Adeladius Makwega-MWANZA
Wakristo wameambiwa kuwa neno la Mungu katika Jumapili ya 17
ya Mwaka A wa Liturjia ya Kanisa linasisitiza kuupa thamani ufalme wa Mungu,
kama kitu cha kwanza katika maisha ya mwanadamu.
Hayo yamehubiriwa na Padri Alex Maya Julai 30, 2023,
anayefanya utume wake katika Parokia ya Ihalu, ambapo alisalisha misa hiyo
katika Kanisa la Bikira Maria, Malkia wa Wamisionari, Parokia ya Malya, Jimbo
Kuu Katoliki la Mwanza.
“Ufalme wa Mungu unafanana na Kokolo, ambalo kazi yake ni
kuvua samaki wa kila aina, hata hapa dunia wapo watu wa kila aina, wasengenyaji,
wazinzi, waongo, wapo wabishi, wote hao wameandaliwa kuutafuta Ufalne wa Mungu,
Mungu anatupatia mvua ulimwegu mzima, wenye wema na wabaya na hata dhambi zetu
hazionekani, je kama tungekuwa na kioo cha kuonesha dhambi zetu ingekuwaje? Mtu
ukipita watu wangeona dhambi zako. Jamani tutambue kuwa sote tumeitwa katika Ufalme
wa Mungu. Kwa mfanio wa kokolo, Je wewe ni samaki wa aina gani? Sato, Sangara au
wewe ni Kamabale? Samaki Kambale kuanzia baba, mama na watoto wote wana ndevu.”
Padri Maya alisema kuwa Mtume Paulo alivyoandika kwa Warumi
alisema kuwa Mungu anafanya kazi na wale wampendao, wale walioitwa kwa kusudi
lake, mimi na wewe tumeitwa kwa kusudi na Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kuwa neno la Mungu linasema,
“Siyo sisi tuliyomchagua, bali yeye ndiye alituchagua sisi,
kama umechaguliwa na Mungu, je unaitambua thamani hiyo ya kuchaguliwa ? Katika
azimisho la misa hii, tuombe Mungu atusaidie kila muumini atambue thamani ya Ufalme
wa Mbinguni katika maisha yake, Ufalme wa Mbinguni ndiyo kitu cha kwanza na
Mungu ndiye anapaswa kuwa kipao mbele cha maisha ya kila mwanadamu.”
Misa hiyo pia ilikuwa na nia na maombi kadhaa ikiwamo kuwaombea
marehemu .
Tamati ya misa hiyo kulifanyika mchango kwa kumtegemeza mwalimu
wa kwaya ambapo katika misa ya kwanza zilipatikana shilingi laki nne na ushehe.
Hadi misa hiyo ya kwanza iliyoanza saa kumi na mbili ya asubuhi
inakamilika, hali ya hewa ya eneo la Malya na viunga vyake limekuwa na baridi kali
wakati wa usiku na asubuhi, huku mchana jua kali likiwaka, nayo hali ya kijani
kibichi imepotea, miti mikubwa ikipukutisha majani yake, huku miti michache
inayostahamili ukame pekee ikibakiza majani yake mabichi yasiyo na chanikiwiti.
Post a Comment