Adeladius Makwega-MWANZA
Baada ya kumaliza kueleza kwa jumla
jinsi Kanisa linavyohusika na wito wa binadamu, hati hii katika sehemu ya pili
inakabili masuala kadhaa yaliyo muhimu zaidi kwa watu wa leo.
Kati ya hayo sura ya kwanza
inafafanua kwanza hadhi ya ndoa na familia na namna ya kuzipa nafasi za kufaa, kwa sababu
mengine mengi yanategemea hali ya familia. Baada ya kueleza utakatifu wa ndoa, kwa kuifananisha na hali ya kuwekwa wakfu
kwa njia ya sakramenti za
kudumu, mtaguso umeonyesha ubora wa upendo kati ya mume na mke na
namna ya kuutekeleza, ukisisitiza unavyoelekea uzazi.
Hivyo watu wa ndoa wanapaswa kupanga
kwa pamoja mbele ya Mungu na kwa kuzingatia mafundisho ya Kanisa ili wazae kwa busara na ukarimu.
Kwa namna ya pekee inasisitizwa kuwa
ni lazima uhai wa binadamu kisha kuanza ulindwe kwa bidii zote: kuua mimba
au mtoto ni maovu ya kutisha.
Katika magumu yanayohusu uzazi wa mpango, wanandoa wajitahidi kuwa na kiasi na kufuata usafi wa moyo jinsi inavyowafaa.
“Hata jamii nzima inatakiwa
kuchangia ustawi wa familia: viongozi watunge sheria na kufanya mipango kwa ajili hiyo; wanasayansi
waendelee kutafuta njia halali za kupanga uzazi; mapadri wafanye juu chini
familia ziishe kwa utulivu.”
Sura pili hii inafikiria namna za
kustawisha utamaduni, yaani zile namna maalumu ambazo binadamu anakabili maisha
katika mazingira na nyakati mbalimbali kulingana na orodha ya tunu
anazothamini. Tofauti na wanyama, yeye hawezi kufikia hali ya maisha ya kumfaa
kweli asipoyafanyia kazi mema yaliyoumbwa na Mungu ndani mwake na kandokando
yake.
Kila kabila na kundi la watu lina utajiri wake ambamo binadamu
achote ili kujiendeleza na kuwaendeleza wenzake.
Lakini huu wa leo ni wakati mpya wa historia kwa sababu ya mabadiliko ya haraka mno. Upande mmoja
zimefunguliwa njia mpya za kukuza na kueneza elimu
na za kuunganisha aina tofauti za utamaduni. Upande mwingine kuna hatari za
kufuta hekima na sura maalumu za kila jamii, kuvuruga mafungamano kati ya
vizazi, kuacha elimu ya juu mikononi mwa wataalamu tu
n.k.
Kufuatana na amri ya upendo Wakristo
wanatakiwa kuchangia na wenzao ujenzi wa ulimwengu ili wote waone vizuri kazi
ya Mungu na namna ya kuiendeleza.
“Kama vile yeye
alivyotumia utamaduni wa watu ajifunue kwao, ndivyo Kanisa pia lilivyofanya na
linavyopaswa kufanya katika kueneza habari njema. Lenyewe limetumwa kwa mataifa
yote, hivyo halibanwi na utamaduni wowote, bali linautumia na kuuchangia,
linausafisha na kuuinua lisiishie ndani yake.”
Ni wajibu wa wote kujitahidi kufuta
ujinga kwa kueneza elimu hasa ya msingi ili kila mtu aweze kuchangia zaidi
ustawi wa jamii. Vilevile kila mtu aelewe wajibu wa kujiendeleza kiutu na
Kiroho bila ya kutawaliwa na kazi za mikono tu, akitumia vitabu na vyombo vingine vya upashanaji
habari, muda huru ulio nje ya kazi n.k.
Sura ya tatu inafundisha kuhusu
maisha ya kiuchumi na ya kijamii ya mtu wa nyakati zetu.Ni lazima huyo awekwe
juu kabisa kuliko maendeleo ya vitu, kwa kuwa ndiye mtendaji, kiini na lengo la
uchumi na la jamii.
Kumbe wengi wanazingatia sheria za
uchumi tu ili kutajirika iwezekanavyo.Matokeo ni kwamba mtengo kati ya mataifa,
na kati ya matabaka ndani ya nchi, unazidi kuwa mkubwa. Anasa za wachache
zinaleta ufukara wa kutisha wa umati hata kuhatarisha amani duniani.
Binadamu wa leo anaweza kurekebisha
hali hiyo, lakini yanahitajika mageuzi mengi katika mitazamo, mazoea na
miundo pia. Hapo tu ongezeko la uzalishaji litasaidia kweli, yaani litamsaidia mtu yeyote
katika mahitaji yake yote ya mwili, ya nafsi na ya roho. Kwa ajili hiyo ni
lazima uchumi usiachwe uende zake wala usitawaliwe na wachache, bali wote
waweze kuuchangia ustawi na uongozi wake bila ya ubaguzi, wakisaidiwa
kushika nafasi yao hasa kwa njia ya ustadi.
Kazi ya binadamu iheshimiwe kuliko
mengine yanayohusu uchumi kwa mfanomtaji aumalighafi.Wote wana wajibu na haki ya kufanya kazi na
kujipatia hivyo riziki za kutosha.
“Vilevile wana haki ya
kupata muda kwa maisha ya kifamilia, hasa akina mama.Wafanyakazi ni haki yao
kuchangia uongozi wa kampuni, na vilevile kuunda vyama vya
kutetea haki zao hata kwa migomo.”
Mojawapo kati ya mambo yaliyozingatiwa
zaidi na mtaguso ni njaa ya umati; kwa ajili hiyo umekumbusha kuwa Mungu ameumba
vyote kwa ajili ya wote, basi ni lazima mali zigawiwe
kwa haki na upendo.
“Ingawa mtu yeyote ana haki ya kumiliki
vitu kadhaa, ni lazima kila mmoja awe na mali za kutosha, wasiwepo wenye
kujipatia mali nyingi kiasi cha kuacha wengine wakose hata mahitaji.Matajiri
wawajibike haraka kuwashirikisha wengine, la sivyo watakuwa wauaji wa wenye
njaa.Hao wa mwisho ni haki yao kujipatia riziki kutoka utajiri wa wenzao.”
Kadiri ya mazingira tunaweza kuwa na
njia mbalimbali za kuhakikisha wote wapate riziki zao kwa desturi za ukarimu,pensheni n.k.
“Mashamba yagawiwe kwa
wakulima wasiyonayo. Pesa zitumike ili kuandaa nafasi za kazi kwa watu wa leo
na wa kesho wa nchi zote.Wakristo watafute ufalme wa Mungu hata katika uchumi
na shughuli nyingine za kijamii.”
Inaendelea katika matini ijayo
0717649257
Post a Comment