Adeladius Makwega-MWANZA
Vijana wametakiwa kuwa wachapakazi, kazi iwe sehemu ya maisha
yao, kupenda kuwajibika na huko kutasaidia kuweza kupata mahitaji yao yote ya
kila siku kwa haki.
Hayo yamesemwa na Padri Samson Masanja, Paroko wa Parokia ya
Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza katika Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari,
ndani ya azimisho la misa ya somo ya Jumuiya ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi,
Julai 29, 2023.
“Mungu alifanya kazi kutoka siku ya kwanza hadi siku ya sita,
akifanya uumbaji, hata tendo la uumbaji wa mtu mme na mtu mke kwa sura na mfano
wake, hilo ni tendo la kufanya kazi, tujifunze katika kufanya kazi ambayo ni
heshima, Mtakatifu Yosefu ni yule anayatoka katika ukoo wa Daudi, ni yule
aliyemposa Bikira Mariamu, tunatakiwa kufanya kazi kama alivyokuwa mtakatifu
huyu ambaye ni somo wa jumuiya yenu.”
Padri Masanja alisema kuwa Yosefu alimtunza Bikira Mariamu na
Yesu kwa nguvu zake zote na kwa jasho lake lote bila ya kuchoka , hata Yesu
alitambuliwa na jamii yake kama ni mwana wa seremala , kazi ya baba wa Yesu ilitambuliwa
vizuri, kazi ya Useremala ilitumika kuitunza familia yake.
“Nawaombeni mtambue kuwa kazi mnazofanya ziwe na heshima
katika jamii unayoishi, usikubali mtu yoyote haidharau kazi yako au kuikejeri,
kazi ni kitu kizuri. Je sisi ni wakereketwa wa kufanya kazi? Sisi ni Wakereketwa wa kuipenda kazi ? Muepuke
kupiga soga ambao ni uvivu, huo uvivu unaweza kuwapeleka kuwa wezi na ombaomba.”
Katika misa hiyo pia kulikuwa na nia kadhaa ikiwamo kuombea wahitimu
kadhaa wa mafunzo mbalimbali Chuoni Malya, huku viongozi kadhaa wa Jumuiya ya
Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi wakila kiapo.
Akizungumza mwishoni mwa misa hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi mwalimu Denis Kayombo alimshukuru Padri Masanja kwa
kusalisha misa hiyo huku akinukuu maneno haya,
“Mungu alituumba bila ya matakwa yetu , lakini hatuwezi kufika
kwake bila ya kuonesha ushirikiano.”
Hiyo ikiwa ni tafakari ya Mtakatifu
Agustino inayosistiza kila mmoja kutekeleza wajibu wake pahala alipo.
Post a Comment