NHIF Kudharau Hati ya Kiapo Haikubaliki

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Oktoba 30, 2023 ni siku ambayo Mwanakwetu ameitumia kutafakari mambo makubwa matatu.

“Bibi mmoja mzaliwa wa Nachingwea alifika Dar es Salaam kwa Mwanaye ambaye ni mwalimu katika shule moja ya msingi wilaya ya Temeke-Dar es Salaam. Bibi huyu alikaa kwa mwanae huku akijiuguza uguza. Bibi huyu alikuwa akipata matibabu yake hapo Hospitali ya Hindu Mandal. Hospitali hii ilikuwa ikimpatia huduma vizuri sana. Kila mara alikuwa akifunga safari kwenda kuchukua dawa zake yeye mwenyewe. Matibabu yake alikuwa akitumia kadi ya NHIF, mwanzoni kwa amani kabisa. Kuna siku bibi huyu akazidiwa sana hivyo akashindwa kufunga safari hiyo ya Hindu Mandal kutokea Mbagala. Hapo ilibidi atumwe kijana kwenda kufuata dawa za bibi huyu. Alipofika hapo kijana aliulizwa maswali akionesha vyeti vya bibi huyu . Mwisho wa siku kadi ya NHIF ya bibi huyu ilichukuliwa na hao NHIF, hadi bibi huyu aende mwenyewe. kijana akarudi nyumbani hana dawa na hana kadi. Bibi huyu akazidiwa sana akiwa ameharibu ratiba za dawa zake, hakula chochote usiku huo na hali yake kuwa mbaya. Kulipokucha mtoto wake aliagiza ngoja atafute namna nyingine majibu atatoa akirudi kazini. Mwalimu huyu akaenda kazini na kuagiza vijana nyumbani wamuhangaikie na akipata pesa jioni hiyo angeweza kununua dawa kwa pesa yake na kabla ya kwenda kuifuata kadi ya NHIF hapo akimaliza mitihani. Mwalimu alienda kazini na jioni hakurudi na dawa. Siku iliyofuata aliporudi kazini hakumkuta mama yake na kujulishwa kuwa aliondoka mapema na kupanda mabasi ya Nachingwea,‘akisema yeye hataki usumbufu kama kufa na afe tu.’ Mwalimu alifunga safari hadi NHIF lakini hakuipata kadi hiyo hadi leo na huu mwezi wa sita, NHIF wakishauri ilipiwe kadi ya NHIF mpya.”

Hilo ni Mosi

“Oktoba 30, 2023 saa 3-20-615 nilikuwa ofisi za NHIF Mwanza kupata huduma ya kuhuisha kadi iliyopotea ya mwenza, nikiwa hapo nilibaini mambo ya ajabu sana yanayofanywa na NHIF. Kubwa kuliko yote kutokuheshimu hati ya Kiapo. Katika taifa la Tanzania na mataifa mengi Ulimwenguni hii Hati ya kiapo inatolewa na Mahakama au Mawakili. Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Heshima ya Hati Kiapo ni kubwa mno.Watu wanakula kiapo na kupata hati hii kuchukulia mikopo ya mamilioni na mabilioni na hata wengine kufungulia makampuni makubwa makubwa.

Hati hiyo kwa lugha ya kawaida ni sawa na maelezo ya mgonjwa yanayotolewa na daktari, anayeweza kuhojiwa juu ya maelezo hayo lazima awe tabibu na tena kwa kufanya vipimo kwa duru ya pili.

NHIF imekuwa haiheshimu hati hiyo na kuagiza wanachama/ wanufaika wake wenye kuhitaji huduma hapo kupeleka nyaraka zingine, kinyume na Hati ya Kiapo. Hilo ni kosa kubwa ambalo NHIF inalifanya kwa makusudi. Hilo ni kosa ambalo halikubaliki na linapaswa kuchukuliwa hatua kali mara moja dhidi ya NHIF. Kingezo cha wateja kufanya udanganyifu hakiwezi kuipoka heshima yake ya kisheria Hati ya Kiapo. Dharau hiyo ya Hati ya Kiapo inasababisha baadhi ya wanufahika/wanachama wa NHIF kutokupata kadi zao kabisa na wakati mwingine kucheleweshwa kadi hizo.Hata wanachama/wanaufaika wengine kuna wakati wanatumia gharama zingine kulipia huduma za matibabu yao huku wanakatwa kila mwezi.”

Hilo juu ni la Pili.


(Hati ya Kiapo ya Mfano)

Mambo hayo mawili yamemkumbusha Mwanakwetu tukio la mwaka 1996 ambapo Jaji Joseph Warioba alipokuwa kazini katika Tume yake ya Rushwa kazi aliyopewa na Rais Benjamin Mkapa, Jaji Warioba alipofika mkoani Iringa yeye na wenzake walikutana tukio la kusikitisha la muuguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa kumnyima huduma mgonjwa aliyepata ajali mpaka ampatie malipo ya shilingi 200 ya bomba la sindano.

Malalamiko hayo kwa Jaji Warioba yaliyotolewa na ndugu wa jamaa huyu aliyepata ajali yalisababisha muuguzi huyu kuchukuliwa hatua kali na mamlaka yake ya nidhamu na taasisi inayosimamia wauguzi Tanzania wakati huo.

Kisa hiki cha Afya ni miongoni mwa visa vingine vingi vilivyosababisha Rais Mkapa kuunda PCB-TAKURU na baadaye kuunda TAKUKURU –PCCB.

Haya Mwanakwetu ameyatafakari mno siku ya leo.



Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Huyu mgonjwa aliyenyima bomba la sindano alikuwa amelazwa tayari hosptalini. Msomaji wangu katika visa hivi viwili vya juu NHIF sasa inamzuia kabisa mwanachama/ mnufaiki ambaye pesa yake inakatwa kila mwezi kupata kadi yake kwa wakati ili akiugua atibiwe.

Mwanakwetu anaona kuwa kosa la muuguzi la mwaka 1996 lilikuwa na nafuu sana maana huyu mgonjwa alikuwa yu tayari hospitalini na aliweza kupata neema kama siyo kwa muuguzi A basi muuguzi B na hata daktari C. Lakini hili la sasa la NHIF kukamata kadi na kudharau hati ya Kiapo maana yake ni kumtoa nje mgonjwa ambaye alikuwa hospitali na kumnyima matibabu kabisa.

NHIF haina mamlaka yoyote ya kisheria kudharau Hati ya Kiapo zinazotolewa iwe na mahakama au hata wakili yoyote anayetambuliwa kisheria.

Kama yupo huyo aliyetoa hilo agizo iwe wazi au kwa siri , iwe kwa mdomo au kwa maandishi achukuliwe hatua mara moja.

NHIF ikumbukwe kuwa yenyewe sasa ndiyo ina miaka 23-24 , lakini mahakama na masuala ya kisheria hayajaanza leo.

Mwanakwetu upo?

NHIF Kudharau Hati ya Kiapo haikubaliki.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



0/Post a Comment/Comments