Mwishoni
mwa mwaka 2009 Mwanakwetu alikuwa akiishi nyumbani kwao Mbagala Dar es Salaam
na wakati huo akiwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kama
Mtayarishaji Vipindi vya Redio, siku iliyotagulia aliingia kazini zamu ya saa 4
usiku na kutoka saa 11 ya alfajiri na kurudi nyumbani kwao Mbagala.
Desturi
ya zamu za usiku, ukirudi nyumbani unalala kidogo alafu kukicha unaamkia kufanya shughuli za hapa na pale.
Mwanakwetu
siku hiyo kazi yake na mwisho ilikuwa ni kuwalisha wanyama wake ikiwamo kuku,
bata na kanga alafu akatoka hapo nyumbani na kuelekea Mbagala Sabasaba, kuna
kijiwe kinachoitwa kwa Gervasi kijiwe hicho ni kwa fundi viatu ambapo tangu
miaka ya 1980 alikuwepo fundi viatu anayeitwa Mirusu ambaye alishiriki vita vya
Kagera kama Mgambo, umri wake ulipokwisha akawa fundi viatu na mwishoni mwa
1999 alihamia shambani kwake huko Kisere akawa mkulima, huyu fundi wa zamani ndugu
Mirusu ni Mndengereko wa asili ya Mbagala ambaye alisoma na Baba wa Mwanakwetu
shule ya msingi.
Hapo
Mwanakwetu anakwenda kushinda katika kijiwe cha baba yake mdogo(MIRUSU),baada
ya Miruso kwenda shambani, kijana wa
Kimbugu Gervasi akarithi hiyo mikoba , akawa anafanya biashara zake hapo.
Mwanakwetu
anashinda hapo mara nyingi tangu akiwa mdogo maana hapo kuna hadithi nyingi sana
likiwa eneo jirani na Mbagala Kimicha.
Siku
hiyo alipofika alikuta jamaa zake wengi wakiwa katika taharuki kubwa wakisema,
“Afadhali
Mwalimu Makwega umefika, siku hizi hauonekani sana, maana tangu uoe binti wa
Kimbugu/Kisambaa Dada yake Gervasi umekuwa mbali na sisi.”
Kumbuka msomaji wangu hawa jamaa wanamfahamu
Mwanakwetu kitambo tangu akiwa mdogo,kijana , mwalimu sasa ni Mtanganzaji wa
RTD lakini ualimu bado ulikuwa umemvaa Mwanakwetu, Kumbuka hata Mtangazaji na
Mwanahabari ni walimu wa umma, hivyo Mwanakwetu hadi sasa ni mwalimu wa umma.
“Sasa
Mwalimu Makwega hapa kapita askari wa JWTZ, kamchukua jamaa kisa amevaa kaptura yenye
mabaka mabaka , tumeongea naye hajatuelewa, tunakuomba tusaidie, yule yule, yule
pale anaondoka naye pengine anaelekea naye Mbagala Maturubai(Polisi), tunakuomba Mwalimu
okoa jahazi, kamuombee msamaha.”
Eneo hilo wakati huo kulikuwa na madereva na
daladala wengi wakishuka hapo, wanapumzika na kula chakula kwa mama mmoja mama
ntilie, huku daladala hizo wanapewa madereva wa dei waka(day work). Wakati
madereva walidamka na mabasi hayo alfajiri wakipumzika.
Mwanakwetu akawauliza,
“Huyo
kijana mnamfahamu?”
Wakajibu kuwa hata wewe unamafahamu. Mwanakwetu
akauliza swali lingine ,
“Siyo
mharifu?”
Wakamjibu ndiyo, Mwanakwetu akauliza swali
tena,
“Hiyo
kaptura aliitoa wapi?”
Jamaa mmoja anayeitwa Msofe , akiwa pia ni dereva
daladala na Mpare wa Same akajibu,
“Kaka
alikwenda kuipointi Tandika Mitumbani .”
Mwanakwetu akakumbuka akilini mwake ni kweli
hizo nguo zinauzwa katika mitumba, zinapoingia wauzaji hawataki hasara wanazipeleka
sokoni na wadau wananunua, maana wako baadhi ya watu walipokuwa wadogo waliulizwa
swali hili shuleni
“What are you going to be?“
Walijibu
“I shall be Soldier.”
Maisha
yanavyokwenda na ndoto hizo hawazifikii kwa hiyo wanasikia fahari sana kuzivaa
nguo hizo tu na si waharifu.
Mwanakwetu na Msofe wakaelekea huko alipoelekea
askari na kijana huyo. Walipofika katika makazi ya mhe.Ramadhani Abdallah Zame
ambaye awali aliikuwa Naibu Meya na baadaye akawa Meya wa Jiji la Dar es Salaam
baada ya Kitwana Kondo (KK)Kushindwa kesi mahakamani na huyu Mwenyekiti wa CCM Dar
es Salaam sasa Abbasi Mtemvu(Haya msomaji
wangu nakwambia tu haya kwa hisani ya Shajara ya Mwanakwetu).
Hapa kwa Mhe. Zame pana Msikiti wa miaka mingi sana unaofahamika kama Masjidi Zame.
Mwanakwetuu akasema,
“Afande
samahani, huyu ni kijana wetu, tunaungama mbele yako amefanya kosa kubwa kwa
mujibu wa sheria, huyu kijana ni dereva wa daladala za Rangitatu-Kariakoo ,
hawa ni wadogo zangu, siyo waharifu, nakuomba msamaha kwako na kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kosa alillolifanya.”
Afande wa JWTZ muungwana sana akasema mbona
unamuombea wewe msamaha yeye hana mdomo? Kijana huyu dereva wa daladala akaomba
msamaha, askari huyu akaupokea msamaha huo na kusema haya,
“Mimi
ninamsamehee, siku nyingine asinunue nguo zenye mabaka mabaka kama haya ni kosa,
maana hizi ni mali ya JWTZ na mtu yoyote harusiwi kuivaa, sasa hii nguo kwa
kuwa nimeikamata hawezi kuondoka nayo, fanyeni utaratibu hii nguo nibaki nayo.”
Kwa kuwa eneo hilo lote Mwanakwetu ni mwenyeji
akaingia nyumbani kwa mhe Zame(Meya wa
Jiji la Dar es Salaam Mstaafu) akawasalimia shikamoni yeye na mkewe Zuweni
Binti Huruga
“Haya
mkina Makwega! Vipi kwangu kulikoni? Maana rafiki yako hayupo Tanzania, eee
umekuja kusali katika msikiti wetu?”
Mwanakwetu akajibu na kueleza tukio hilo alafu
akaomba kaptura ili kijana huyu ajihifadhi.
Mke wa Mhe Zame yaani Zuwena Omari Binti
Huruga yeye anazaliwa Mbagala Sabasaba jirani na kina Mwanakwetu, huyu Binti
Huruga amesoma na Shangazi wa Mwanakwetu anayefahamika kama Otilia Makwega.
(Mhe.Zame Meya -wa Zamani wa Jiji la Dar es Salaam na Mkewe Binti Huruga.)
Hapa kwa Mhe Zame, Mwanakwetu yupo kwa
shangazi yake huyu Binti Huruga,mama
mheshimiwa, Mama mmoja mwembamba, mrefu, mweusi wa asili na mpole.
Mama mheshimiwa akaingia chumbani kwa vijana
wa kiume na kutoka na kanzu na kumpatia Mwanakwetu, naye kurudi mbele ya nyumba
hii ambapo wakati huo kulikuwa flemu za maduka nyingi.Kanzu ile alipewa kijana
huyu huku Meya wa Jiji wa zamani akitazama kwa mbali alafu afande akamsindikiza kijana huyu hadi katika choo cha Masjidi Zame na kijana huyu akavua
kaptura yenye mabakamabaka na kumpa askari na kuivaa kanzu hiyo ya hisani ya mhe Zame.
Watu wa Mbagala kwa Makuka wakawa wengi, huku
huyu Meya wa zamani anawasimulia kile kilichotokea baada ya kuambiwa na
Mwanakwetu. Askari wa JWTZ aliomba kibiriti, akapewa akaiwasha kaptura hii na
ilipoungua akaenda zake.
Mhe Zame ambaye sasa mzee sana akasema,
“Makwega
mwambie huyo ndugu yako asiirudishe hiyo kanzu.”
Mwanakwetu akamshukuru sana mhe Zame na kurudi
zao Mbagala Sabasaba, wakafika Kijiweni kwa Gervas wakawa wanamtania huyu
kijana aliyekamatwa,
“Leo
ungekiona cha moto, ungeenda kujaza karo la maji kwa kijiko cha chai sijui
ingekuwaje, na hata huyo bosi wako Baniani daladala lake angempa dereva
mwingine.”
Msomaji wangu kumbuka wadau hapo kando kijiweni wanacheka
sana.
Mwanakwetu upo?
Huyu kijana kwa kuwa alikuwa dereva wa
daladala, tangu siku hiyo Mwanakwetu alikuwa akipanda bure tu kila basi alilokuwa
akiendesha huyu kijana na mabasi ya madereva wengine walishuhudia tukio hilo.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Katika kisa hiki huyu kijana hata kama asinguruhusiwa
na askari huyu kwa hakika angepelekwa kituo cha Polisi Mbagala Maturubai na shauri
lingefunguliwa askari wa JWTZ angekuwa shahidi tu mbele ya mahakama. Hata nduguze
huyu kijana wangeenda kumtafuta hapo polisi ndugu yao na siyo kambi ya JWTZ .
Mwanakwetu anakubali kwa asilimia 100 kuwa uvaaji
wa nguo za kijeshi kwa mtu ambaye si askari ni kosa lakini analipiga chapuo
lake kwa sauti ya juu akikumbusha kuwa kuna nguo zinazoingia nchini kama
mitumba hivyo zinapaswa kudhibitiwa huko si kwa uraiani.
Pia Mwanakwetu anakumbusha majukumu ya msingi
ya JWTZ,
“Kulinda Katiba
na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi wa Mipaka ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Kufanya Mafunzo na Mazoezi ili kujiweka tayari Kivita
wakati wote, Kufundisha umma shughuli za Ulinzi wa Taifa, Kushirikiana na
Mamlaka za Kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa
maafa, Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) na Kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani Kimataifa.”
Hoja ya kukamata sare na nguo hizo libaki
mikononi mwa Jeshi la Polisi Tanzania na kufanya hivyo kunaepusha taharuki
katika jamiii, JWTZ wanaweza kutoa matamko kama nchi imeiingia katika hali ya
hatari na siyo masuala ya sare, haya yabaki kwa Jeshi Polisi Tanzania.
Mwanakwetu anaiweka chini kalamu yake
siku ya leo anakumbuka kuwa Watanzania tangu baada ya vita vya Kagera
vilinvyomtimua Nduli Idd Amini, Watanzania wenyewe waliamua kuwapa heshima
kubwa JWTZ ambapo katika mabasi ya daladala hawatozwi nauli kama ile ngekewa aliyopewa
Mwanakwetu na madereva wale wa daladala wakati ule, hii ni Heshima ya Watanzania.
0717649257
Post a Comment