WANYAMA WANA WAO ULIMWENGU

 




Adeladius Makwega-MWANZA

Wanachuo wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya mkoani Mwanza wamefanya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania, Mei 27, 2023 ikiaminika kuwa ni hifadhi pekee yenye mkusanyiko mkubwa wa wanyama wanaohamahama pamoja na kuna uwepo wa wanyama wengi jamii ya paka.

Ziara hiyo ilizinduliwa na wanachuo hao kuona kundi kubwa la swala ambalo mwongozaji wa watalii ambaye alikuwa mahiri mno kwa kutoa simulizi za wanyama hao alisema,

“Katika makundi ya swala kuna aina mbili; kundi la swala dume mbabe ambaye huambatana na majike kadhaa ambapo kundi hilo la swala dume mbabe mmoja hupanda kundi kubwa la majike. Kundi la pili huwa na  swala ambao ni madume pekee ambayo hawana umiliki wa kundi lolote ambapo kumiliki kundi la majike hao lazima dume mgeni apigane na dume lenye hadhi hiyo, akishinda anaondoke na majike maana majike ya swala yanahitaji dume jasiri kwa kuwalinda na kupandisha .”

Safari ya utalii iliendelea na baada ya mwendo wa dakika tano hivi walikutana na kundi la swala madume kadhaa ambayo yalikuwa yanakula nyasi yenyewe, yakisubiri na kuvizia kuvamia kundi la swala dume aliyekuwa anamiliki majike kadhaaa.




Maelezo hayo ya mpambano wa kumiliki kundi yalithibitiswa na swala dume alionwa na Wanachuo wa Chuo cha Maendelea ya Michezo, alikuwa na pembe moja ya mkono wakushoto ilikuwa imevunjika nusu, hilo likionesha kuwa pengine kabla ya kumiliki kundi hilo kulikuwa mapigano makubwa.

Akifuatilia hatua kwa hatua ya ziara hiyo Ladislaus Lungunya ambaye ndiye aliyekuwa mratibu wa ziara hiyo kwa wakurufunzi hao alisema kuwa anashukuru ziara yao inafikia ukingoni lakini amejifunza kuwa maisha ya wanyama yamemshangaza mno.

“Huku duniani tunasema ni ulimwengu wa binadamu, kumbe mbugani pia kuna ulimwengu wa wanyama ambao una mambo mengi makubwa na mazito pale unapoyafuatilia tu.”

Usafiri waliopanda uliendeshwa na dereva mmoja makini mno, alipokea maelekezo kutoka kwa mwongozaji wa watalii kuhusu njia ya kupita. Wanachuo hao macho yao kwanza yalikutana na Tembo ambao hawakuwa na shida kwao.Walielekezwa kwa mwendo kidogo huko walikutana na simba waliopumzika.

Wananchuo hao walipotoka hapo walikwenda umbali mrefu na wakawaona mamaba kadhaa waliokuwa katika bwawa moja ambao ilibainika kuwa kulikuwa na kama bonde ambalo maji yalikuwa yakikimbia kwa kasi mno nao mamba walikaa katikati ya kona hiyo naye mwongazaji wa watalii akisema,

“Mamba amekaa hapo akiwakamata kambale kadhaa wanaotoka katika maji hayo na kuwala, mamba yule ambaye mdomo wake ulikuwa wazi pengine hufunga na kumeza wadudu wote waliopo humo na wkati mwingine wadudu na ndege wanaotua katika mdomo huwa wanamtoa kumsaidia kuwa kama vijiti vya kutoa uchafu katika meno ya mnyama .



 

Safari ya Hifadhi ya Senrengeti ilielekea upande wa pili ambapo kulikuwa na mto mmoja ambao ulikuwa umepungua maji huku yakionekana magogo meusi yaliyolala katika maji, hapo mwongozaji wa watalii hao wa ndani alisema kuwa hayo si magogo bali ni viboko na kweli mara baada ya dakika kadhaa viboko hao wakaanza kupiga kelele. Huku mwongozaji akijibu kuwa hapo kiboko mkubwa anawajulisha wenzake kuwa wawe tayari kwa chochote kile maana kando yu adui.


Mara walitokea viboko wawili jike na dume toka upande wa pili wa mto ambapo mwongozaji watalii alisema walitoka kula majani .

“Kama ilivyo duniani watu wawili wawili yaani mke na mume kila mmoja na wake na hata katika ulimwengu wa wanyama mambo ni wawili wawili. Jamani na ndiyo maana hata mimi nilimchagua mwongozaji awe jirani yangu katika kutalii mbuga hii maana nilivutiwa na utanashati wake. Nawaomba mpunguze maswali msimchoshe sana.”

Hayo yalisemwa na mwanachuo mmoja wa kike ambaye alikuwa jirani na mwongozaji watalii huku wanachuo wengine wakishangilia maneno haya ya utani ndani ya Hifadhi ya Serengeti.

Hadi jua linazama la Mei 27, 2023 wanachuo hao walikuwa wameshazunguka sehemu kubwa ya hifadhi hii wakiwaona Tembo, Twiga, Swala, Mamba , Nyumbu, Pundamilia , Nguruwe Pori na wanyama wengine ambao ni utajiri mkubwa wa Hifadhi ya Serengeti

makwadeladius@gmail.com

0717649257





0/Post a Comment/Comments