Adeladius
Makwega-MWANZA
Mei 29, 2023 Mwanakwetu alikuwa katikati ya Jiji la Mwanza ambapo
alitumia muda wake mwingi wa siku hiyo katika ofisi moja ya serikali, mara
baada ya kumaliza kilichompeleka huko alipanda daladala kutoka katika ya Jiji
hilo kuelekea Nyamuhongolo ambapo kuna kituo kikubwa cha mabasi yanayokwenda
maeneo mbalimbali ikiwamo Kwimba.
Hapo Nyamhongolo alifika saa nane na dakika ishirini za
mchana huku ukiwa ni muda wa mabasi ya mwisho mwisho, akiwa upande wa mabasi
yanayokwenda Kwimba, Sumve na Ngudu alimpa utingo shilingi 5000/=na kumwambia,
“Ninakwenda kula, narudi mara moja, tiketi
yangu nakuja kuchukua, natambua basi lenu ni la mwisho, msiniache.”
Kondakta alipokea pesa hiyo na akamwambia
Mwanakwetu maneno haya,
“Mzee nakukumbuka sana, nakukumbuka sana mzee wangu, tulikuja
na wewe alfajiri, wewe ni abiria wetu, nakumbuka pale Malya saa 10 ya Alfajiri uliniuliza
nauli hadi Mwanza ni kiasi gani ? Nikakujibu ni shilingi 6000/= Natambua wewe
unatoka Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya.”
Mwanakwetu akatabasamu si kwa kuwa
Utingo huyo alizungumza kwa maneno yenye matamshi ya Kisukuma tu bali kutokana
na utingo kumfahamu mno abiria wake mgeni.
Mwanakwetu akaenda kununua chakula
chake katika mkahawa wa kando na stendi hiyo ambapo alikuwa na njaa ya siku
nzima maana hakula chochote tangu Mei 28, 2023 na huku hakuwa na mfungo wa
Kwaresma wala Ramadhani.
Akiwa anaagiza chakula hicho
Mwanakwetu alisema maneno haya moyoni,
“Kituo hiki cha basi ni kizuri sana, lakini shida ni
ukamilishaji wa miundo mbinu yake ya nje ya kituo, maana kisipomaliziwa mvua
zikinyesha kinaweza kuharibika hasa eneo linalopokelea daladala la nje ya kituo
bado halijakamlishwa, kinapaswa kukamilishwa mara moja kabla ya msimu wa mvua.”
Mwanakwetu akalipia chakula, akaanza
kula, huku kwa kando yake walikuwapo jamaa wawili wakila chakula, jamaa hawa
wawili aliwasikia wakijibizana na muuzaji wa mkahawa huu juu ya malipo ya umeme
kwa kuwa walitumia kompyuta mpakato kwa kuichomeka katika umeme.
“Hapa utaratibu wetu hata kama umekula chakula cha gharama kiasi
giani kama unachaji simu au unatumia kompyuta mpakato na umechomeka katika
sokti yetu unatakiwa kulipa shilingi 1000/=“
Jamaa hawa walibishana na muuzaji wa
kiume hivyo akaitwa mama mmiliki wa mkahawa huo wa kituo cha basi cha
Nyamhongolo, alipofika akasema maneno haya,
“Jamani hapa tunalipia umeme na gharama ni kubwa, nawaombeni
mlipie ili biashara zetu zisonge au mnataka turudi Musoma tukalime? Tena nyinyi
ni kaka zangu ebu lipeni mara moja.”
Walizngumza maneno ya lugha moja ambayo
Mwanawetu hakuitambua, wakacheka na hawa ndugu wakalipia shilingi 1000/= huku
mama huyu akarudi alipokuwa ameketi katika sehemu ya kaunta.
Hawa jamaa waliolipa shilingi 1000/=
mmojawpao akatoa simu yake akawa anasikiliza maelezo ambayo yalikuywa
yakichezwa katika simu hiyo.
“Jamani mimi nimekuja hapa kuwaona, kuwasalimu na kuwapa pole
kabla sijakwenda kule, nawaombeni kuwa ili kutatua mgogoro huu lazima nifike alafu
nitakwenda kule na ndiyo maana leo nipo hapa, tambueni kuwa serikali yenu ya
mhe. Rais Mama Samia haipendi migogoro…”
Jamaa hawa wakasema huyu ni mhe Said
Mtanda mkuu wa mkoa wa Mara, anaonekana ni mtu mwema, kiongozi mzuri na mchapa
kazi. Jamaa mmoja mwingine akasema muda wote tulikuwa tunachelewa wapi kumchagua
ndugu Mtanda kuwa mkuu wa mkoa? Mwenzake akasema kuwa serikali huwa haichelewi.
Mwingine yaani aliyelipa shilingi 1000/=ambaye ndiye aliyekuwa na simu iliyocheza
video hiyo akasema sawa serikali huwa haichelewi lakini wananchi wake huwa wanachelewa
akaendelea kusema,
“Unaweza kusema watu wa Mara ni wakorofi, hivyo aende mkorofi
akawaongoze, hilo ni kosa, tunataka watu waungwana kama Mtanda. Kwa
ninavyomuona huyu jamaa atatusaidia mno .”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu
kando anakula wali wake, samaki na soda, mara akaona kwa mbali basi alilowapa
nauli yake linaondoka, hivyo hawa jamaa wa mkahawa akawaomba wamfungie samaki
wake haraka haraka katika mfuko na akaelekezwa alikimbilie getini kwa kulikatia
denge basi hilo na kweli alikimbilia na kuwahi na kupanda, huku begi mgongoni
na samaki mkononi. Akaoneshwa kiti chake na kukaa, akamla samaki na kunywa soda
yake na kuendelea na safari ya Malya Kwimba.
Mwanakweu siku ya leo anasema nini?
Hawa jamaa wawili mkahawani
walimkumbusha Mwnakwetu kumtakia kazi njema mhe. Said Mtanda katika kuwahudumia
watu wa mkoa huu ambao ni nduguze mwalimu Julius Nyerere. Kwa hakika Mwanakwetu
anaushaidi mkubwa wa uhodari wa mwanasiasa huyu (Said Mtanda) , ushahidi wa
miaka karibu 12 wa kuwa kiongozi ambaye ukimwambia jambo analifanyia kazi na
kulipatia ufumbuzi,yeye siyo kiongozi wa kumwambia jambo alafu aone unamsumbua.
Kwa ufupi tu na kwa faida ya wasomaji
wa Mwanakwetu, mwaka 2011 Mwanakwetu aliwasiliana na ndugu Phares Magesa ambaye
alikuwa mjumbe wa Halimashauri Kuu ya CCM Taifa wakati huo akitokea mkoa wa
Dares Salaam, ndugu Phares Magesa ambaye alisoma Azania sekondari miaka 1990 na
Mwanakwetu aliyesoma Tambaza kipindi hicho hicho wanafahamiana maana walikuwa
vijana wa Dar es Salaam.
Waliwasiliana na mhe. Said Mtanda na
alipopewa jambo hilo walilolilamikia mhe. Mtanda alilifanyia kazi na
kuwasikiliza waliomfuta hadi jambo hilo likapatiwa ufumbuzi, wakati huo
mhe.Mtanda hakuwa na nafasi yoyote kubwa, bali ni moyo wake wa kuwasaidia watu
wenye shida na kuzipatia ufumbuzi kwa kuzikifikisha pahala husika na huo
Mwanakwetu anasema ndiyo uongozi.
Mwanakwetu anatambua miaka hiyo 12 ni
mingi inawezekana mh. Said Mtanda amesahau labda akumbushe na ndugu Phares
Magesa ambaye alikuwa Rais wa Mpira Kikapu na Kiongozi wa Skauti Tanzania.Ndugu
Phares Magesa kwa ambao hawamfahamu yeye ndiye mtoto wake amekubwa bingwa wa Hisabati
hivi karibuni.
Mwanakwetu anaomba sana Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara kwa wanaopanga safu waitazame kwa umakini ili
iwe na viongozi watakaendana na kumshauri vizuri mhe Said Mtanda. Mwanakwetu
anatambua fika inapotazamwa kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa , Jeshi la
Polisi halina shida maana wao kila mara wanabadilisha na kuhamisha makamanda
wao. Idara zingine zipigwe picha kwa kina ili kuweka safu bora ili kuyafikia malengo
ya wananchi na serikali, kumbuka sana maneno ya hawa jamaa wawili katika kituo
cha Nyamuhongolo kuwa watu wanachelewa lakini serikali haichelewi. Mwanakwetu
anasema kama watu wanachelewa na serikali inachelewa pia maana serikali ni watu
na watu ni serikali.
Mwanakwetu upo ?Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment