Adeladius Makwega-MWANZA
Sura yake ya kwanza inaeleza hadhi ya binadamu yeyote: ingawa karibu wote
wanakubali kuwa mtu ni kiumbe bora duniani, Kanisa linasisitiza ukweli huo kwa
kumuona na kumuita “sura ya Mungu” hata
baada ya kuathiriwa na dhambi.
Ndio msingi wa heshima anayostahili
katika mwili na zaidi katika roho
ambayo kwa akili inaweza kujipatia ukweli na hekima, kwa dhamiri inasikia wito wa Mungu,
na kwa hiari inaweza kuuitikia.
Lakini Kanisa, pamoja na kusisitiza
hiari kama wanavyofanya wengi siku hizi, linahimiza pia kuitumia vizuri, kwa
kuwa mwishoni kila mtu atahukumiwa juu ya matumizi ya vipawa vyake.
Baada ya kukabili suala la kifo kwa
kutangaza habari njema ya ufufuko, hati inakabili janga mojawapo la siku hizi, yaani
kwamba wengi wanakanusha uwepo wa Mungu au wanaishi bila ya kumjali yeye.
“Mtaguso ulifikiria hasa
ukomunisti na misimamo mingine ya kupinga na kuzuia dini zote,
lakini badala ya kuilaani tu, umehimiza Wakristo wajadiliane na kushirikiana nayo,
pamoja na kutoa ushuhuda wa maisha bora, ukikiri kuwa pengine mifano yao mibaya
ndiyo iliyosababisha wengi wakose imani.”
Mwisho inachorwa taswira ya Yesu Kristo,mtu mpya, ambaye
pekee yake anaangaza fumbo la binadamu pamoja na uchungu na kifo.
Katika sura ya pili kwa kifupi
inatoa mafundisho kuhusu jamii yanayozingatia mpango wa Mungu wa kuwa watu
waishi kwa ushirikiano: kuukamilisha kwa msingi wa haki
ni muhimu kuliko maendeleo ya ufundi tu.
“Kwa ajili hiyo kila mtu
awajibike kuhusu wenzake wote bila ya kumsahau hata mmoja, akiwa jirani na wa wenye
shida na kujitahidi kustawisha usawa kwa kutumia nafasi
yoyote aliyonayo katika jamii.Maadili ya kibinafsi hayakubaliki, bali wajibu mkuu
mmojawapo ni kujihusisha na ustawi wa jamii na
mshikamano ili wote kwa neema
ya Kristo waishi kijamaa.(kidugu).”
Sura ya tatu yenyewe inalipigia
chapuo msimamo kuhusu utendaji wa binadamu
ulimwenguni.Hasa leo ambapo maendeleo ni ya haraka watu wanajiuliza kuhusu
maana ya juhudi zao na namna ya kuziendeleza. Ni hakika kuwa Mungu amewaagiza
wafanye kazi na kutawala ulimwengu ili wote wapate hali ya maisha
wanayostahili walio sura yake.
“Wakristo wanapaswa kuwa
mstari wa mbele katika kutafuta ushindi
wowote wa binadamu juu ya maadui wake ambao ni ujinga,maradhi na ufukara na ushindi huo unatangaza ukuu wa Mungu aliyemuumba binadamu
.”
Pia hapa imesisitizwa binadamu
asisahau kuwa ubora wake hautokani na wingi wa vitu anavyojipatia, bali
unategemea tunu za kiadili anazostawisha kwa kazi yake, hasa haki na udugu.
Shida ni kwamba mara nyingi akishindwa
na dhambi anafuata ubinafsi au utaifa na kuanzisha miundo ya dhuluma na vita hata kutengeneza silaha za kutosha kuangamizia uhai wowote
duniani.
Mbele ya hali hiyo Wakristo wameombwa
wanapaswa kutofuata mitindo ya ulimwengu bali njia ya upendo nyuma ya Kristo,
wakiwa tayari kubeba msalaba wanaotwishwa wale wanaotafuta haki
na amani.
Tumaini la uzima wa milele lisipunguze bidii za kuboresha maisha ya binadamu wa leo, kwa kuwa huyo anaandaliwa hapa duniani kuingia katika ufalme wa mbinguni. Katika utendaji wake mtu ana haki ya kufuata taratibu zaelimu dunia,siasa n.k.
Imani haiogopi kumuachia nafasi
hiyo, kwa kuwa Mungu yuleyule aliyejifunua kwetu kwa imani ameumba pia vitu
vyote na kutujalia akili na uvumbuzi. Mtaguso
umelaumu mawazo finyu yanayogonganisha imani na sayansi.
Katika sura ya nne, hii inaeleza
yatokanayo na zile zilizotangulia, yaani uhusiano wa Kanisa na ulimwengu.
Kanisa likiwa na lengo la milele,
linaishi duniani na wanae pia raia wa nchi zao. Hivyo linachangia ustawi wa
binadamu pamoja na kupokea kwa shukrani misaada
mbalimbali ya walimwengu. Lina ujumbe kwa watu wote kuhusu wokovu, lakini pia kuhusu maisha haya, hasa hadhi na haki za
kila mtu.
“Kwa hiyo, ingawa utume
wa Kanisa ni wa kidini hasa, linashughulikia pia ustawi wa jamii na umoja wa mataifa. Wakristo wasisahau tena majukumu yao ya
kidunia, wala wasiyaone hayahusiki na imani.Mojawapo kati ya makwazo makubwa
zaidi ya nyakati zetu ni utengano huo kati ya imani na maisha ya Wakristo
wengi. Kwa namna ya pekee, walei wanapaswa kushughulikia malimwengu yote kwa
mfano wa Yesu huko Nazareti. Wasisubiri kuagizwa na
wachungaji wao, kwa kuwa kuratibu hayo ni kazi ya walei hasa.”
Mtaguso umekiri tena ukosefu wa wanakanisa
na kuwahimiza kujirekebisha wasije wakazuia uenezaji wa
Injili. Vilevile umeshukuru kwa juhudi za watu wowote kwa ajili ya
ustawi wa familia, utamaduni, uchumi, jamii, amani na mshikamano wa
kimataifa, hata ukakiri Kanisa limefaidika sana na upinzani na dhuluma za
maadui wake.
Inaendelea sehemu ijayo.
0717649257
Post a Comment