Adeladius Makwega –MWANZA
Mwanakwetu alifika katika eneo kilipo Chuo Cha Maendeleo ya
Michezo Malya, Kwimba- Mkoani Mwanza mwishoni mwa Aprili 2023, alipokanyaga
katika mandhari ya chuo hiki alikaribishwa na sauti la ndege waliokuwa wakipiga
kelele sana katika mti iliyokuwa mingi katika eneo hilo lenye viwanja kadhaa
vya michezo, madarasa na ukumbi mkubwa wa michezo mbalimbali.
Mwanakwetu katika shajara yake ya mwaka 2021 anakumbuka aliwahi
kufika Malya akiambatana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo wakati huo mhe Pauline Gekul.Shajara ya Mwanakwetu inaeleza kuwa
safari hiyo ilikuwa ngumu sana maana gari alilopanda Mwanakwetu la Serikali injini
yake ilifia njiani wakielekea Malya, huku wakifika hapo na kurudi Dodoma kwa
gari la hisani.
Sasa Mwanakwetu yu Malya mara ya pili. Akiwa anazunguka katika
viunga vya eneo hilo alikutana na kijana mmoja, mwembamba , mrefu na mweupe.
“Kaka samahani, Shikamoo! Wewe ni Kazimbaya Makwega? Kama ninakufananisha!
Samahani sana kwa kuuchukua muda wako, mimi ninaitwa mwalimu Hamza Jafari, mwalimu
wa Shule ya Msingi Ubiri iliyoyopo katika Halmashauri ya Lushoto Mkoani Tanga, nipo
hapa chuoni ninasoma Stashahada ya Michezo, mwaka wa pili na wa mwisho.”
Hapo Mwanakwetu kasimama
anayasikiliza maelezo hayo na kweli
Mungu bahati Mwanakwetu alimkumbuka mwalimu Hamza Jafari vizuri, wakayazungumza
mengi, huku Mwanakwetu akimuuliza mwalimu Hamza Jafari aliwezeje kufika Chuo cha
Maendelea ya Michezo Malya kilichopo umbali mrefu na Halmashauri ya Lushoto?
Mwalimu Hamza alimjibu,
“Kuna mwalimu anaitwa Secilia Ngovu, Unamkumbuka?
ninayefundisha naye shule moja pale pale Ubiri, aliwahi kusoma hapa Malya miaka
ya nyuma, aliponiambia juu ya chuo hiki nikavutiwa, nilitambua nina elimu ya
cheti cha ualimu na nina alama za ufaulu wa kidato cha nne na nina alama za
ufaulu nzuri za kidato cha sita, hivyo nikawa na sifa za kujiunga na Stashahada,
nikakata shauri, baada ya taarifa hiyo nikafika hapa, nikajiunga na chuo hiki
ndiyo maana tumekutana.”
Msomaji wangu hiyo ilikuwa ni siku ya
kwanza ya Mwanakwetu akiwa hapa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya, huyu mwalimu
Hamza Jafari alifahamiana na Mwanakwetu kwa mara ya kwanza mwaka 2016 huku
Lushoto Tanga, miaka nane iliyopita.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu
alikaribishwa na milio ya ndege juu ya mti, kwa kuwa mwalimu Jafari Hamza yeye
alikuwa mwenyeji hapa Malya zaidi ya Mwanakwetu, Mwanakwetu akamuuliza juu ya
ndege hawa waliokuwa wakipiga kelele.
Mwalimu Hamza alimtafuta binti mmoja
wa Kisukuma anayefahamika kama Neema Masunzu ambaye alicheka sana pale alipoulizwa
juu ya ndege hao, alafu akasema,
“Hao hawa ndege ni jamii ya Flamingo, huku tunawaitwa Kimelanzoka
maana wanakula sana nyoka na wanapenda kukaa katika miti inayofahamika kama
Msina, humu juu yake hujenga matundi yao na hizo kelele juu ni zao na mkinda
yao.”
Hapo Mwanakwetu ni kuku mgeni,
akasikiliza vizuri maelezo hayo Neema Msunzu akaongeza kuwa,
“Ndege hawa huwa wanafika katika eneo jirani na Chuo cha Malya
na maeneo mengine, yenye miti mingi ya Msina mwezi wa 4 na 5 na hukaa hapo na
kutaga mayai hadi kutotoa watoto wao wakiwa wakubwa mwezi wa 9 na 10 ambapo
mvua zikianza kunyesha huwa wanaondoka kuelekea maeneo ambayo hayana mvua kama sana
wakati huo kama vile Morogoro, miezi hiyo hapa Malya huwa hawaonekani tena hadi
mwezi 4 wa mwaka mwingine.”
Mwanakwetu hiyo ni siku ya kwanza
hapa Malya, alifika kwa wakubwa wa Chuo hiki na kukutana na Makamu Mkuu wa Chuo
ndugu Alex Mkenyenge na baadaye akapelekwa kwa Mkuu wa Chuo ndugu Richard
Mganga ambaye alimueleza Mwanakwetu haya,
“Karibu sana Malya Mwanakwetu, hapa tupo, tunachapa kazi,
tunaijenga Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapa tunatoa kozi mbalimbali kama
vile; Stashahada ya Elimu ya Uongozi na Utawala katika Michezo (Ordinary Diploma
in Sports Development & Adrminstration), Stashahada ya Ufundishaji Michezo (Ordinary
Dipoloma in Sports Coartching Education), Stshahada ya Elimu ya
Michezo(Ordinary Diploma in Physical Education & Sports na Kozi ya Astashahada
ya Elimu ya Michezo kwa Wanamichezo (Basic Techinician in Certificate in Physical
Education and Sports).”
Mwanakwetu yu Chuo cha Maendeleo ya
Michezo Malya, sasa ana marafiki watatu; wakazi wa Malya , wakufunzi, watumishi
wa chuo hiki, Wanachuo wanaosoma chuo hiki na ndege hawa Kilimanzoka ambao walikuwa wa kwanza wa kumuimbia wimbo wa ukaribisho
alipofika Malya.
Mwanakwetu akapata marafiki wengi
kama alivyokudokeza mmojawapo ni Faraja Msigwa huyu ni mzaliwa wa Pwani lakini
kwa asili yeye ni Mhehe wa Iringa jirani na Lilinga Ngome ya Chifu Mkwawa, yeye
ni mtumishi wa umma huko Mkoani Kagera, kwa kuwa Mwanakwetu anamfahamu Binti
Msigwa miaka mingi akamuuiliza haya ulifikaje huku ?
“Mimi nilikuwa na rafiki yangu tunafanya nae kazi huko huko
Kagera, alinieleza na mimi nikaingia katika mtandao ya kijamii nikachukua fomu
na kuijaza na ndiyo mama sasa ninasoma hapa. Maana nina cheti cha ualimu kwa
hiyo sifa hiyo ninayo na nitasoma hapa hadi nikapomaliza Stashahada yangu,
alafu nitajiunga na Chuo Kikuu.”
Mwanakwetu pia alipata marafiki zake wengine
watatu Grace Mpokonya, Elias Mashenzi na Mohamed Mussa, kumbuka hawa ndugu
anawafahamu miaka mingi .
Mohamed Mussa yeye anatokea mkoani
Dodoma
“Mimi nimeshamaliza mitihani yangu, hapa nipo njiani kuelekea
Dodoma Makao Makuu ya nchi, sisi tumekaa miaka mingi tangu 2021, nimeshapata
ujuzi wangu mkubwa wa michezo na kiu
yangu ilikuwa kuufahamu, kuucheza na kuufundshia mchezo wa mpira wa kikapu, kwa
hiyo ninarudi Dodoma kazini. nitaendelea kujituma na kufuata taratibu zote ili niweze kuwa mahiri zaidi
katika mchezo huo kuufundisha ndani na nje ya Tanzania.”
Msomaji wangu upo?
Rafiki kadhaa wa Mwanakwetu sasa
wanaondoka, Mohammed Musa anarudi Dodoma kamaliza masomo yake , Hamza Jafari
anarudi Lushoto kamaliza masomo yake , Grace Mpokonya anakwenda zake Rukwa
likizo, naye Elias Mashenzi anakwenda zake Geita likizo lakini huyu na Faraja
Msigwa anakwenda zake Kagera likizo.
Mwanakwetu anabaki na rafiki zake Kimelanzoka
pekee ambapo ameambiwa mwezi wa 9-10 na wao watakuwa wanaondoka kuelekea maeneo
yasiyo na mvua. Mwanakwetu anapata matumaini ya kutokuwa mpekwe maana mwezi wa
8 na 9 Kimelanzoka watakuwa angani hadi hawa rafiki zake ambao hawajamaliza
chuo watakaporudi akiwamo Elias Mashenzi, Grace Mpokonya na Faraja Msigwa.
Msomaji wangu Mwanakwetu siyo mpekwe,
yeye sasa na Kimelanzoka jamii ya Korongo, katika kipindi hicho anatoa ahadi
kwako msomaji wake kuwa atakusimulia simulizi nyingi za rafiki zake hao watatu hapa Chuo Cha Maendeleo
ya Michezo Malya umbali wa KM 100 kutoka Mwanza mjini.
Mwanakwetu Upo?
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment