Hifadhi ya Serengeti ambapo haukuwa umbali mrefu sana, akiwa na kundi la watu wanaokaribia 50, katika safari hiyo ndugu mmoja ambaye alijitambulisha kuwa yeye ni mzaliwa wa eneo hilo, wazazi wake wakitoka mikoa mingine ya Tanzania na kwenda kufanya kazi huko, ndugu huyu anadai kuwa alisoma na kupata kazi ya ualimu kando kando ya Serengeti yenye wanyama wengi, akijinasibu kuwa anahifahamu vizuri Hifadhi ya Serengeti

Mwalimu huyu alikuwa mtu muhimu sana safarini humo kwa kutoa maelezo ya kina, kulingana na uzoefu wa maisha yake ndani ya hifadhi hiyo kwa miaka mingi. Kumbuka kwa pamoja wapo ndani ya basi, huku mwongozaji wa watalii akiwa msomi aliyesomea mambo hayo akitoa maelezo ya kina na katika utalii ndani ya hifadhi ya Serengeti.

Mwanakwetu na wenzake wakiipata elimu hiyo kwa kina, safari inaendelea huku dereva akikata mbuga ambayo ilikuwa na miti michache mikubwa na vichaka vifupi vifupi.

Walifika sehemu mojawapo palikuwa na kijiji kiichochangamka mno, basi hilo likasimama na mwongozaji watalii akiwajulisha kuwa kama wanataka kunywa chai basi wanywe hapo maana bei yake ni nafuu, akiwakumbusha kununua maji, soda na vitafunwa vingine.

“Jamani kuleni mshibe, wala msiwe na haraka, huko mbugani bei ya kila kitu ni juu, kwa hiyo kama mnanunua maji, soda na mikate chukueni haraka.”

Mwalimu mzaliwa wa Serengeti akirudia tena maneno yaliyosemwa na mwongozaji watalii, hapo walipo bei ya chai ilikuwa nafuu mno, huku supu ya nyama ya ng’ombe ikiuzwa shilingi 2000/= bei ya vinywaji kama soda na maji ilikuwa ni ile ile ya maeneo mengine. Kwa hakika Mwanakwetu alikunywa supu tamu na nzuri katika kijiji hiki ambayo hajakunywa kwa miaka mingi, akisema wazi kuwa supu hiyo katika jiji la Dodoma ingeweza kuuzwa hata kati ya shilingi 7,000-15,000.



Watalii makabwela walipomaliza kunywa chai hiyo nzito waliingia ndani ya basi na kuanza kuitafuta hifadhi hiyo. Wakiwa njiani Mwanakwetu ambaye nayeye ni mtalii kabwela alimkumbuka msomi mmoja wa masuala ya haya wa Tanzania, ambaye mpaka sasa anakaribia kufikisha miaka 30 akihudumu katika nyanja hii hii ya utalii katika kona mbalimbali za taifa letu, nayeye ni Profesa Melubo Kokel.

Gari lao huku likikata mbuga, Mwanakwetu alikumbuka mwaka 2005 Profesa Kokel alikuwa miongoni mwa wasomi ya masuala ya haya walioshiriki kuanzisha na kusomesha kozi ya shahada ya kwanza ya utalii katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa akishirikiana na Profesa Mshana. Huku wakati huo jambo mojawapo ambalo lilisitizwa mno na Profesa Kokel ni ujuzi wa kila Mtanzania kujitahidi kuwa mshawishi kwa Mtanzania mwenzake kufanya utalii wa ndani na siyo kungoja tu watalii kutoka ng’ambo. Watanzania wengi wanaweza kutembelea vivutio vyao vya utalii kama huduma katika vivutio hivyo kuwa rafiki kwa watalii wazalendo na kupewa hadhi sawa kama watalii wageni, akilini mwa Mwanakwetu anamkumbuka Profesa Kokel akimueleza maelezo hayo ofisini kake huku Mwanakwetu akiyanukuu katika shajara yake.Kumbuka Mwanakwetu yu ndani ya basi wanakwenda katika hifadhi .

“Kwanini tusinywe chai ndani ya hifadhi hiyo? Tuwe tumekaa katika viti vizuri, huku kila mwenye simu yake akijipiga picha ya kuwalingishia wenzake baadaye katika mitandao ya kijamii. Sasa tumekunywa chai na supu nzuri nje ya hifadhi tunahofia gharama.”


(Mbunge wa Malinyi mhe.Antipas Mngungusi)

Mwanakwetu alijisemea moyoni.

Urafiki wa Melubo Kokel na Mwanakwetu kwa pamoja waliweza kuandika makala nyingi za utalii hapa Tanzania, huku wakijiuliza namna ya ushiriki kwa Watanzania wengi katika kutembelea mbuga na vivutio hivyo , Mwanakwetu alimkumbuka mwanachuo mmojawapo Profesa Kolel ambaye alisomeshwa masuala haya ya utalii ni Antipas Mngungusi aliwahi kuwa mtumishi wa TANAPA sasa ni mbunge wa CCM Jimbo la Malinyi.

Hivi sasa ni miaka karibu 20 ya makala hayo lakini bado watalii makabwela wanahofia hifadhi zetu kwa gharama za huduma zake na Mwanakwetu akiwa miongoni mwao. Safari iliendelea na kufika ndani ya hifadhi hiyo, Mwanakwetu akiwa mnyonge, hata katika baadhi ya vituo wahudumu wa mbuga hii hawakuwapokea vizuri, wala hawakuhangaika na watali wazawa. Vijana wa hifadhi waliowapokea vizuri ni wale wa Uwanja wa Ndege wa Mbugani Soronera na pale kwenye Media Center tu na hata hapa kwenye media Center ni yule mtoa maelezo tu, huku kundi la watu 50 lilikuwa kubwa lakini kijana huyu alijituma vizuri . Wengine waliendelea kufanya mawasiliano yao ya simu na kufanya kazi zingine.

Watalii makabwela wengi hawakuweza kununua chochote kile isipokuwa mama mmoja ambaye aliuliza bei ya soda akiambiwa ni shilingi 2000, naye Mwanakwetu akiwa mzee wa dare for more alipouliza aliambiwa kuwa soda za kampuni hiyo hawana , hata alipouliza vituo karibu vitatu, Mwanakwetu hakupata soda za dare for more akisema moyoni kuwa,

“Siku nyingine nikijaliwa kutali kwa ngekewa kama safari hii nitanunua ile chupa kubwa kubwa ya dare for more, naiweka katika jokofu langu inaganda hadi iwe barafu alafu naingia nayo katika hifadhi huku nakunywa, maana mbugani hazipatikani.”

Kumbuka watalii makabwela wanaendelea na utalii wao huku wakiwaona wanyama wengi, msomaji wangu kumbuka mbugani hakuna uchoyo wa kuwaona wanyama, uchoyo uliopo ni pa kulala na kula tu, kuona wanyama ni nguvu ya macho yako.


Wenzake na Mwanakwetu wakawa wanamcheka wakisema sasa ndugu yetu wewe umetupiga picha nyingi, kwa tunavyoona inawezekana sasa tunakaribia kumaliza utalii wetu wewe utakosa picha hata moja hivyo ngoja na wewe tukupige picha. Kweli Mwanakwetu katika picha 1000 alizopiga yeye alikuwemo katika picha tatu tu ambazo zilipigwa katika eneo linafahamika kama Saronera huku chaji ya betri ya kamera yake iliisha.

Saronera palikuwa pamechangamka mno, Mwanakwetu aliingia katika kampuni moja binafsi iliyokuwa inakatisha tiketi za ndege na kuwaomba kuchaji betri yake, huku akiwauliza chanzo kikubwa cha nguvu ya umeme huo katika hifadhi ni nini? Alijibiwa kuwa ni nguvu za jua ambayo gharama yake ni nafuu sana kuliko kutumia jenereta.

Kwa kando Mwanakwetu aliona jengo moja zuri lililofahamika kama Kituo cha Habari cha Utalii, alliingia hapo na kupata taarifa nyingi, likiwa ni jengo zuri lililofunguliwa na Waziri wa Utalii mhe.Mohammed Mchengerwa Machi 2023. Mwanakwetu akiwa hapo alibaini kuwa chanzo cha umeme cha jengo hilo jipya kilikuwa ni jenereta ambalo lilikuwa likiunguruma nyuma ya jengo hilo, akajiuliza- jamani mbona mnatumia jenereta muda mrefu?

“Hilo ni stand by jenereta, jengo letu lina mitambo ya jua lakini kuna itilatu imetokea na ndiyo maana tunatumia jenereta hilo.”

Msomaji wangu kumbuka jengo limefunguli Machi 2023 hadi Mei 27 ambayo inakaribia mwezi mwezi na siku chache itilafu ya umeme imetokea jenereta linaokoa jahazi.

Mwanakwetu alibaini kuwa inavyoonekana kuwa chanzo hicho cha umeme wa jua katika jengo hilo kimeharibika kwa siku kadhaa kwa hiyo jenerata linatumika kwa siku kadhaa pia, akasema moyoni mbona kampuni binafsi zinatumiwa chanzo cha jua kwa nini chanzo hiki cha jua cha Chumba Habari za Utalii cha umma kisitengenezwa haraka?Mwanakwetu alikwenda kuchukua betri yake na kuendelea na safari yao ya kutali ndani ya hifadhi ya Serengeti.

Walipotoka hapo , yule ndugu mwalimu aliyezaliwa ndani ya eneo hilo akasema maneno haya

“Mnaziona hizi barabara za mbugani? Zamani zilikuwa nzuri sana, lakini sasa hali yake si nzuri maana miaka ya nyuma hauwezi kupita mbugani usikutane na harakati za utengenezaji wa barabara, sasa hilo ni adimu mno, maana pesa inakusanywa inakwenda hazina, alafu unaomba pesa za kutumia ndipo wakupatie.”

Kweli hadi wanatoka mbugani saa 12.00 ya jioni hawakuweza kuona utengenezaji wa barabara yoyote japokuwa kwa mtazamo wa Mwanakwetu barabara zote zilikuwa zinapitika vizuri.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Mwanakwetu anaunga mkono utaratibu wa kukusanya mapato ya serikali na kwenda hazina na baada ya kukusanya ndipo matumizi yapangwe nayaombwe kwao. Hilo Mwanakwetu analipigia chapuo na lidumu milele.

Mwanakwetu anakumbusha TANAPA wafahamu kuwa chanzo cha gharama nafuu cha nishati ya umeme katika hifadi ni nguvu ya jua pekee, kama kuna hitilafu yoyote ile kama ile Sorenera itengenezwe mara moja. Taasisi zote za TANAPA na za umma tujitahidi kuishi kama majumbani mwetu, hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kuliwasha jenerata lake la dharura nyumbani kwake hata kwa siku tatu mfululizo lazima ataumizwa na gharama za mafuta, moyo huo uhamishiwe katika mali za umma. Hilo wakaguzi wa ndani wa TANAPA wanapaswa kuliona mapema kabla ya mkaguzi wa Mkuu wa hesabu za Serikali hajafika kukagua maana dharura itakiwa ziwe chache.

Gharama za vyakula katika mbuga zetu ziwe rafiki ilikusaidia watalii makabwela kama akina Mwanakwetu wasiogope kula vyakula ndani ya mbuga hizo, kukiwa na gharama nafuu hilo litasaidia watalii wengi kuwa moyo na kutamani kwenda kutalii kila mara, leo akitoka Mikumi kesho atakwenda Serengeti, siyo tena Mwanakwetu abebe chupa ya soda yake ya dare more kutoka nyumbani. Hili la chakula ni jepesi tu akina mama jirani na mbuga watengeneze vikundi vya lishe, TANAPA wawatengenezee boma nadhifu, wapike kwa zamu kipindi wakati watali ni wachache, watalii wakiwa wengi wapike wote ili makabwela waweze kula na siyo kushinda na njaa siku nzima katika hifadhi zetu.

Mwanakwetu alipotoka huko akaamua akusimulie simulizi hii ya uchoyo wa mbugani ambayo ni kulala na chakula siyo kuona wanyama.Mwanakwetu upo ? Nakutaki siku chema na huu uchoyo wa mbugani.

makwadeladius@gmail.com

0717649257













0/Post a Comment/Comments