WASUKUMA NA ZAWADI YA NAZI

 

Adeladius Makwega-MWANZA

Maisha baina ya jamii ya Wasukuma na jamii za Pwani yana simulizi ndefu ambazo hata kama zikiandikwa na kusimuliwa zinaweza zisiishe, japokuwa simulizi chache mno zimeandikwa.


Mwanakwetu leo anakuomba msomaji wake kwa heshima na taadhima zote akusimulie simulizi mojawapo ambayo iliandikwa mwaka 1970 na ndugu S. Kazi ambaye alifanya utafiti juu ya maisha baina ya Wasukuma na na makabila ya Pwani .

Ndugu S Kazi anabainisha kuwa mawasiliano baina ya Pwani na Bara ni ya miaka mingi, huku yakipitia hatua mbalimbali, tangu kutembea umbali mrefu kwa miguu na kutumia wanyama kama punda ambapo safari hizo zilitumia miezi mingi hadi Wasukuma kufika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Hali ya usafiri ilikuwa ya nafuu baada ya Mjerumani kujenga reli ya kati ambapo usafiri wake ulikuwa mwepesi na wakati huohuo kulikuwa na ujio wa motakali(magari ya mota).

S Kazi anasema kuwa watumishi wengi katika gari moshi na vituo vyake vilivyotapaka tangu Pwani hadi Bara walikuwa makabila ya Pwani wakiwamo Wazaramo , Wakwere , Waruguru, Wapogoro, Wandengeroko na mengine.

Mjerumani aliwahusudu hawa jamaa kwa sababu kadhaa ikiwamo ujanjaujanja, kufahamu lugha nyingi na pia kuwa wajuzi wa Kiswahili.

Msomaji wangu leo Mwanakwetu hataki kuzungumzia mahusiano baina ya Wasukuma na makabila ya Pwani wakati wa Wakoloni bali anazungumzia kabla ya ugeni huo.

Ndugu S Kazi anasema kuwa siku moja Wasukuma walikwenda Pwani wakauza walivyobeba na kununua walivyovitaka , wakaifunga mizigo yao wakijianda kurudi Usukumani.

Wakati wanataka kurudi kwao Bara, Wazaramo walimpa zawadi mkuu wa msafara wa Wasukuma na zawadi hiyo ilikuwa ni mzigo wa NAZI kavu zilizokwisha fuliwa. Walipouliza zawadi hii inatumikaje Wazaramo walimpa maelekezo yao msaidizi wa mkuu wa msafara wa Wasukuma,

Mzigo wa zawadi hiyo ulifungwa vizuri na wapagazi wa Kisukuma wakabeba zawadi yao kigulu na njia hadi Usukunani.

Walipofika mzigo huo wa NAZI ulifunguliwa na wale waliambatana na Mkuu wa Msafara wakagawawiwa kila mmoja NAZI mbili mbili ili wakatazitumie majumbani mwao.

Msaidizi wa Mkuu Msafara huo aliyepewa maelekezo na Wazaramao ya namna ya kuitumia NAZI hizo aliwaambie wenzake,

“Unachotakiwa kufanya ni kukoka moto, unauwasha, unauweka chungu chenye maji mekoni na unaiweka nazi hiyo katika chungu chenye maji kama ilivyo, Nazi itachemka kwa muda mrefu hadi itaiva na NAZI itakuwa tayari kuliwa kama KIAZI, ni tamu sana.”

Wale wote waliotoka safari ya Pwani waliyapokea maelekezo hayo na kurudi majumbani mwao na kuwapa maelekezo hayo wake zao na shughuli yakuipika NAZI ilianza.

Kumbuka msomaji wangu katika mila za Kiafrika zawadi huwa inakuwa ni kitu cha kwanza kufunguliwa na kuliwa,  kwa hiyo kila aliyepewa zawadi ya NAZI alipofika nyumbani kwake kuipika NAZI lilikuwa jambp la kwanza.

Wanawake wa Kisukuma walipokea maelekezo ya kupika NAZI vizuri, pika pika na wewe ya NAZI  ikaanza , akina mama wa Kisukuma kila walipobonyeza NAZI hiyo ilikuwa bado ngumu, waliongeza maji na kuweka magadi NAZI bado ilikuwa ngumu, kuni zilichochowa weee mapishi yaliendelea ili waweze kula zawadi hiyo kutoka Uzaramoni lakini wapi NAZI hakuiva .

Wanawake wa Kisukuma kuwaambia waume zao NAZI haiivi kwanza ilikuwa aibu, maana huko ni kushindwa kutekeleza majukumu yao kama wanawake.



Akina mama wa Kisukuma kwanza waliulizana wao kwa wao majibu hayakupatikana hata mmoja NAZI hiyo kuiva. Hapo ndipo jambo hilo lilikwenda kwa waume zao.

Wasukuma wakatambua kuwa Wazaramo wamewachezea mchezo, hapo tayari Wazaramo walikuwa wameshawazidi kete Wasukuma. Wasukuma walikasirika mno lakini safari ya kutoka Bara hadi Pwani ni ndefu sana njiani hasira zinaweza kukuishia, lakini Wasukuma wakawa wanajipanga namna ya kulipiza kisasi.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini ?

Unaweza ukapewa zawadi vizuri tu na ukaifurahi mno hiyo zawadi, hoja si kupewa zawadi bali la msingi ni yale maelekezo yanayotolewa je yatakuwa sahihi? Unaweza kupewa kitu cha thamani kubwa lakini maelekezo yakewa siyo sahihi na kile kitu cha thamani kisiwe na manufaa kwako hata kidogo.

Mwanakwetu upo?

Nakutakia Siku Njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257





 

 

0/Post a Comment/Comments