Adeladius Makwega-MWANZA
Septemba 25, 2022 ambapo inakaribia mwaka mmoja uliyopita, ndugu yetu Mwanakwetu aliyaandika makala haya, leo anayarudia kwa hisani yako msomaji wake.
Mwaka 2014 aliajiriwa kama Afisa Mtendaji katika Halmashauri ya Mbozi, wakati huo ikiwa ni wilaya ya mkoa wa Mbeya, lakini baadae wilaya ya Mbozi ikawa ndiyo makao makuu ya mkoa mpya wa Songwe, wakati huo ukiongozwa na mheshimiwa Chiku Galawa, kwa maoni Mwanakwetu anayoendelea kukusanya kutoka Songwe bado rekodi ya utendaji wa kazi Bi Chiku Galawa haijavunjwa..
Mtendaji huyu alifanya kazi katika kata kadhaa zikiwamo Vwawa, Hasanga na Hasamba katika vipindi tofauti. Utaratibu wa Halmashauri ya Mbozi wakati huo, madiwani, baadhi ya watumishi wa wilaya hii na viongozi wakuu kiwilaya walikuwa wakizunguka katika kata hizo kupokea kero za wananchi, hilo kwa uhakika lilikuwa jambo zuri .
Ndani yake baadhi ya viongozi wakitumia vikao hivyo kuwa mwiba wa kuwachoma, kuwajeruhi na kuwapunguza kasi baadhi ya watumishi wa umma waliokuwa na moyo thabiti, wakipinga baadhi ya tabia za baadhi ya wanasiasa na viongozi wasio na nia na tabia njema.
Katika kata moja kulikuwa na walimu, wauguzi, matabibu, maafisa kilimo, maafisa mifugo na watendaji wa vijiji na kata, huku kiongozi mkubwa wa siasa kwa kata ni diwani na mara moja moja wabunge walipita huko.
Mtendaji huyu wa kata alihimiza shughuli kadhaa za maendeleo katika kata hizo za Hasanga, Vwawa na Hasamba na wakati huo kumbuka hapo Songwe ni mkoa mpya na kata hizo ni kata zilizo hatua chache na makao makuu ya Halmashauri, Wilaya ya Mbozi na mkoa wa Songwe.
Msomaji wangu kumbuka sana ili mkoa upate maendeleo unahitaji viongozi wenye juhudi sana,wabunifu, siyo viongozi wa kuziba nafasi tu. Miongoni mwa shughuli alizohimiza Mtendaji huyu ilikuwa ni ujenzi wa zahanati ya eneo la Old Vwawa, malengo yalikuwa siyo vizuri Hospitali ya Wilaya ikapokea hata wagonjwa wenye matatizo madogo madogo, ni vizuri wagonjwa hao kupata huduma kutoka zahanati na ndiyo waende kituo cha afya, hospitali ya wilaya, mkoa au rufaa. Huo ndiyo utaratibu wa Kiserikali katika tiba Tanzania.
“Japokuwa mgonjwa akienda moja kwa moja hospitali ya juu hawezi
kufukuzwa, anapewa huduma huku akielezwa utaratibu huu.”
Pale inaposhindikana au
kutokufanya hivyo ni kuzibebesha mizigo hospitali ya juu na maelekezo yaliyotolewa
kuwa ni wajibu kila mgonjwa kuanza kupata huduma kutoka katika zahanati. Kwa
hiyo wakazi wa Old Vwawa waliwajibika kujenga zahanati yao, kinyume chake
waliwajibika kutibiwa katika zahanati ya Mlowo na maeneo mengine, huku wakiiona
Hospitali yaWilaya ile ambayo baadaye ilichukuliwa na mkoa wa Songwe kwa muda.
Mtendaji huyu alihimiza ujenzi huo kwa kukusanya matofali, mawe, vifaa kadhaa na pesa taslimu na ujenzi huo kuanza mara moja. Kwa kuwa wakati huo serikali ilikuwa ikihimiza ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kieletroniki jambo hilo lilisaidia kila mtendaji wa kata na vijiji kuwa na mashine ya kukusanyia mapato ya halmashauri husika vizuri sana.
Utaratibu wa kukusanya mapato kupitia mashine ulisadia mno pesa za serikali kuingia moja kwa moja katika mifumo ya kibenki, huku jambo hilo la watendaji wa vijiji na kata kusimamia mapato likikumbwa na changamoto kadhaa. Baadhi ya wanasiasa walitamani mashine hizo kupatiwa watu wanaowaweza na kuwataka wao kwa manufaa yao.
Kumbuka utaratibu wa viongozi wa wilaya kuzunguka katika kila kata uliendelea kama kawaida na siku wakafika katika kata aliyekuwepo mtendaji huyu na kukuta ujenzi wa zahanati ukiendelea vizuri kabisa, walipouliza baadhi ya wanasiasa juu ya ujenzi wa zahanati hiyo walisema kuwa hawafahamu lolote juu ya ujenzi huo wa zahabati hii ya Old Vwawa.
Maamuzi yaliamuliwa mtendaji huyo apokonywe mashine ya kukusanyiwa mapato na kuwekwa kolokoloni muda huo huo mbele ya wananchi na watumishi wa kata hii aliyokuwa akiiongoza.
Polisi hawakuwa na shida yoyote
wao walipokea maelekezo tu kutoka kwa waheshimiwa sana walikuwapo katika
mkutano huo wa hadhara.Mtendaji huyu alipata msukosuko mkubwa kwa sababu
mbalimbali, kwanza hulka yake ya kujiamini, pili jinsia yake ya kike huku baadhi
ya wanasiasa wakishangazwa na tabia hii ya mwanamke kujiamini mno mbele ya
wanaume.
Wakati haya yanafanyika Mwanakwetu hakuwepo lakini haya aliyakuta yakiendelea mwisho mwisho, alipochunguza mwisho wa siku mtendaji huyu hakuwa na kosa lolote lile. Alirudi kazini bila ya kukata tamaa, huku akihimiza wanakijiji wa Old Vwawa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ambapo Mwanakwetu alikutana na mtendaji huyo uso kwa uso huko huko Old Vwawa.
Kwa hakika wananchi wa Mbozi na mkoa mzima wa Songwe ni wapenda mno maendeleo, japokuwa changamoto ni siasa za baadhi ya viongozi wa eneo hilo, mtendaji huyo alipata ushirikiano na kukamilisha zahanati hiyo, lakini haikuwa hekima kubakizwa kufanya kazi eneo hilo na alihamishiwa kata ya Hasamba.
Akiwa Hasamba mtendaji huyu alifanya kazi nzuri sana ya kukusanya mapato kwa kuwa kata hii ilikuwa hodari wa kutengeneza matofali mazuri ya kuchoma yaliyonunuliwa kila kona hadi Tunduma na Mbeya hivyo mapato mengi yalipatikana kutokana na chanzo hicho kilichosimamiwa vema na mtendaji huyu.
Baadaye Mwanakwetu alibaini kuwa
“Wengi waliompinga mtendaji huyu hodari, walichukizwa na uhodari
wake wa kazi, kujiamini kwake na shida ya walio wengi wanadhana kuwa mtumishi
wa umma mwenye cheo kidogo ana anawajibu wa kuitikia ndiyo katika kila jambo
kutoka kwa mkubwa.”
Je hiyo ni kweli?
“Kwa hakika mtumishi wa umma anapaswa kuwa mtii kwa mambo ya msingi, lakini siyo utii kwa udhalimu na uovu. Kwa kupinga udhalimu na uovu kunaweza kuhatarisha nafasi yake, ajira yake na hata uhai wake lakini heri ya usalama wa roho kuliko kuwa na usalama wa mwili. Utendaji kazi wa mtendaji huyu wa kata unadhihirishwa hata sasa kwa kuwa zahanati ya Old Vwawa sasa inatoa huduma ya tiba kwa wakazi wa eneo hilo ikiwa na watumsihi kadhaa na kuwapa nafasi ya kupata huduma ndogo ndogo hapo hapo .”
Mwanakwetu anatambua baadhi wakazi wapya wa Old Vwawa wanaweza wasimkumbuke mtendaji huyu, lakini wanapokwenda kupata huduma katika zahanati hiyo wanapaswa kumkumbuka mtendaji huyu anayesimuliwa katika matini haya.
Tukio hilo la kumsumbia mtendaji huyu linatokea mhe. Chiku Galawa alishaondoka Songwe, mtendaji huyu akaamua kuhamia Dodoma, barua yake ilipitishwa na Mwanakwetu, maana watu wanaweza kukutafuta kazini alafu wakahamia mitaani, mtendaji huyu akaahamia Wilaya ya Chamwino.
Mwanakwetu maisha yanasonga na hayarudi nyuma, mwaka 2020 mtendaji huyu wa kata ya aligombea ubunge wa viti maalumu kupitia CCM katika mkoa wa Geita na kushinda kwa kura nyingi. Hapo sasa Mwanakwetu yupo Dodoma, usiku mmoja mwishoni mwishoni mwa mwaka 2020 akapigiwa simu na mama mmoja.
“Shikamoo, mimi naitwa Rose Vicent , za siku , unaendeleaje ? Familia
yako haijambo ?cMkuu sipo Dodoma, siku hizi mimi ni mbunge wa Viti maalumu CCM
mkoa wa Geita. Nilipohamia Dodoma nilienda nyumbani kugombea ubunge sasa ni mbunge, umenikumbuka mkuu? ”
Kweli Mwanakwetu alimkumbuka sana, akampa pongezi mhe. Rose Vicent sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Msomaji wangu maisha ni safari ndefu. Mwanakwetu anakwambia msomaji wake kuwa mhe Rose Vicent ni,
“Mwanamke hodari, mchapakazi, anayejiamini, anayefahamu
analolifanya, siye wa kuitikia ndiyo kwa kila jambo, mwenye kuheshimu ndoa yake
na mwanasiasa makini.”
Mwanakwetu Upo?
Mwanakwetu anakuuma sikio
msomaji wake kuwa waliyompiga mizengwa mhe. Rose Vicent leo hii Julai 30, 2023
hakuna hata hata mmoja aliyebaki katika ulingo wa siasa wala utumishi.
Sikuitishi msomaji wangu bali huo ndiyo ukweli. Ndugu hao wote Mungu amewajalia
uhai, Mwanakwetu anaamini kuwa wanafuatilia michango yake Bungeni katika hoja
mbalimbali.
Michango ya mhe Rose Vicent wataiona sana, mwenzao Mwanakwetu anapigiwa simu na sana mheshimiwa huyu, hata namba yake anayo hata sasa.
Mwanakwetu yupo Mwanza, Mwanza na Geita ni jirani, Mwanakwetu anajiuliza hivi kama ningemfanyia ubaya huyu mama ingekuwaje , unajificha wapi? Mwanakwetu atakwenda Geita kwa mhe Rose Vicent kumsalimia na akatembelee na kaburi la marehemu Dkt. John Pombe Magufuli.
Mwanakwetu anasema ,
“Mwenzenu anapigiwa Simu na Mheshimiwa
Mbunge.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment