SARE JWTZ JUKUMU LA JESHI LA POLISI


Adeladius Makwega MWANZA

Miaka ya 1990 Mwanakwetu alikiwa mwanafunzi wa shule ya Tambaza, palikuwa na basi ndogo moja kama Nissani ambayo ilikuwa inakuja shuleni hapo kila asubuhi, mchana na wakati mwingine jioni kuleta na kuwachukua wanafunzi fulani.

Basi hiyo ndani yake ilikuwa imejaa wanafunzi wa shule kadhaa za msingi na sekondari, jambo hili liliibua maswali mengi,

“Jamani hii basi ndogo inawaleta kina nani?”

 

Swali hili lilidumu kwa muda mfupi, baadaye ilibainika kuwa kuna watoto wa mkubwa fulani wa vyombo vya ulinzi wakati huo, huwa wanaletwa shuleni na pia katika shule zingine za msingi na sekondari na kurudishwa nyumbani.

Hilo lilibainika baada ya kuwaona wale waliokuwa wanasoma Tambaza wakishuka kila asubuhi katika basi hilo lililokuwa na rangi nyeupe. Wanafunzi wa Tambaza walikuwa wafuatiliaji sana wa mambo, walibaini kuwa kati ya wanafunzi hao ni watoto waliozaliwa kwa mama wengi na huku pia wakiwamo ndugu ambao walikuwa wakilelewa nyumbani kwa mkubwa huyo.

Kati ya watoto hawa, mtoto mkubwa alikuwa anasoma Tambaza na alikuwa mtundu mtundu, hasa hasa utundu wa ujana, huku akiwa na jina ambalo ni vigumu kumtambua kama ni mtoto wa mkubwa,Mwanakwetu yeye  binafsi hakufahamu kwanini jina lake hilo lilikuwa tofauti.

Kijana huyu alijulikana kwa vituko vyake ambavyo viliwasumbua kiasi walimu wa Tambaza. Huku kile kitendo cha wao kuletwa kila siku kwa basi hakukipenda, hapa aliona ananyimwa uhuru wake, vituko(pikiniki) vya wanafunzi wenzake wa Tambaza mitaani alivikosa kuviona mubashara bali aliambulia simulizi tu.

 

“Jana tulikuwa pikiniki Mwenge”

 

Alisimuliwa darasani.

 

Wasaidizi wa huyu mkubwa walifanya kazi nzuri sana na wakati mwingine kumfuata hadi darasani, huku wakiwa wakali mno. La msingi kwa kuwa baba yake alikuwa mkubwa na anafanya maamuzi makubwa, mahasidi wangeweza kumfanyia ubaya kijana wake, Mwanakwetu binafsi yake hilo alikubaliana nalo kabisa, lilikuwa jambo jema.

Wakati ule shuleni hapo walikuwa wanasoma hadi jumamosi, siku hii ikiwa pia ni ya kusafisha madarasa kwa ndani na kufuta vioo lakini ilikuwa nusu siku. Kila jumamosi ndugu huyu alikuwa anakuja na gari dogo binafsi ya nyumbani kwao, huku ikiwa ni siku ya kuwatembelea rafiki zake mbalimbali hadi majumbani. Hapo alikuwa huru hata aliwatembelea rafiki zake wa shule zingine ikiwamo Zanaki, Mwanakwetu kama ni kamba siku hiyo ilikuwa imekatika.

Kuna wakati ilitokea fujo iliyowahusisha wanafunzi kama 20 na kijana huyu alikuwepo, kwa hiyo jambo hili lilijadiliwa mno na maamuzi yalifikiwa kuwa kosa lao ni onyo la mwisho, fimbo sita na kila mmoja afike Tambaza na mzazi wake siku ya adhabu, saa mbili ya asubuhi na uwakilishi wa mtu mwingine ulikataliwa bali mzazi/mlezi tu.



Msomaji wangu siku hiyo ilifika na ofisi ya mkuu wa shule ya Tambaza mandhari yake ilikuwa hivi,

 

“Ukiingia tu mlangoni, mkono wa kushoto ni chumba cha ofisi ya mkuu wa shule na chumba cha mkono wa kulia ni ofisi ya makamu mkuu wa shule na katikati ilikuwa pahala pa karani na mhudumu.”

 

Shule hii haipo mbali sana na Bahari ya Hindi, siku hiyo upepo wa bahari hiyo ulivuma mno, nao mzizimo wake ukigonga kuta za shule hii aliyojenga H. H Aghakhan enzi hizo na kuilenga miili ya wanafunzi wengi wa Tambaza walikuwa na miili midogo myembamba lakini wenye umoja katika kila jambo.

Sasa wazazi wakawa wanafika wanaingia ofisini hapo, kila mzazi akiambatana na kijana wake, karani akawa analitaja jina mwanafunzi anaingia kwa mkuu wa shule.

 

“Karibu mzazi, mimi ni mwalimu Julius Mushi, mkuu wa shule ya Tambaza, tumekuita kwa kuwa mwanao ameonesha utovu wa nidhamu, kwa hiyo atachapa fimbo sita na litakuwa onyo la mwisho, akifanya kosa lolote atafukuzwa shule.”

 

Alisema mwalimu Mushi kwa lafudhi ya Kichaga.

Kazi hiyo ilikuwa nzito, kundi lilikuwa kubwa na wanafunzi hao wakiwa wamependeza mno ambaye alikuwa haogi siku hiyo alioga, ambaye alikuwa achani nywele, alichana na wale waliokuwa wamefumua mapindo ya kaptula zao siku hiyo zilipindwa kwa maana unaongozana na mzazi wako. Mandhari ya ndani na nje ofisi ilionekana wanafunzi waliovaa nadhifu mashati meupe, kaptura za polista rangi ya kijivu, soksi nyeusi na viatu vyeusi.

Kwa desturi ya shule hii ilikuwa ukimuona mwanafunzi wake amependeza sana, basi tambua huyo alikuwa ni wa kidato cha kwanza, kidato cha tano au kidato cha sita na pia mwanafunzi mwenye kesi ambao wameitwa katika vikao vya nidhamu.

Mwalimu Mushi alikuwa akiendelea kuzungumza na wazazi na wanafunzi hawa huku maneno yalikuwa yale yale, kilichokuwa kinabadilika ni muda na jina la mwanafunzi tu.

Gafla wanafunzi wakaona ugeni unaingia, jamaa waliingia wana nyeo vikubwa vikubwa, huku shule hii imezungukwa na hawa jamaa kila kona,

 

“Jamani mbona tupo chini ya ulinzi?”

 

Walijiuliza wanafunzi wa Tambaza huku wakichungulia madirishani. Lakini darasa lenye kesi hii, baadhi yao walibaki walipoona ugeni huo walijua kinachoendelea na hilo lilisambaa haraka likaleta utulivu kw adesturi wanafunzi wa Tambaza katika hali ya hatari wlaikuw wakiipiga sauti kama king’ora hiyo ikiwa ishara na wote watakusanyika kwenye tukio, siku hiyo King’ora hakikupigwa.

Pale pa karani palikuwa na nafasi ya kukaa wazazi wachache, kwa hiyo walipajaza vizuri , wengine wametoka Mbagala wamepiga barakashea zao, wengine baibui, wengine magauni na wengine mashati na salawili zao. Kwa kuwa sehemu hii ilikuwa ndogo wanafunzi wale wenye kesi walikaa nje. Karani alikuwa akiiita jina tu fulani Bin fulani anaitika anaongozana na baba/mama yake wanaingia ndani kwa mkuu shule.

Sasa msomaji wangu kumbuka kuna jamaa wameingia na sare zao na vyeo vyao, huyu jamaa mwenye vyeo kama akienda sehemu nje ya ofisi yake hiyo ni ziara, sasa hapo yupo Tambaza kwa wito wa mkuu wa shule, mwalimu Julius Mushi.

Karani wa mkuu wa shule akapatwa na bumbuwazi, mara akafungua mlango wa mkuu wa shule, ndani kuna mzazi. Karani huyu akasema

 

“Mkuu hapo nje kuna ugeni mkubwa kutoka kwa majirani zetu , je una taarifa?”

Mkuu wa Shule alijibu,

 

“Nini tena mbona hatuna taarifa,”

Mara alisimama kutoka katika kiti chake, akachungulia akamuona ndugu huyu akiwa ameongoza na mtoto wake.

 

“Karibu mkuu, karibu, karibuni sana.”

Alisema mwalimu Mushi,

 

“Nimekuja kuitikia wito, huyu ni kijana wangu, nimeambiwa analeta usumbufu shuleni,”

 

Mkuu shule akajibu ni kweli.(Huku wakiongea wamesimama .)

 

“Naomba jambo hili mlimalize mara moja.”

Aliambiwa mwalimu Mushi.

 

“Ukiendelea na usumbufu wako, nitakunyoosha.”

Aliambia mtoto wake.

 

“Mtanipa taarifa.”

 

Aliwaambia wale wasaidizi wake.

Mwanakwetu, zilipomalizika sentensi hizo tatu aligeuka, huku wasaidizi wakawa wanapiga saluti. taa- taaa, taa- taaaa akatoka nje na kuingia ndani ya gari kurudi ofisini kwake jirani na shule ya Tambaza.Kila mmoja alishangazwa na tukio hilo, si mkuu wa shule, si karani, si wazazi wale waliokuwapo hapo na hata wanafunzi wote wa Tambaza. Ni nina huyo, ahaa huyo ni fulani…ahaa ndiyo ahaa ndiyo walizungumza. Ule mpango wa kuingia mzazi mmoja mmoja ofisini uliishia hapo hapo.

 

“Jamani wazazi, watoto wenu wanashida, tumeshayamaliza, tunawaombeni mrudi nyumbani.”

 

Alisema mkuu wa shule huku akitetemeka.

 

Mwanakwetu hata zile fimbo sita, hawa vijana hawakuchapwa tena, kesi iliishia hapo hapo.

Kijana huyu alisoma na kumaliza salama shuleni Tambaza, sifahamu kwa sasa yupo wapi, lakini nina hakika simulizi hii itamuibua huko alipo.

Natambua msomaji wangu unajiuliza maswali kwa nini siku ya leo Mwanakwetu anakikumbuka kisa hiki kilichotokea miaka zaidi 30 iliyopita?

Mosi, Agosti 1, 2022 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwaapisha wakuu wa mkoa na makatibu tawala alisema jambo kwa mstari mdogo mno kwa wale waliokula kiapo baadhi yao wakiwa wanajeshi waliopandishwa ngazi kutoka ukuu wa wilaya hadi ukuu wa mkoa.

 

“Msivae kombati, hizo mtazivaa tena mkirudi jeshini.”

 

Kauli hii ina mantiki kubwa kwa jamii ya Tanzania, ebu fikiria kisa hicho cha Tambaza, mkuu wa shule Marehemu Julius Mushi alishindwa kabisa kuyakamilisha maamuzi yake kwa kuogopa kombati zile na vyeo vile wakati ule.



Mwalimu Mushi alikuwa msomi mwenye shahada ya ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) lakini kombati zile na vyeo vile vilimtisha na hata fimbo sita hawakuchapwa, japokuwa kamati ya shule iliamua hivyo. Binafsi nina amini kama ndugu yule angefika shuleni Tambaza na mavazi ya kawaida wanafunzi wale 20 lazima wangechapwa viboko sita kama maamuzi ya kamati ya nidhamu. Fikiria kama msomi mwalimu Mushi aliogopa vyeo vile na mavazi yale mwanakwetu sembusu akina pangu pakavu tia mchuzi?

Pili hivi sasa JWTZ imesisitiza juu ya wale wenye sare zao kuzisalimisha mara moja vinginevyo mambo yatakuwa balaa. Mwanakwetu anakubaliana na dhana hiyo ya watu wasio wanajeshi hawapaswi kabisa kuzisogelea sare za ndugu zetu hao. Mwanakwetu anashauri JWTZ kazi hii ya kuwafuatulia wenye sare hizo ifanywe na Jeshi Polisi Tanzania maana lina uwezo wa kuwadhibiti ndugu hao.

 

Tatu Mwanakwetu anayakumbuka majukumu ya msingi ya JWTZ ambayo ;

Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ulinzi wa Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kufanya Mafunzo na Mazoezi ili kujiweka tayari Kivita wakati wote, Kufundisha umma shughuli za Ulinzi wa Taifa, Kushirikiana na Mamlaka za Kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa, Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani Kimataifa.”

Ambapo sasa hivi mijadala mingi kwa Watanzania mitaani na mitandaoni wanatamani JWTZ kukabidhiwa bandari waendeshe ili kuondoa wizi bandarini .

Mwanakwetu upo?

Mwanakwetu anaamini kama hilo litakubaliwa basi JWTZ watakuwa wanatekeleza majukumu yao mawili ya msingi ambayo ni,

“Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).”

Mwanakwetu anatamani sana kama JWTZ sasa wafikirie juu ya bandari yetu namna ya kuweza kuindesha, je vijana wetu watajifunza wapi? Je vinaitajika nini? Kama baadhi ya Watanzania wanatamani hilo je JWTZ liko tayari kwa asilimia ngapi? Nalo suala la sare lingebaki tu kwa Jeshi la Polisi kulifanyia kazi wao ndiyo wanaoshughulikia usalama wa raia kwa mujibu wa sheria.

 Nakutakia siku njema.

 makwadeladius@gmail.com

0717649257



 


0/Post a Comment/Comments