Adeladius Makwega-MWANZA
Julai 29, 2023 Mwanakwetu aliposhituka usingizini dakika 15
baadaye alichukua simu yake na kuingia katika kundi mojawapo la mitandao ya
Jamii, kundi hilo ni la huko wa Songwe. Alipoingia humo alikaribisha na
sentensi hii,
“Mungu adhihakiwi, yetu macho na masikio.”
Mwanakwetu alipoitazama sentensi hiyo
vizuri alibaini ilikuwa imepachikwa chini ya sentensi nyingine iliyokuwa na
maneno haya,
“Ukweli unachelewaga na wakati ukifika, nao huo unakuja.”
Mwanakwetu akawa anafuatilia huo
mjadala kutokana na ujumbe aliyoupokea karibuni hadi ujumbe aliyoupokea mapema
katika kundi hilo. Wakati anaendelea kusoma ujumbe huo akakutanna na ujumbe mwingine,
“Kichaa huyu.”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu
anaendelea kusoma ujumbe huo taratibu, hatua kwa hatua, sasa akakutana na
ujumbe huu,
“Pale unapogundua aliyekupiga risasi yupo ndani ya nyumba
yenu.”
Huu ujumbe juu ulikuwa umepachikwa katika
picha ambayo ilimuonesha mwanasiasa wa CHADEMA, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA,
Wakili wa muda mrefu wa kujitegemea na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa mbunge huko
Singida, mhe. Tundu Lissu.
Hapo Mwanakwetu akabaini kuwa
anayezungumziwa ni mhe. Tundu Lissu.
Mwanakwetu akatupa jicho tena tena
katika kundi hilo akakutana na picha kama ya ile ile iliyopachikwa katika
ujumbe lakini ilikuwa ni video, akaigonga, ikafunguka na kuanza kuitazama.
“Nyie mnamjua mambo yake, nyie si mnamjua mambo yake ! Lakini
kwenye hili tumsimlaumu, kwenye hili hayupo na mimi nitakwenda kufanya mkutano
Chato, nilikuwa nafikiria nisiende Chato kumuombea, nisiende kumuasha,
nitakwenda, nitakwenda kumwambia amka, amka uone (kelele za walihudhuria mkutano
zikisikika)amke amke usilale…”
Mwanakwetu akabaini kuwa katika video
ile mhe. Tundu Lissu alikuwa akihutubia mkutano mmojawapo wa siasa wa hivi
karibuni.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu
nyumbani kwake Asubuhi ya Julai 29, 2023. Mara baada ya video hiyo kukatika,
Mwanakwetu akapigiwa simu na kiongozi wa Jumuiya ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji,
“Kaka wahi jumuiya, viongozi wa Parokia wamefika, leo ni siku
ya mavuno.”
Mwanakwetu akakurupuka kukimbilia jumuiya
yake, akakuta wanasali na viongozi wa Parokia wapo mbele akiwamo Padri, ibada
ilikuwa fupi ambapo mwisho walimwagiwa maji ya baraka na kupewa baraka ya
mwisho ya ibada hiyo ya jumuiya na ibada hiyo ilikuwa fupi. Tamati ya yote
viongozi wa Jumuiya wakagawa stakabadhi za michango ya mavuno hayo huku Mwanakwetu
akipata stakabadhi yake namba 129.
Mwanakwetu akarudi nyumbani kwake, alipofika
tu akachuku simu zake alizoziacha mezani, huku video aliyoitazama awali ikiwa
bado katika kioo cha simu hiyo.
Mwanakwetu alipoiona video hiyo mara
ya pili, akasema maneno haya,
“Maoni yoyote yale ya mhe. Tundu Lissu dhidi ya John Pombe
Magufuli ambaye amefariki dunia, yanapaswa kutiliwa maanani leo hii sana sana na
yataendelea kutiliwa maanani kwa miaka mingi. Wale tulipobahatika kuishi
kipindi hichi ambao tumewaona hawa ndugu wawili, chochote tulichofanya au
tunalofanya hata tunavyoongea tutabeba mzigo ya hayo hapo kesho. Hawa ndugu
wawili wataendelea kuifikirisha dunia kwa kipindi kirefu sana. Vizazi vijavyo
vitatamani kama vingewashuhudia hawa ndugu.”
Kumbuka Mwanakwetu yu nyumbani kwake,
akaamua kufanya usafi wa nyumba yake, asubuhi hiyohiyo huku akiwatafakari ndugu
hao akilini mwake.
Hapo hapo zikamjia picha za watu watatu;
Dereva wa Tundu Lissu siku ya Septemba 7, 2017, Katibu Mkuu wa Wizara wa Afya
wakati huo na pia Mbunge mhe. Salim
Hassan Turky.
Mwanakwetu akamtilia maanani mno mhe
Salim Turky aliyezaliwa Februari 11, 1963, ambaye alikuwa Mbunge wa CCM Jimbo
la MPENDAE-ZANZIBAR.Mwanakwetu aliwaweka kiporo dereva na Katibu Mkuu wa Wizara
yaAfya wakati huo kwa sababu nyingi,kumbuka mhe Turky alifariki dunia Septemba 15, 2020.
Mwanakwetu akiwa bado akifanya usafi
huo, akakumbuka mara baada ya tukio la shambulio la mh Lissu , mhe. Turky alisema
maneno haya,
“Kwanza napenda kuiweka Tanzania katika hali ya usalama na
ukweli, maneno mengine siyo vizuri kuzushiana, tusifanye tukio la Tundu Lissu
tukataka kufanya siasa. Mimi binafsi tukio la Tundu Lissu, mbunge mwenzangu limenisononesha
sana na limenisikitisha sana na nikiwa kama kamishina wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, lakini kabla ya hapo pia mimi ni binadamu, ninaamini
kuna kuzaliwa na kufa. Kwa hiyo tukio lilivyotokeza, tuliitwa na spika
wetu(Job Ndugai), makamishina tukakaa na bahati nzuri Bwana Mbowe na Bwana Msigwa,
spika(Job Ndugai) na timu yake, waziri wa afya na madaktari, sote tukashirikiana
pale. Yaliyopita, yamepita mengi. Swali
lako ni dogo tu ni kuniuliza kuhusu ndege, kwanza nikujibu ilikuwapo pale airport
ambayo ilikuwa imeshaagizwa na Bunge kupitia Bima yaAfya, ilikuwa stand bye
kumchukua mgonjwa huyu, kumpeleka Muhimbili, sasa kilichotokelezea, wenyewe walivyoamua
huyu mgonjwa lazima aende Nairobi, ndege ile ilikuwa haina kibali cha kwenda Nairobi,
ili uende Nairobi inabidi uwe na marubani wawili, bahati nzuri spika(Job Ndugai)
alihangaika kuipatia kibali, iweze kumchukua kumpeleka Nairobi yule mgonjwa. Kilichotokelezea,
rubani akasema kuna kitu kinaitwa Landing Instrument ndege hii haina kwa kule
Nairobi, kwa hiyo haitoweza kuruka, hapo tukaingia katika dilemma tunafanyaje
katika hali kama hiyo? Kwa hivyo mimi nikatumia uwezo niliyojaliwa
na Mungu, nikatafuta ndege kwa Flight
link, kwa ndugu zetu tunaofanya nao biashara sana,wakatoa bei za juu sana
lakini kwa kuwa tunafahamiana, wakatoa bei hizo watakusaidia kwa dola 9200
pamoja na ambulace, kwa hiyo ile ndege mimi ndiye niliyeiita kwa
kukubaliana na mwenyekiti wa CHADEMA,
Bwana Mbowe na Bwana Msingwa wakisema, ‘Turky ! haya mambo yasimamie,
sisi baadaye tutakuja kuyasatled’ na ndicho kilichotokelezea, kwa hiyo wao
walipofika kule, siku ya pili ilibidi warekebishe mambo yale, lakini walipofika
kule hawakuweza, siku ya tatu imepita, Jumanne imepita , Jumatano jana imepita
naona leo Bungeni watu wameanza kuzungumza, na nafikiri katika taarifa ya Spika
(Job Ndugai ) alizungumza, ‘Bwana Turky alitoa pesa hizo na CHADEMA watalipa.’
Hii ni kauli ambayo haina matatizo kwa sababu kama CHADEMA wasingelipa mpaka
leo, lazima mimi ningetoa pesa zangu, niwalipe kwa sababu wale mabwana
wangekuwa wameshapitiliza zile siku, siku zingeshakuwa nyingi. Kwa bahati nzuri
mchana huu wa leo, saa sita na nusu, nimempigia mwenye ndege, akasema ‘CHADEMA
wamekwenda kumlipa.’ Kwa bahati mbaya siku ile ndege isingeweza kuruka kama
zisingeweza kupata dola 9000, maana lazima pesa zile ulipe ndipo ndege ile
iruke na hapo Dodoma hakuna hata mmoja ambaye alikuwa na dola 1000,
ilikuwa kidogo, hali ngumu! Lakini tunamshukuru mwenyezi Mungu. Kwenye
Nia njema Mungu hufungua Milango Yake.”
Mwanakwetu Upo?
Mwanakwetu hayo ni maelezo ya mhe. Salim
Turky aliyekuwa mbunge wa CCM, aliyefanya kitendo cha utu kwa mbunge CHADEMA,
mbunge wa upinzani. Utu , uungwana wa hali ya juu na funzo kwa walio wengi; watu
wa kawaida na viongozi wetu. Funzo hilo ndiyo limekuwa hamira kwa Mwanakwetu
kuandika matini haya leo hii likichochewa na mjadala wa kundi lile la Songwe.
Mwanakwetu anasema kuwa linapotokea
tukio lolote kwa mwanadamu mwenzako, wewe kama mwanadamu uliye kando unatakiwa
kuokoa jahazi kamaaliyofanya mhe Turky ambaye nayeye leo ni marehemu.
Msomaji wnagu yakumbuke maneno ya mhe
Turky kuwa Kwenye Nia Njema Mungu Hufungua Milango Yake.Msomaji wangu tena na
tena kumbuka Septemba 15, 2023 itatimia miaka mitatu tangu alipofariki dunia
mhe Salim Turky, aliyekuwa mbunge wa MPENDAE. Staki kuweka neno linguine lakini
Kwenye
Nia njema Mungu hufungua Milango Yake.
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment