Lucas Masunzu- MAKOLE
Ilikuwa inakimbilia kuwa
saa mbili na nusu usiku. Kabla ya kulala Nduguyetu aliwasiliana na rafiki yake mmoja
ambaye walifahamiana muda mrefu. Rafikiye huyo anaishi mji wa Kano nchini Nijeria
ambako wanapatikana waigizaji wa filamu waliowahi kukonga nyoyo za watazamaji wengi
ndani na nje ya nchi akina Aki na Ukwa. Walizungumza mambo mengi huku
mazungumzo yao ya kijamaa yakitamatika kwa kufufua ahadi yao ya kutembeleana.
Baada ya mazungumzo hayo ndugu
yetu alijitupa kitandani kwake, alichelewa sana kupata usingizi siku hiyo akajikuta
kumbukumbu zake zinamkimbiza mpaka kwa Mchungaji Dkt. Paul Enenche ambaye naye
anatoka huko huko Nijeria mzawa wa mji wa Orokam alikutana naye tarehe 24 Juni,
2023 katika jiji la Dodoma. Mchungaji huyo ni mwandishi wa vitabu, mhubiri, na
kajaliwa talanta ya uimbaji mwenye uwezo wa kupiga vizuri mno baadhi ya ala za
muziki.
Nduguyetu alikumbuka
vizuri siku hiyo namna ambavyo Mchungaji huyo alivyotengeneza darasa kwa vijana
na watu wote waliokamia kuwa viongozi katika maeneo mbalimbali. Alizungumza
mambo mengi huku nyundo yake ya msisitizo iligonga zaidi msumari wa tabia kwa
kuwa tabia ina nguvu kubwa na inatazamwa mno kwa kiongozi yeyote yule.
“Ili uwe kiongozi lazima
uwe na wafuasi, tabia yako nzuri itafanya watu wengi wakufuate tena kwa hiari.
Tabia nzuri huaminisha na kukupa mamlaka.
Kiongozi yeyote mwenye tabia nzuri ana mamlaka huamrisha watu katika
kufanya majukumu mbalimbali na watu hao hutii. Kijana yeyote anayetaka kuwa
kiongozi lazima awe msafi wa tabia maana usafi wa tabia humfanya kiongozi awe
jasiri, kama hakuna ulichoficha hakuna cha kuogopa. Uchafu wowote wa tabia
hupunguza ubora wa kiongozi. Mathalani uchafu ukiingia kwenye mafuta hupunguza
ubora wa mafuta na ukiondolewa thamani ya mafuta hayo huongezeka. Ndivyo ilivyo
kwa kiongozi tabia yoyote chafu inapoishi moyoni mwa kiongozi mathalani ya
udanganyifu hupunguza ubora na thamani ya kiongozi huyo”
Kumbukumbu za ndugu yetu
zilichokoza hamu ya kuandika makala haya. Nduguyetu anasema kuwa kiongozi
akikosa sifa bora, ni vigumu mno hata kwa walio chini yake kufanya wajibu wao,
migogoro, kutokuelewa, hujuma, utegeaji, kukosa hamasa ni baadhi ya mambo
anayoweza kutaga kiongozi huyo mwenye
tabia ovu. Ili uwe kiongozi bora mathalani kanisani, kwenye biashara, kwenye
siasa au kwenye utumishi wa umma dondosha tabia zote ovu kwa maana ili mwezi uandame
ni lazima uliotangulia udondoke hivyo huwezi kuwa viongozi bora wakati bado unang’ang’ania
tabia, hulka na mienendo mibaya.
Nakutakia siku njema, Kwa heri!
theheroluke23@gmail.com
0762665595
2023.
Post a Comment