FURAHA NA MATUMAINI IV



Adeladius Makwega-MWANZA

Sura  ya nne hapa inafikiria siasa ambayo pia siku hizi inapitia mageuzi makubwa.Mchango wa Kanisa ni kutetea heshima ya kila mtu kwa kusisitiza kwamba lengo la siasa ni ustawi wa jamii nzima kuanzia watu na familia.

Uongozi unahitajika ili kulinganisha kwa haki madai ya watu mbalimbali. Wananchi wote waelimishwe kuhusu siasa ili watoe mchango wao kwa kutumia nafasi wanazopewa kura n.k.na kwa kutetea haki zao bila ya kuwadai mno viongozi.

“Jamii na Kanisa vinawahudumia watu walewale lakini kwa namna tofauti, hivyo havichanganyikani bali ni vema vishirikiane. Hata hivyo Kanisa halifungamani na siasa yoyote, liweze kutangaza kwa uhuru maadili yanayotakiwa hata katika siasa, likipima mambo yote na kuhimiza yaliyo mema.”

Sura ya tano na ya mwisho inaongelea ujenzi wa amani na umoja kati ya mataifa.Wakati ilipoandikwa ulikuwa wa mafadhaiko makubwa kuhusu dunia nzima kuja kuangamizwa na wingi na ukali wa silaha zilizotengenezwa. Kwa msingi huo suala la vita linatakiwa lifikiriwe upya kabisa, wote wasiridhike na misimamo ya zamani kuhusu masharti ya uhalali wake.

Vilevile Wakristo wa madhehebu yoyote waungane kati yao, tena na wote wenye mapenzi mema, katika kujenga amani na haki. Kwa kuwa amani ya kweli sio tu kusimama kwa vita, labda kwa hofu tu ya silaha zilizolundikana; amani ni tunda la haki ambayo itafutwe mfululizo kwa bidii, tena ni tunda la upendo ule wenye msingi ndani ya Mungu.

Kuhusu vita vinavyoendelea huku na huku, kwanza ukatili wake upunguzwe kumbe siku hizi umezidi kwa sababu ya silaha mpya, mashambulizi ya raia, uangamizaji wa kabila zima n.k.

 

“Utiifu kwa maagizo hauwezi kuwa kisingizio cha kutenda maovu,

bali ni wajibu kuyakataa.”

Mapatano ya kimataifa kuhusu vita yaheshimiwe na wote. Ni wajibu wa viongozi wa nchi kuzilinda hata kijeshi, lakini wasitumie jeshi ili kugandamiza wengine. Pia waheshimu dhamiri ya wasiojisikia kutumia silaha.Vitendo vinavyowezekana leo vya kuangamiza miji mizima au maeneo mapana pamoja na wote waliopo ni makosa ya jinai yasiyovumilika.

Wanaotengeneza au kununua silaha ili kujikinga na maadui wasije wakashambuliwa, wafikirie hatari ya silaha hizo kuja kutumika kweli, tena hasara ya maskini wanaokosa misaada wanayostahili kwa sababu tu pesa nyingi sana zinatumika kwa silaha.



Itafutwe mapema njia za upatanisho na muundo wa kimataifa wenye uwezo wa kudumisha amani na haki kwa wote. Hapo katikati akiba za silaha zipunguzwe kwa mpango wa pamoja.Viongozi na watu wao waache utaifa na misimamo yo yote inayotenganisha watu.

Hasa malezi ya vijana na upashanaji habari vieneze mawazo ya amani na mitazamo mipana yenye faida kwa binadamu wote.

La sivyo watu watafikia tu ile amani ya kutisha itakayopatikana kwa kufa wote.Kanisa likisema hivi haliachi kutumaini na kuhimiza wongofu wa mioyo.

Kuhusu kujenga umoja kati ya mataifa, mara nyingi misingi ya kutoelewana ni hali tofauti mno za uchumi, nia ya kutawala, dharau ya wengine na vilema mbalimbali. Basi, ushirikiano mkubwa unaowezekana leo uwe njia ya kutatua matatizo hayo na kukidhi mahitaji ya watu, hasa maskini.

Miundo ya kimataifa iliyopo iwajibike kuzingatia zaidi nchi zinazoendelea, wakimbizi na wengine wenye shida maalumu.

“Ingawa miaka ileile ya mtaguso nchi nyingi zilipata uhuru wa kisiasa, hali ya uchumi inazirudisha chini ya ukoloni mamboleo; basi, mshikamano uendeleze kweli nchi hizo. Lakini maendeleo yanategemea watu kuliko pesa, kwa hiyo kazi ya kwanza ni kuandaa raia wa nchi maskini kwa elimu na ufundi.Inahitajika misaada, mikopo na vitegauchumi tena kwa ukarimu, lakini pia kurekebisha sana sheria za uchumi wa kimataifa.”

Upande wao viongozi wa nchi maskini wapokee misaada hiyo kwa uaminifu, na raia wao wajitahidi kutumia vile vyote walivyo navyo. Maendeleo ya uchumi yasisahaulishe roho ya binadamu, kwa kuwa huyo haishi kwa mkate tu.

Wengi leo wanafadhaishwa na kasi ya ongezeko la watu. Jawabu la kwanza kwa suala hilo ni kuleta usawa mkubwa zaidi kati ya watu na kueneza ujuzi kuhusu kilimo n.k. Halafu zitungwe sheria zinazosaidia familia, izuiwe kasi ya watu kuhamia mijini, watu waelimishwe kwa ukweli kuhusu hali ya nchi..

Wote wajiepushe na njia za mkato zinazokwenda kinyume cha maadili na cha haki ya msingi ya wananchi kufunga ndoa na kuzaa wanavyoona vema wenyewe. Basi, wasaidiwe kuunda dhamiri na kujifunza njia halali za kupanga uzazi.

“Wakristo wawe mstari wa mbele katika mshikamano wa kimataifa, wakijua Yesu katika maskini analia na kudai upendo.”

Mtaguso uliita kikwazokuona nchi za Kikristo zikitapanya mali, wakati nyingine zinalemewa na njaa, maradhi n.k.Wakristo wajitolee kuhamia kwenye shida ili kusaidia kwa hali na mali wakishirikiana na miundo na watu wowote, kwa kuwa tunaye Baba mmoja na tunapaswa kuishi wote kidugu.

Hapo watatambulikana kama wafuasi halisi wa Kristo.

“Wakikumbuka kuwa hawataingia mbinguni kwa kusema tu, Bwana, Bwana, bali kwa kutimiza mapenzi ya Baba, wakabili kazi hiyo kubwa ambayo watahukumiwa siku ya mwisho kwa jinsi walivyoifanya.”

Mwisho.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



 

 

0/Post a Comment/Comments