MWANAKWETU OFISINI KWA PROFESA SARUNGI


Adeladius  Makwega-MWANZA

Katika maandishi ya Mwanakwetu juu ya Mgogoro Baina ya Azania na Tambaza sehemu ya XLIV yaliyoandikwa Mei 11, 2022 kulikuwa na nukuu hii.

.....................................................................................................................................................

“Shangazi wa kariakoo Salome Makwega akawauliza wale wale maafisa elimu, rafiki wa dada yake Honesta Makwega, wakamwambia kuwa hapa jiji tumeshalimaliza suala hilo, hoja ni kwa Mkurugenzi wa Shule za Sekondari nchini, fuatilieni hilo huko.

 

Lakini kwa sasa barua ndiyo zinapelekwa, pumzikeni hata juma moja alafu kijana aende.Nikaelekezwa niende Wizara ya Elimu wakati huo ipo Magogoni, nimuone mama Makuhana , yeye alikuwa ni Msaidizi wa Waziri wa Elimu.

Juma moja lilipita, Mwanakwetu akaingia wizarani, akaandika jina katika kitabu cha wageni na kuingia katika ofisi ya Waziri wa Elimu. Alipofika hapo akapokelewa kwenye chumba, akaambiwa unapotaka kuingia kwa waziri unatakiwa kukaa katika mabenchi haya, alafu mtakuwa mnaingia mmoja mmoja, kwa zamu.

 

Alikaa katika mabenchi hayo, kukiwa na watu wengi na palikuwa na mabenchi matatu yaliyopangwa kwa mtindo wa herufi U yaani moja kulia, moja kushoto na moja ukutani.Mwanakwetu alikuwa mtu wa mwisho kabisa kwenye pembe ya U na wa kwanza alikuwa kwenye pembe ya herufu U ya upande mwingine.Mabenchi yote yalijaa watu, mara wakaja watu wengine wawili wakakaa nyuma ya Mwanakwetu hapo tena yeye hakuwa wa mwisho .

Mara akawa anatoka mzee mmoja mrefu sana, mwembamba mno, amevaa shati jeupe sana na suruali nyeusi,akiwa na upala kava tai ya mistari miyeupe na miyeusi. Anawachukua watu wanne. Mtu mmoja mmoja, wa kwanza kutoka katika kila benchi la kulia na kushoto alafu anachukua watu wawili kutoka bechi la ukutani wa kulia na kushoto, anaingia nao ndani.

Kwenye benchi zile tatu palikuwa na watu aina tofauti lakini wote walikuwa na umri mkubwa isipokuwa Mwanakwetu peke yake. Watu hawa wakawa wanasema,

 

‘Huyu ndiye Waziri wa Elimu, anatoka mwenyewe, anatuchukua wageni wake, anakwenda kutusikiliza ndani, anaitwa Profesa Philenon Sarungi, huyu ni dakitari wa binadamu, alikuwa Muhimbili na hata huko alikuwa anafanya kazi vizuri sana.Yeye ni dakitari bingwa wa kuunganisha mifupa, ni Msabato na mkewe ni Mzungu.’

 

Muda unasonga, watu wanachukuliwa wanne kwa wane, wanaingia ndani kusikilizwa.Mazungumzo katika benchi hilo yanaendelea

 

‘Kama Ali Mwinyi angekuwa ana mawaziri kama hawa wanne, basi Tanganyika ingekuwa mbali sana.’

 

Hapo Mwanakwetu aliona muda mwingine wanafika wasaidizi wake wanawachukua watu wanne wanne na kuingia nao ndani na kuwasikiliza.

 

Hapo Mwanakwetu aliona Waziri huyu mbinu hii alitumia kuwaona watu wengi mno na kujenga udugu baina ya serikali na wananchi wake. Hapo Mwanakwetu ana miaka 17 kuelekea 18 na ndiye alikuwa mdogo kuliko wote ofisini kwa Waziri huyo siku hiyo.

 

Njia ile ilikuwa na tija mno, ilikuwa ni sayansi ya pekee yake, sijawahi kuiona tena tangu mwaka 1994 katika ofisi yoyote iwe ya umma au binafsi. Binafsi ninadhani Profesa Sarungi mbinu hii aliitumia akiwa Daktari Muhimbili, kuwaona wagonjwa wengi akishirikiana na madaktari wenzake wakati huo

.

Ikafika zamu ya Mwanakwetu, hapo Profesa Sarungi akaja akamshika mkono Mwanakwetu, wale wakubwa akawaingiza ndani ya ofisi yake akainama chini akisema,

 

‘Mwanangu unashida gani ?’

 

Hapo tupo kwa makarani wake.Vipi mwanagu mbona unachafua zulia la Waziri wa Elimu kwa vumbi ? Akisema kwa sauti ya chini na upole sana kwa utani, zulia hilo lilikuwa jekundu. Wale makarani wa waziri wanamtazama Mwanakwetu kusubiria jibu lake.

 

Akauliza unaitwa nani? Mwanakwetu akajibu ?Unashinda gani? Akajibu.

‘Mimi ni wale wanafunzi wa Tambaza, nimeambiwa nije kupangiwa shule.’

Mwanakwetu akampa barua ya jiji akaisoma kwa haraka sana, ikiwa imesainia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo mhe. Ditopile Ukiwaona Radhamani wa Mzuzuri.

Hapo Mwanakwetu hakumtaja tena Mama Makuhana.

Profesa Sarungi akauliza, wewe ulikuwa kidato cha ngapi? Mwanakwetu akajibu cha tatu. Sasa ulipaswa uwe kidato cha ngapi? Akajibu cha nne. Akaitwa, Mama Makuhana! Alipofika, waziri akasema,

‘Huyu mwanafunzi wangu wa Tambaza, mwambie Katibu Mkuu mwanafunzi huyu akariri kidato cha tatu na apangiwe shule ya bweni ya umma mara moja’.

Katibu Mkuu wa Elimu nadhani alikuwa Hassan Kenya (Msambaa) kabla hajaondolewa na Rais Mwinyi kwa Fagio la Chuma (Kutumbuliwa) kwa kashfa mojawapo.

Mama Makuhana kwa Katibu Mkuu, akatoka na karani wa Katibu Mkuu hadi Kwa Mkurugenzi Sekondari na kwa bahati mbaya hakuwepo, wakatafutwa maafisa wanaoshungulikia Elimu Sekondari. Hapo sasa Karani wa Katibu Mkuu akamwambia mzee mmoja mwembamba mweupe mrefu, agizo hili ni la Katibu Mkuu na limetoka kwa Waziri wa Elimu, Mkurugenzi wenu hayupo, Mkuu anasema tekeleza haya haraka.

Kwa kando yupo Mama Makuhana.

 

Kumbe huyu afisa mwembamba mweupe ni Mwalimu Julius Mushi ambaye awali alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Tambaza, kabla Tambaza kuhamishwa walimu na wanafunzi wote na shule ya Tambaza kuwa na walimu wapya.

‘Naombeni nishauri mbele yenu na mbele ya mwanafunzi, sasa shule zinafungwa lakini kazi hii tunaifanya leo naomba shuleni akaripoti mwezi wa saba, zitakapofunguliwa shule. Huyu mwanafunzi hakuwa mwanafunzi wa bweni, sisi tutawasiliana na shule hiyo na kumpa orodha ya mahitaji yote, akienda shuleni awe na kila kitu. Mwanafunzi arudi nyumbani na baada ya juma moja aje.’

Alisema Mwalimu Julius Mushi ambaye sasa alikuwa Afisa Elimu Wizarani.Mwanakwetu akaondoka na Mama Makuhana na karani wa Katibu Mkuu.

Mama Makuhana akasema,

‘Siku ukija tena wakikupa barua upitie kwangu mwanangu’.

Mwanakwetu akajibu ndiyo. Akaondoka zake na kurudi Mbagala.

.......................................................................................................



 

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

 

Hilo ni tukio la kweli la mwaka 1994 ndani ya Wizara ya Elimu, bila shaka walio wengi wamefariki dunia walioshuhudia hilo, leo hii Mwanakwetu kwa kuwa alikuwa kijana analikumbusha baada ya kuona kituko katika ofisi za NHIF Oktoba 30, 2023 (saa 3 hadi saa6 mchana) mkoani Mwanza kushindwa kutoa huduma kwa wakati, japokuwa ofisi hii ina watumishi wa kutosha.

Ofisi zetu za umma zikiwa na wateja wengi, inapaswa wakubwa wavue makoti waingie kazini  kuwasikiliza wateja wao.

Malalamiko dhidi ya ofisi yoyote ya umma hayo ni malalamiko kwa serikali, wakubwa katika ofisi zao wasijifungie maofisi kupigwa viyoyozi wakati huduma zinaendelea, nawaomba wajifunze unyapara huku wakizunguka kuona kazi zinavyokwenda wasingoje mafaili tu yawafaute mezani kwao, wafuatilie hatua kwa hatua mzunguko wa utendaji kazi.


Mwanakwetu Upo?

Wakubwa wasijifungie maofisini. Jifunzeni katika kisa hicho cha Mwanakwetu Ofsini kwa Profesa sarungi.Mwanakwetu anamtakia maisha mema yenye heri na afya njema mzee Sarungi. Profesa Sarungi leo hii nakushitakia  kwako kuwa binti yako Maria Sarungi huwa ananichokoza huwa mara zote nakuwa mpole kwa heshima yako .


Mwanakwetu upo?


Nakutakia siku njema.

 makwadeladius @gmail.com

0717649257








0/Post a Comment/Comments