HAWAWEZI KUWAAMINI KWA LOLOTE NA CHOCHOTE


Adeladius Makwega-MWANZA

Kuna muungwana mmoja kampigia simu Mwanakwetu akimwambia kuwa  kunafanyika uzinduzi wa maktaba ya  kigitali ya mhe Dkt. Salim Ahmed Salim. Mwanakwetu alijibu kuwa hafahamu kitu katika hilo.

Mazungumzo haya yalikuwa marefu sana juu ya kiongozi huyu aliyeshika nafasi kadhaa za  Kitaifa na Kimataifa.

 

Katika mazungumzo hayo Mwanakwetu alimwambie nduguye huyu kuwa yeye anamuheshimu sana mwanasaiasa huyu kwa mambo makubwa matatu.

Ndugu  huyu alitamani kuyafahamu mambo hayo.

Kwanza kabisa ni maisha ya mwanasiasa huyu na mkewe Bi Amne Ahmed Salim.

‘Katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, Zanzibar ilikuwa na mahusiano mazuri na makubwa na KUBA(CUBA). Vijana wengi wa Kizanzibar iwe katika vyombo vya ulinzi au wasomi walipata mafunzo mafunzo huko KUBA. Mafunzo haya pia yaliwakaribisha raia wengi na wanasiasa wengi wa  KUBA kufika Zanzibar. Miongoni mwao ni Dkt.Ernest Che Guvera. Kipindi cha uhai wa  Che Guvera  aliwahi kuingia Tanzania kwa namna mbili tofauti kwanza kwa jina lake na wakati mwingine kutumia majina bandia na hata nambali za lugha Kiswahili akigawana na wenzake moja, mbili na TATU. Safari ya majina yaabandia ya Che Guvera ilikuwa hasa  pale alipoelekea Zaire ambapo KUBA walikuwa wakimuunga mkono  marehemu  Laulence Kabila baada ya kifo cha Patrice Lumumba.

Che Guvera ailiwahi kukaa Tanzania katika maeneo mawili tafauti,  kwanza ni kwenye nyumba zinazotazamana na Gereza la Ukonga kama unakwenda Pugu nyumba za vigae na makazi yake ya pili yalikuwa ndani ya ubalozi wa KUBA  Dar es Salaam pale Upanga, ambapo alipewa chumba kidogo  na alikaa kwa siri na baadaye mkewe alikwenda katika makazi yake hayo akitokea KUBA.

Kabla ya safari hizo juu ,Che Guvera alifika Dar es Salaam na kukutana na viongozi kadhaa wa ukanda huu na alipotoka Dar es Salaam Che alifika Zanzibar na huku alikutana na viongozi kadhaa akiwamo Dkt Salim Ahmed Salim.

 Akiwa Zanzibar ya Che Guvera ailfika nyumbani  kwa Dkt Salim Ahmed Salim na   kupikiwa ugali na  mke wa  Dkt Salim -Bi Amne na kula chakula hicho hapo hapo na baadaye Che Guvera  aliondoka zake na kurudi  Dar es Salaam na mwisho kurudi KUBA.’

Katika maisha ya Dkt Salim Ahmed Salim na mkewe Bi Amne unamuona tangu awali yeye na mkewe. Balozi wa Tanzania nchini Misri, pale Cairo.akiwa  OAU Adis Ababa, na hata pale Zanzibara Che Guvera anakula ugali BI Amne anaonekana.

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anaongea na simu na akamwambia huyu ndugu kuwa Dkt Salim Ahmed Salim ni mtu wa familia.



Taswira ya Dkt. Salim Ahmed Salim pale ofisi ndogo ya chama.

Mwanakwetu akamwambia ndugu huyu kuwa yeye alisoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja-Ilala  ambayo ipo kando na Ofisi Ndogo ya CCM jijini Dar es Salaam.   Wanafunzi wa shule hii walikuwa wakitumiwa sana kama Chipukizi wa CCM au shule ya kuokoa jahazi kama kuna ugeni mkubwa wa gafla unafika hapo.

‘Haya  darasa la Tano D , sita  D na saba D nendeni ofisi ndogo ya chama sasa hivi mtapewa  maelekezo.

Kwa hiyo wanafunzi hao kunharisha masomi kwenda kumpokea mgeni hilo lilikuwa jambo la kawaida mno. Ndiyo kusema kuwafahamu viongozi wa kitaifa wa Tanzania  kwa kuwaona moja  kwa moja kwa macho ililikuwa ni jambo la kawaida sana .

Mwanakwetu anakumbuka akiwa Darasa la tano mkondo D, darasa lao lilikuwa ndilo darasa jirani na mnara wa ofisi ndogo ya CCM. Darasa hilo lilikuwa  juu kidogo huku Ofisi Ndogo ya Chama na mtu akiwa chini  anaingia unamuona. Mara nyingi  wanafunzi wa darasala la tano D akiwamo Mwanakwetu kama darasa halina mwalimu kiliposikika  King’ora tu  walitoka wote na kuchungulia nje  je hapo Ofisi Ndogo anaingia  nani?

Siku moja kulikuwa na ugeni, king’ora kikalia wanafunzi hao wakatoka kuchungulia wakamuon akiongozi anashuka.

Mwanafunzi mmoja  wa  darasa la tano D akasema,

Saliiiiim…. na wenzake wakaitikia… Ahmed Salim.

Tukio hilo lilileta tabu kidogo na Mkuu wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja wakati huo  Mwalimu Mtolela alifika hapo darasani na alitoa adhabu ya fimbo nyingi kwa waliofanya hivyo.

Lakini kubwa wanafunzi wa shule hii waliwatambua viongozi hao kwa haiba na wajihi wao kila mmoja bila ya kukosea.

‘Huyu Salim Ahmed Salimu, Huyu Mwalimu Nyerere na  huyu ni Mwinyi’

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu alikuwa anaendelea kuongea na simu na rafiki yake.

Safari ya miguu kutoka Mnazi Mmoja hadi Mbagala.

Mwanakwetu akasema akiwa ia darasa la tano mkondo ule ule D, shule hii ya Msingi Mnazi Mmoja. Siku moja mapumziko ya saa nne alikuwa na shilingi tano mfukoni alizopewa na baba yake, alinunua mihogo ya kukaanga kwa bwana mmoja ambaye alikuwa bahari mstaafu, akifanya biashara hiyo. Shilingi mbili alinunua mihogo miwili na shilingi moja alinunua barafu (Ice Cream) na kubakia na shilingi mbili mfukoni. Eneo la shule ya Msingi Mnazi Mmoja lilikuwa kubwa hadi makutano ya Barabara inayoshuka kuelekea Kisutu na makutano na Mtaa wa Lumumba, kuelekea Sokoni Kariakoo. Katika kona hiyo ndipo muuza mihogo huyu baharia mstaafu alikuwepo.

Baada ya kumaliza kula mihogo na Ice Cream na wenzake, Kengele ililia na Mwanakwetu kurudi darasani. Saa nane kengele ilipigwa ya kurudi nyumbani ambayo yenyewe ilikuwa hawakai mstarini, bali ni kuondoka tu. Katika wanafunzi waliokuwa wakikaa mbali na shule hii mmoja wapo alikuwa ni Mwanakwetu.

Sihlingi mbili iliyobaki katika matumizi ya mapumziko yale ilikuwa ni ya nauli ya kutoka Mnazi Mmoja hadi Temeke, alafu shilingi nyengine kutoka Temeke hadi Mbagala, hiyo ikiwa ni nauli kwa mwanafunzi.

Mwanakwetu alikuwa na rafiki yake mmoja aliyekuwa akifahamika kama Alexzander(Huyu ni kaka wa damu wa mwanamuziki Chege Chigunda) ambaye alikuwa akikaa Kurasini jirani na Chuo Cha Ualimu Chang’ombe. Siku hiyo wakiwa wanaelekea Stendi ya Mnazi Mmoja, Mwanakwetu ndipo alibaini kuwa ameangusha pesa yake ya nauli yaani zile shilingi mbili. Alishindwa cha kufanya, bali akamueleza rafiki yangu Alexzander kilichotokea.

Naye Ndugu huyu alimwambia

‘Hilo halina neno, basi leo tutatembea kwa mguu kutoka Mnazi Mmoja hadi Kurasini, alafu nikifika kwetu nitakugaia (nitakupa) shilingi moja yangu ili ukapande basi Mtoni Azizi Ali ili uweze kufika nyumbani kwenu Mbagala’.

Kweli tulitoka zetu kwa mguu tukaambaambaa na Mtaa wa Lumumba, hadi Gerezani, tukapita Mtaa wa Mafia tukaibuka na Msimbazi. Hapo tukavuka makutano ya KAMATA tukaanza na Barabara ya Kilwa, tukatembea kidogo tukavuka hadi katika Viwanja vya Mpira wa Netiboli  Reli Gerezani.



Ndugu Alexzander akasema,

‘Kazimbaya, muda bado, twende tukaangalie kinachoendelea ndani ya uwanja huo maana mbona kuna kelele nyingi za kushangilia?’

Wakiwa nje ya uwanja huu, huku magari yakipita kuelekea Kurasini na Mbagala, walichungulia getini na walikaribishwa na milio ya filimbi za mchezo huo, huku sauti za kike zikisikika zikiyataja majina ya wadada wanaocheza mpira wa Netiboli.

…Halima, Jane, Anna, Rose, Pili Amina na Latifa.’

 Mithili ya mwalimu anayewaita wanafunzi majina darasani

Walipenya getini, wakati geti linamfungulia kwa ajili ya Mgeni Rasmi ambaye alikuwa Salim Ahmed Salim ambaye walikuwa wanamfahamu sana, lakini hawakutambua cheo chake. Alexzander na Mwanakwetu walipoingia getini walikuwa wamevaa sare mlinzi alichukuia na aliwakaripia tu na yeye kuendelea na kazi yake Ukolokoloni hapo Reli Gerezani.

 Wakiwa pale Mwanakwetu alivutiwa mno na wachezaji wa mchezo huo namna walivyovalia jezi zao ambazo zilikuwa na vifupisho vya herufi kadhaa. Ndugu Alexzander ambaye alikuwa anaishi jirani na Polisi Kurasini alikuwa akiufahamu mchezo huu huku akimwambia Mwanakwetu,

 

C ni mchezaji wa kati(CENTER) ambaye anacheza popote isipokuwa katika mzunguko duara la goli tu. GS akiniambia ni (GOAL SHOOTER) huyu ni mfungaji.GK (GOAL KEEPER) mlinzi wa lango, GA aliniambia (GOAL ATTACK) anapeleka mashambulizi golini, WA ni mshambuliaji wa pembeni (WING ATTACK), WD aliniambia ni mlinzi wa pembeni (WING DEFENCE) na GD ni mlinzi ambaye analinda hata lango la goli.

Jezi hizo zilikuwa na blauzi zenye mikono mifupi na sketi fupi sana ambazo zilimvutia mno namna walivyokuwa wakiruka juu wakiwa angani, zikipepea kama bendera mlingotini kana kwamba mchezaji wa ngoma za asili aliyevalia kibwaya. Huku chini wakiwa wamevalia viatu kama laba hivi ambazo ziliwasaidia kuweza kukimbia katika kiwanja hicho kilichokuwa kimejengwa kwa sakafu. Japokuwa siku hiyo Mwanakwetuhakuona mchezaji hata mmoja akidondoka.

Huku mtazamaji Mwanakwetu akijiuliza je wakianguka itakuwaje?

 Alexzander alimwambia Mwanakwetu kuwa dawa zipo maana kwa chonjo alioneshwa jamaa na sanduku lake la msalaba mwekundu.

“GK-GS, WD-WA, GD-GA, C-C, GA-GD, WD-WA na GK–GS Hivyo ndivyo wanavyocheza kwa kukabana kila mmoja na mwenzake.”

Alisema rafiki yake Alexzander-rafiki wa Mwanakwetu amabye alijfunza mchezo huo Polisi Kurasini. Baada ya dakika kadhaa walibadilishana magoli na Mwanakwetu alimwambia rafiki yake kuwa yeye anakwenda Mbagala na ni mbali sana tuondoke zetu. Kweli walitoka na kuendelea na safari yao ya kuunga mkono azimio hadi Kurasini. Hapa ndugu yAlexzander alifika kwao na kubadilisha nguo na kumsindikiza Mwanakwetu hadi kambi ya Jeshi la Wananchi Kambi ya  Twalipo huku akimkabidhi shilingi moja ya kwenda kupanda basi Mtoni Azizi .  Alipofika Aziz Ali akapanda zake basi la UDA za Temeke- Kongowe hadi Mbagala 77 aliposhuka.

Alipofika nyumbani tu huko akiulizwa mbona leo unaingia usiku wakati shule nimetoka mapema? Alieleza kilichotokea lakini alificha kama alipita kutazama mpira wa Netiboli pale Reli Gerezani ambapo walimuona mhe Dkt. Salim Ahmed Salim. Ambaye walikuwa wakimfahamu vizuri maana bakora za Mwalimu Mkuu Mtolela walizikumbuka mno.

Hapo hapo simu ya bwana mkuu huyu aliyempigia Mwanakwetu ilikata.



Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Msomaji wangu kumbuka sana bakora sita za wanafunzi wale darasal Tano D  kwa kumuita  kiongozi huyu, hiyo maana yake Dkt Salim Ahmed Salim ni mtu watu hata watoto wa wadogo wa wakati huo walimfhamu na walimpenda. Hao watoto wadogo wa wakati huo leo hii  ndiyo wanamuandikia makala makala haya mzee wao.

Pia msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu na Rafiki yake Alexzander waipoingia  viwanja vya Reli Gerezani walimuona Kiongozi huyu akiwa Mgeni Rasmi katika mashindano ya Netiboli, ndiyo kusema Dkt Salim Ahmed Salim alikuwa kiongozi mpenda michezo.

Tatu na mwisho kabisa  Dkt . Ernest Che Guvera alipofika Tanzania nyumba ya mwanasiasa  huyu aliingia na kupikiwa ugali na kula.

Jiulize msomaji wangu katika hilo hajatajwa kiongozi yoyote wa wakati huo kuwa  Che Guvera alikula kwake  bali ni  Dkt Sakim Ahmed Salim pekee na hapo hapo jina mkewe Bi Amne linaonekana.

Kwa hakika maisha ya Dkt Salim na mkewe Bi Amne yametenganishwa na kifo tu, ndiyo kusema  tunapoandaa lolote lile la Dkt Salim Ahmed Salim Mwanakwetu anaomba tumkumbuka na Bi Amne.Kama alivyofanya Che Guvera ambaye alionana na Dkt salim vikaoni lakini aliamua kwenda kumsalimu nyumbani kwake, huo ukiwa ni udugu wa hali ya juu.


Hapo linatolewa funzo kubwa kuwa siasa siyo uadui, siasa inatakiwa kujenga udugu maana kama wnasaiasa hamna udugu kwa kweli ,hamuaminiani  je wananchi wa kawaida Hawawezi Kuwaamini kwa Lolote na Chochote.

Mwanakwetu upo?

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 



0/Post a Comment/Comments