Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu aliamka kitandani kwake saa 12.15 ya asubuhi na
kubaini kuwa amechelewa misa ya kwanza ya Dominika ya 20 ya Mwaka A wa Liturjia
ya Kanisa Agosti 20, 2023, muungwana huyu aliamka akavaa haraka haraka na saa 12.19
alikuwa amefika Kanisa la Bikira Maria, Malkia wa Wamisionari , Parokia ya Malya
,Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
Akiwa katika mandhari ya kanisa hilo,taa za ndani ya kanisa hazionekani
kuwaka, bali giza tele, isipokuwa nje taa moja tu ya mbele ya kanisa hilo, hapo
akakutana na vijana wawili wakimwambia kaka vifungo vya shati lako vya juu umevigeuza
vifunge vizuri, hapo Mwanakwetu alifanya hivyo na kuwashukuru mno hawa
ndunguze, haraka haraka imesababisha vifungo vya shati kupishana.
Kwa kila dalili misa ya kwanza inayoanza sa 12. 00 haikuwapo
jumapili hii na hata alipouliza vijana hawa walijibu kuwa na wao wamefika hapo
wanashanga hakuna misa.
Mwanakwetu aliwaaga vijana hao na kurudi nyumbani kwake
kulala, kweli alilala hadi saa 2. 20 ya asubuhi na kuamua kufanya shughuli za
nyumbani kwake, alafu akaondoka na kurudi Kanisa kwa mara ya pili, alipofika
hapo alikutana na mfanyabiashara wa bizaa za dini ya Kikristo kama vile Biblia,
Katekisimu, Misale ya Waamini , rozali na Chuo Kidogo cha sala. Jamaa huyu
alikuwa na bizaa nyingi ambayo ilijaza eneo kubwa alipozilaza bizaa hizo ambapo
yalikuwa mataji mekundu na meupe.
Mwanakwetu akamsalimia alafu akamuuliza jamaa huyu bei ya mataji
mekundu na meupe, akaambiwa alafu akamuuliza huyu jamaa juu ya misa ya dominika
hii inaanza saa ngapi?.
“Juma hili zima Mhashamu, Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande
yupo Parokia ya Malya, kwa leo anatoa Kipaimara kwa vijana wetu kama 100 na misa
ni saa 4.00 ya asubuhi, leo tuna mis amoja tu, Kaka kwani wewe haufahamu hilo?”
Mwanakwetu alijibu kuwa ndiyo
hafahamu, maana hakuwepo katika Viunga vya Parokia ya Malya kwa majuma kadhaa,
jamaa akasema hakuna neno.
Mwanakweta alirudi nyumbani kwake, alikaa
na kufanya shughuli zake zote na saa nne kamli alikuwa Kanisani hapo na kubaini
kuwa ni kweli Mhashamu Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande yupo na anaongoza
adhimisho la Misa Takatifu ambayo itatoa Kipaimara, macho ya Mwanakawetu ndani ya
kanisa hili mabechi ya mbele, mkono wa kushoto wa altare walikaa vijana waliokuwa
wanapewa Kipaimara.
Misa ilianza na maneno ya utangulizi
ya Mhashamu Baba Askofu Mkuu Nkwande,
“Kwa mazingira haya, unaweza kuamini kumbe hata utumwa unaweza
ukarudi, unamuweka mtu katika lango la nchi yetu ! Akakaa pale, kukatokea shida
hapa ndani akachukua upande mmoja wa mgogoro huo hali itakuwaje? Nchi jirani na
sisi tukapata nayo shida, naye huyu jamaa akachukua upande mwingine itakuwaje? Tumuombe
Mungu ili wanasiasa na mtu yoyote yule katika uongozi wasikilize maoni ya wengi…Tusikabidhi
usalama wetu kwa watu. Wale waliosoma Historia wanakumbuka baadhi ya viongozi
wetu wa zamani walishirikiana na wale waliokuwa wakifanya biashara ya utumwa
wakawauza wenzao kwa malipo ya nguo, shanga na vitu vingine vidogo vidogo. Tunapaswa
kusaIi na tunapaswa kumwoomba Mungu ili tuepukana na majanga kama hayo. Tujute dhambi zetu…Nakuungamia Mungu
Mwenyezi…”
Mwanakwetu misa hiyo inaendelea na masomo
yote kusomwa vizuri; mawili la kwanza na pili walisoma wale wanaopata Kipaimara
na Injili ilisomwa na Padri Samson Masanja ambaye ndiye Paroko wa Parokia hii,
baada ya somo la injili Mhashamu Baba Askofu Mkuu Nkwande alisogea mbele ya marufaa
ya Kanisa hili la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari na kutoa mahubri ya misa
hii. yaliyokuwa ya uwazi bila kufichana mambo.
“Mama Kanisa katika jumapili ya leo anasema kuwa wokovu upo
kwa watu wote na hata nyakati hizo Waisraeli walikuwa ndilo taifa linalotahiri
tu na mataifa mengine walikuwa ni wapagani, hawa wapagani hawakuwa na agano
hilo la tohara na Mungu, walitazwamwa kama ni watu wa kupotea tu,-wakwenda motoni,
Kristo analeta mageuzi katika hilo. Mwanadamu kwa desturi amekuwa ni mtu wa
kujifinyangia vitu na kuviabudu, msifanye hivyo. Watu wanaweza wakajichongea
umaarufu ukawa ndiyo Mungu wake, wengine ukatili ukawa ni Mungu wake, wengine
uzinzi–utasikia mimi ni mwanaume na hata wengi sasa mali inakuwa ndiyo
Mungu wake. Mtu anajifanyia haya kuwa Mungu na bila ya hayo mambo maisha yake
hayaendi. Sasa watu wanajivunia dhambi, tusijivunie dhambi hilo siyo sahihi.”
Mahubiri haya yanaendelea huku kanisa
hilo lilikuwa kimya, labda nyuma ya benchi alilokaa Mwanakwetu ilisikika sauti
ya mtoto aliyekuwa akiuchezea mwamvuli kwa kuuburuta na wakati mwingine sauti
ya mtoto huyu ikisikika akimuita mama yake aliyekuwa naye kando yake.
Mbele ya Altare ya Kanisa hili kukiwa
na mashemasi watatu, Padri mmoja na Askofu Mkuu Mmoja.
“Mjitahidi kutenda haki katika familia zenu, kutenda haki kwa
kila mzazi kwa familia na watoto wake, kutenda haki huko ni pamoja kutokuonesha
matendo mabaya mbele ya watoto hao, kutowakwanza watoto hao. Mzazi Imara huona
aibu kuonesha tabia zake mbaya, hawezi kulewa na kuangauka mbele ya watoto wake
na hata watoto wa wengine, ‘Baba unalewa wee, alafu unaanguka mitaroni!’ Tunaambiwa,
‘twendeni tukatende haki, maana wokovu wake uu karibu kuja, tuishi kitakatifu,
tusikwaze watu, maana mwenyezi Mungu yu karibu kuja, Bwana wetu Yesu Kristo
anatuambia kuwa hakuna anayejua muda wala saa atakayokuja mwana wa adamu.’ Katika
injili ya leo Miji ya Tiro na Sidoni ilikuwa ni miji ya mataifa siyo miji ya
Israeli, hii ilikuwa ni miji ya wapagani. Yesu anakutana na mama huyu wa Kipagani
ambaye alikuwa anamcha Mungu sana, lakini hata katika upagani wake na hata katika
dhambi zake alimlilia Yesu juu ya pepo yule kwa bintiye, majibu ya awali ya
Mitume na Yesu yalikatisha tamaa lakini mama mpagani hakukata tamaa, ‘Ni kweli
basi, hata mbwa hula makombo ya mezani yaliyoanguka katika meza ya bwana wake.’
Yesu akasema mama Imani yako imekuponya.”
Mahuburi hayo ya Mhashamu Baba Askofu
Mkuu Nkwande yalitumia karibu dakika kumi na alipofika dakika ya nane kwenda ya
tisa alimalizia kwa kusema haya,
“Tuliombee na taifa letu katika mahangaiko haya linaloyapitia,
lisije likateketea, tusije tukakuta tumezidi kugawanyika, maana tumegawanyika
katika kitu ambacho hatukupaswa kugawanyika. Tunapaswa kubakia imara, watu wa nje
wasitugawe, Sisi ni kitu kimoja, kama kuna wenzetu tumewaona wanataka
kutupeleka kubaya, tujifunze kusema hapana, tujifunze kusema no hata kwa kimombo.”
Mhashamu Baba Askofu Renatus Nkwande
alitoa Kipaimara na mwishoni mwa misa hii lilisomwa tamko la Baraza la Maaskofu
Katoliki(TEC) dhidi ya makubaliano na kuendesha Bandari ya Dar es Salaam baina
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya DP World ya Emirate
of Dubai, awali Baba Askofu akisema kuwa nayeye ni miongoni mwa wale Maaskofu
37.
Baadaye Baba Askofu alipokea zawadi
kadhaa kutoka Parokia ya Malya, ambapo alisema anashukuru kwa zawadi hizo
zikiwapo pesa Taslimu shilingi milioni 4 zitakwenda kugharamia mafunzo ya
mashemasi saba wanaosoma nje ya Tanzania.
Misa hiyo ilipomalizika Mwanakwetu
alianza kurudi nyumbani kwake akijisemea moyoni japokuwa waliopata Kipaimara walikuwa
karibu vijana 100, Mwanakwetu hakuwa na mwaliko hata mmoja, akisema moyoni kuwa
Wasukuwa siyo wachoyo labda ugeni wake hapa Malya Kwimba , mkoani Mwanza ndiyo
unamponza maana yeye bado ni kuku mgeni. Huku mawazo mengine yakimjia kuwa na yeye
hajafanya sherehe awaalike Wasukuma wa Malya.
0717649257
Post a Comment