Adeladius Makwega-MWANZA
Juni 12, 2023 Mwanakwetu alipata taarifa juu ya kifo cha mwanahabari
mkongwe, Bi Leila Sheikh ambaye alikuwa mtetezi wa haki za wanawake katika vyombo
habari hapa nchini.
Msiba huo ulimsitua Mwanakwetu na alipofuatilia zaidi alibaini
kuwa mazishi yake ni Korogwe Tanga Juni 13, 2023 ambapo Mwanakwetu amemuagiza
mkewe akashiriki mazishi ya mama huyo.
Kwa hakika Mwanakwetu ameipokea taarifa ya msiba huo kwa
masikitiko makubwa, maana kwa ulimwengu wetu wa sasa watu wengi si kwamba hawajitoi
kwa ajili ya watu wengine, wanafanya hivyo lakini kwa maslahi yao binafsi ,
tofauti na marehemu Bi Leila Sheikh ambaye aliweza kujitoa kwa maslahi makubwa
ya wanahabari wanawake kwa wanaume kujenga uimara wa habari Tanzania.
Mwanakwetu
anakumbuka mawasiliano ya awali baina yake na Bi Leila Sheikh ni miaka karibu
18 ambapo kufahamiana na mwanahabari huyu kulitokana na Mwanakwetu kusoma sana
maandiko yake hasa juu ya wanahabari wanawake walivyokuwa wakikosa fursa nyingi
katika vyombo habari kutokana tu na kuwa mwanamke .
“Wanawake
wana mambo mengi, kazi hiyo mtumeni mwanaume , itafanyika vizuri.”
Haya yalikuwa maneno ya kawaida katika vyumba vya habari. Unaweza
kuona sasa Mkurugenzi wa TSN Bi Tuma Abdallah kuongoza taasisi hiyo kwa sasa ni
jambo la kawaida, Mwanakwetu mambo zamani hayakuwa hivyo , zipo simulizi nyingi
za kusikitisha ambazo Mwanakwetu hataki kuzisema leo hii lakini mfano mmojawapo
hata kwenda kuripoti Vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa
ni mtihani mzito kupangiwa mwanahabari mwanamke.
Mwanakwetu
alikuwa akisoma makala nyingi za Bi Leila Sheikh na mara nyingi kuzinukuu makala
hizo, hapo ndipo Bi Leila Sheikh akamfahamu Mwanakwetu kwa jina na si jinsia.
Urafiki baina
ya Leila Sheikh na Mwanakwetu ulikuja kwa utata ambapo mwanahabari huyu alituma
ujumbe Mwanakwetu ajiunge na TAMWA, mjumbe huyo akamjibu kuwa Adeladius Makwega
na mwanaume.
“Bwana
nilitaka ujiunge na TAMWA, hapa nimeambiwa kumbe wewe ni baba, samahani
mwanangu, ukifika Dar es Salaam nitafute tuongee.”
Tangu siku hiyo Iringa Press Club na vyama vingine vya kihabari
vikawa na jirani na Mwanakwetu ambaye alikuwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari
Isimani Tarafani Iringa Vijijini na mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa.
Kuna wakati Mwanakwetu aliandika habari na makala katika
Gazeti la KULIKONI juu ya Shule ya Msingi Ugele iliyopo katika Manispaa ya
Iringa Mjini ambapo ilikuwa na mwalimu mmoja tu huku kaka mkuu akisaidia kufundisha
wanafunzi wenzake wa darasa la kwanza, pili , tatu na la nne. Mwanakwetu alifika
shuleni hapo na kupiga picha ya tukio hilo na kuandika habari na makala hiyo baada
ya kujulishwa hilo na mwanahabari Mpoki Mwakapisu ambaye sasa ni Afisa Habari
mkoani Iringa.
(Pili Mtambalike, Wangali Maasai (Prof) na Leila Sheikh mwaka 2002)
Mwanakwetu anakumbuka MISA TAN,TAMWA na Ubalozi wa Marekani
Nchini Tanzania walitoa zawadi na vyeti kwa wanahabari walioandika habari za vijijini
ambapo Adeladius Makwega alikuwa miongoni mwao, huku akishiriki mafunzo,
akapata cheti, akapata pesa na hapo ndipo alikutana uso kwa uso na marehemu Leila
Sheikh kwa mara ya kwanza
“Mwanangu
mwandishi wa Iringa umekuja ? Umepata posho yako ? Umefikia wapi? Vipi Shule
yako ya Ugele walipelekwa walimu? Vipi na yule kaka mkuu alifaulu mtihani wa
darasa la saba?”
Mwanakwetu alijibu kuwa amefika, posho yake amepata, amefikia
nyumbani kwao Mbagala na Shule ya Msingi Ugele ilipangiwa walimu wa kike wanne,
huku walimu watatu wameripoti na mwalimu mmoja aliripoti na kutorudi tena kituo
chake kipya cha kazi kutokana na mazingira magumu ya eneo hilo yalivyokuwa
wakati huo.
Shule hii ilikuwa na mwalimu mmoja ambaye alikuwa mwanaume
hivyo ujio wa walimu watatu hilo lilisaidia mno eneo hilo wakati huo.
Msomaji wangu gazeti la KULIKONI walichapisha habari na makala
hayo,MISA TAN, TAMWA na Ubalozi Marekani wakatoa zawadi kwa mwandishi , hapo
hapo Afisa Elimu Mkoa wa Iringa alipoona tu Makala hayo wakalifanyia kazi jambo
hilo, ambalo leo hii si tatizo tena. TAMWA iliyofanya hivyo ni ya Leila Sheikh ambaye
leo hii amefariki dunia.
Inawezekana watu wa Kijiji cha Ugele Iringa Mjini jambo hilo
wamelisahau, lakini Mwanakwetu anatumia buriani hii kuwakumbusha hilo kuwa mama
huyu aliyempa motisha mwanahabari aliyendika makala juu ya uhaba wa walimu shuleni kwao amefariki dunia.
Kwa Mwanakwetu, ndiyo kusema Bi Leila kwake ni mama yake kwa
maana hata pesa ya kwanza ya kihabari aliipata kwa fursa aliyopewa nayeye.
Mwanakwetu kwa heshima zote anatoa pole kwa wananahabari wote
wanaoheshimu mchango wa huyu mama, pili anatoa pole kwa TAMWA kwa kuondokewa na
kiongozi wao wa zamani na tatu anatoa pole kwa ndugu na familia yake kwa kumpoteza
ndugu yao aliyeliwakilisha vema jina la ukoo wao katika kutenda utu kwa
binadamu wenzake.
Mwanakwetu upo? Buriani Bi Leila Sheikh.
makwadeladius @gmail.com
0717649257
Marehemu Leila Sheikh akiwa binti.
Post a Comment